Na Dkt. Rajabu Mlaluko
KUTOKANA na kukosekana kwa elimu juu ya magonjwa ya macho, baadhi ya watu hufikia hatua ya kupoteza uoni au kuwa wapofu kutokana na ugonjwa wa mtoto wa jicho bila kujua.
Kwa kukosa elimu baadhi ya watu wanahisi na kuamini kuwa, maana ya mtoto wa jicho ni kuwa jicho linapata mtoto, hapana si hivyo.
Ukweli ni kwamba, mtoto wa jicho kwa tafsiri rahisi ya kitaalamu ni ugonjwa wa macho unaosababishwa na lenzi ya jicho kupata ukungu (opacity) na kusababisha uoni hafifu na hata upofu kama mgonjwa asipotibiwa, kitaalamu ugonjwa huu unaitwa ‘cataract’.
Mgonjwa wa mtoto wa jicho huanza kuhisi upungufu wa uoni katika jicho moja au macho yote na kumfanya ashindwe kumtambua mtu akiwa umbali fulani na mwisho kusababisha upofu kabisa. Mtu anaweza kumgundua mgonjwa wa mtoto wa jicho kwa kumuangalia jichoni na kuona kitu cheupe ndani ya mboni ya jicho lake.
Ugonjwa huu huwapata watoto wadogo, vijana na hata watu wazima kutokana na sababu mbalimbali. Sababu zinazoweza kuchangia kupata mtoto wa jicho, ni kuumia kwa kupigwa au kuchomwa na kitu cha ncha kali jichoni, ugonjwa wa kisukari, na kukaa kwenye mionzi (radiations).
Sababu nyingine ni matumizi ya baadhi ya dawa za macho kwa muda mrefu, maambukizi ndani ya jicho au macho (uveitis), uvutaji wa sigara, uzee kuanzia miaka 50 na baadhi ya watoto wanazaliwa na tatizo hili hivyo ni muhimu kuwachunguza watoto macho yao mara baada ya kujifungua na hata kila siku.
Watu wengi wameendelea kuwa vipofu kwa kushindwa kufikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu. Tofauti ya upofu unaosababishwa na ugonjwa wa shinikizo la macho (glaucoma), ugonjwa wa mtoto wa jicho unatibika kabisa na mtu anaweza kuona mara baada ya kufanyiwa oparesheni.
Hivyo, Dkt. Mlaluko kutoka hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya anashauri kuwa watu wawe na tabia ya kufika hospitali/kliniki ya macho kwa ajili ya uchunguzi kuliko kutumia dawa kiholela bila kufanyiwa uchunguzi, mgonjwa wa kisukari anashauriwa kufika hospitali ili kujua kama ugonjwa wa kisukari umesababisha madhara ndani ya jicho (diabetic retinopathy).
Ugonjwa wa mtoto wa jicho unatibika kwa njia ya oparesheni na wala sio kwa dawa za kuweka machoni kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidanganywa kufanya hivyo na hata kuamua kutumia dawa za kienyeji/mitishamba; hii ni hatari kwa afya ya macho. Pia, kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwakamulia maziwa au kuwawekea watoto asali ndani ya macho, hii sio sawa na wala haishauriwi kabisa kitaalamu.
*Mwandishi wa makala hii anapatikana Hospitali ya rufaa ya Kanda Mbeya, anapatikana kwa Simu: +255 753 938 628. Barua pepe: drrajabumlaluko@gmail.com.