Hizi ndio fursa za mazao ya kilimo zinazopatikana Dubai

0
A man picks some green mangoes at Lulu Hypermarket, Khalidiyah Mall in Abu Dhabi. Victor Besa / The National

Na Syd. Chifu Lukwele IV – Dubai, U.A.E

NIKIWA hapa Dubai moja ya changamoto nilizokutana nazo wakati nikihangaika kusaka soko la uhakika la mazao ya Kilimo, mbali na kuwepo soko lisilo na shaka, tumejikuta sisi ndiyo wenye matatizo (na sio wanunuzi); kwani soko la mazao ya kilimo la Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) ni kubwa kuliko uzalishaji wetu.

Waimarati (U.A.E) wananunua kuanzia majani ya kulishia mifugo hadi mboga, matunda, nafaka, na mazao mengine ya kilimo na mifugo.

Nimezuru Ubalozi wa Tanzania hasa Ofisi ya Dubai mara mbili, ambapo Balozi Mdogo Ali Jabir Mwadini na timu yake, wameonesha kufahamu nini hasa maana ya Diplomasia ya uchumi, na wanafanya jitihada kubwa kusaka masoko ya bidhaa za Tanzania, wakati huohuo wakivutia uwekezaji wa wafanyabiashara wa hapa kwenda Tanzania kuwekeza.

Binafsi, timu hii ya wanadiplomasia imenipa msaada mkubwa mno juu ya suala hilo na kunionesha njia ya kupita kulifikia soko. Tatizo lililopo ambalo nimelikuta sokoni, Wanunuzi kadhaa hasa hapa Dubai wanasema kwamba, tunazalisha kwa kiwango cha chini mno kuliko hitajio (tunachozalisha ni kichache na kinachohitajika ni kingi), ingawa chakula chetu kwa kiasi kikubwa kina ladha nzuri na kina uasilia.

Mathalan, nimepewa mifano ya baadhi ya makampuni (majina nayahifadhi) ambayo yamepewa mikataba ya kuleta bidhaa hapa U.A.E, mfano moja ilisaini kuleta majani ya kulishia wanyama, na kutakiwa kila wiki ilete tani 500, baada ya wiki tatu ikaishiwa pumzi (sijui kwa uzalishaji mdogo au kukosa mtaji wa kununua kwa wengine), mkataba ukafia hapo!

Wapo pia waliopewa fursa ya matunda (yakiwemo Mafenesi ambayo huku kwa Fenesi kubwa lenye ubora wa juu kama la kule Kinole kwa Ndugu yangu Mwenyekiti wa Machifu wa Uluguru Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15 linaweza kufika hadi Shilingi Laki Moja) wakajikuta uzalishaji wao wote unashia wiki moja tu, pumzi ikakata!

Kwa hali hiyo tunapoteza soko, wenzetu wa Mashariki ya Mbali na Amerika Kusini wanalidaka japo ladha ya matunda yao si ya kugusa nyoyo kama ile ya matunda ya Choma, Mgeta, Mlali, Nyiachiro, Matombo, Mkuyuni n.k.

Wapo waliopewa soko la uhakika la nyama ya Ng’ombe na Mbuzi nao wakatakiwa kila wiki walete zaidi ya tani 400, pumzi ikakata baada ya muda usiozidi miezi miwili tu, kwani ranchi yao ikakaukiwa, na hakukuwa na mipango kabambe ya kushirikisha wazalishaji wengine, soko likapotea!

Hilo limenisikitisha ukizingatia Mikoa yetu ikiwemo Morogoro wafugaji wanatoleana macho na wakulima il-hali wanaweza kuanzishiwa programu maalum ya kunenepesha mifugo kwa gharama ndogo sana, kuongeza thamani kupitia ranchi zilizoko mkoani hapo, na badala ya kuwa na mifugo mingi, unakuwa na michache yenye uzito mkubwa na thamani kwenye kila kitu kuanzia ngozi, mikia, kwato, mifupa na mbolea (Soko lipo bado linachezewa)!

Pili, Wanunuzi wanalalama kuwa baadhi ya wakulima wetu hawazingatii kanuni za kilimo bora, hivyo kuharibu mazao yao toka yakiwa shambani! Wengine huaribu ubora wa mazao wakati wa uvunaji (kwa kutozingatia taratibu za uvunaji); na wengine huaribu ubora wa walichokivuna katika uhifadhi (vifungashio), yaani aina ya vifungashio na namna ya kuweka kwenye vifungashio.

Wengine uharibu ubora kwenye usafirishaji; yaani namna ya kusafirisha, aina ya usafiri, vifaa vya kusafirishia, upakiaji na upakuaji, na aina ya barabara ukizingatia kuwa barabara za mashamabani nyingi ni sawa na mahandaki ya vita au migodi isiyo rasmi!

Lakini, wengine uharibu ubora wa mazao kwenye uhifadhi usio sahihi kwenye ghala, au kutokuwepo maghala yenye sifa ya kuhifadhi mazao husika; ilhali wengine uharibu ubora kwenye uongezaji thamani.

Yapo mazao yenye ushindani mkubwa kutokana na kuwa na wazalishaji wengi hasa wa Mataifa yaliyowekeza sana kwenye kilimo kama ya Ulaya, Marekani, Amerika Kusini, na Asia ya kati pamoja na Mashariki ya Mbali, na baadhi ya jirani kama Oman.

Usishangae kukuta soko la Dubai, Abu Dhabi na kwingineko hapa U.A.E likiwa limetawaliwa na Tangawizi, Ndimu, Malimao au Vitunguu Saumu toka China, Viungo toka India, Indonesia na Malaysia, Maboga toka Oman, Korosho toka Vietnam na India, Parachichi toka India, Ndizi Mbivu toka Ecuador, Shelisheli toka Brazil, Majani ya kulishia Mifugo toka Kenya, Unga wa Mahindi au Ngano toka Marekani, Mchele toka Thailand n.k.

Ikumbukwe pia kuwa, Waarabu hawakukaa hivi hivi, nao wana programu ya aina yake ya kugeuza sehemu ya jangwa kwa ajili ya kulima na kufuga (hasa mifugo ambayo ilikuwa nje ya utamaduni wao kama vile Ng’ombe); mathalan, ipo kampuni moja ya Ufalme wa Abu Dhabi ina Ng’ombe 10,000, lakini inanywesha maziwa katika eneo kubwa la nchi za Kiarabu (Sisi wafugaji wetu wanakumbatia utitiri wa mifugo huku maisha yao yakiwa hayaridhishi, na ugomvi kati yao na wakulima umekuwa kama homa ya vipindi)!

NINI TUFANYE?

Kwa maoni yangu, kuna umuhimu wa kujitathmini sote yaani wakulima; wataalamu wa kilimo; Vyuo vya kati na vikuu vya kilimo na biashara; taasisi za Kilimo, miundombinu na biashara; Bodi za Mazao ya Kilimo (na hata mifugo); taasisi za fedha; Viongozi wa ngazi mbalimbali kwa namna moja au nyingine; kujua tuliposimamia na si tulipoangukia.

Wataalamu wakiwapatia wakulima mafunzo, ushauri, maelekezo na mbinu juu ya kilimo bora cha kisasa na mnyororo mzima wa kutunza na kuongeza thamani ya mazao yao; miundombinu ya usafirishaji hasa barabara za mashambani na vijijini (Feeder roads) ikiboreshwa na kupewa kipaumbele cha kwanza; ukiondolewa ukiritimba wa upatikanaji nyaraka za kuthibitisha ubora na vibali husika kuwezesha uuzaji nje mazao ya kilimo.

Taasisi za fedha zikiwawezesha wafanyabiashara, wakulima, taasisi za wakulima, na vyama vya ushirika ili waweze kupanua uzalishaji na kuongeza kiwango cha mauzo ya nje; bodi za mazao, wizara husika, na viongozi wa maeneo husika ya kilimo wakiwajibika ipasavyo kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha fursa hizi adimu na adhimu za masoko ya nje zinachangamkiwa; basi ndoto ya kuwainua wakulima na hata wafugaji wetu kupitia sekta hizo itatimia kwa mafanikio ya hali ya juu, na kilimo na hata mifugo vitachangia pakubwa ukuwaji wa uchumi wa Taifa letu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here