‘Panya road’ majibu mepesi na tafakari hafifu

0

Na Yahya Msangi

UKIWA hutaki kujifikirisha, unaweza kutumia pafyumu kukabili harufu mbaya mwilini. Kila kunapozuka tatizo la wanaoitwa ‘panya road’ utasikia akili zilizopata kutu zikidai ni tatizo ni ‘ukosefu wa ajira kwa vijana.

Wengine utasikia wakisema ‘ni bomu linalosubiri kulipuka.’ Miaka inaenda bila bomu kulipuka. Hivi kama ‘panya road’ ni ukosefu wa ajira, wanapovamia wanapata ajira? Kama wanachotaka ni pesa kwa nini hawavamii benki? Au kama wanalaumu Serikali kwa nini hawavamii Ofisi ya Waziri Mkuu au ya Waziri wa Kazi?

Hizi ni akili ndogo kudhani ni tatizo la ajira. Mbona wanaokamatwa hawana sifa ya kuajiriwa au kujiajiri? Kwa dhana hii kwa nini wanaobaka isisemekane ni kwa kuwa hakuna wanawake au wanawake wamekuwa wagumu kuolewa?

‘Panya road’ ni uhalifu kama ulivyo ubakaji, ufisadi, ujambazi! Hata ungetoa ajira kwa vijana wote wapo watakaofanya upanyarodi tu. Ni sawa na ufisadi. Jinsi cheo na kipato kinavyoongezeka, ndivyo jinsi kiwango cha ufisadi kinavyoongezeka kwa fisadi. Ni kanuni ya uhalifu.

Kama Taifa tunapaswa kukaa chini na kutafakari ni nini hasa vichocheo vya upanya rodi. Binafsi ninaona vichocheo hivi:-

Kwanza, vijana kuaminishwa na manabii feki kuwa mafanikio yanaweza kuja kwa miujiza. Kwamba unaweza usisome, usijishughulishe, usijitume lakini ukafanikiwa kimiujiza.

Uhusiano wake na ‘upanyarodi’ ni huu;- kijana anapopewa matumaini hewa huja kukata tamaa. Kukata tamaa kunamsukuma kutenda uhalifu kama njia ya kufidia muda aliopoteza.

Tumeruhusu kila ‘mjanja’ awahadae vijana kwa mwamvuli wa imani. Kadri tunavyowaacha ndivyo tatizo linavyoongezeka. Ipo siku tutajikuta nchi nzima vijana wanategemea miujiza kufanikiwa.

Pili, vyombo husika vya dola kupoteza weledi. Mfano: kijana anatenda uhalifu, anapelekwa polisi. Badala ya sheria kuchukua mkondo anatoa rushwa, anaachiwa.

Kijana anaanza kuamini hakuna hatari akifanya uhalifu. Hela itamlinda. Anaamua sasa uhalifu uwe kazi yake kuu. Hana tena woga wa polisi wala jela.

Tatu, Malezi. Ukiwasikiliza wanaokamatwa utabaini malezi ni Tatizo. Hakuna anayemuuliza unaenda wapi usiku wote huu, umepata wapi hii simu, au hili jeraha ulipataje? Ni jukumu la Serikali kuhamasisha watu wake kuhusu malezi bora ya watoto.

Ndiyo maana ya kuwa na idara na vyuo na maafisa ya Ustawi wa jamii nchi nzima. Binadamu ni kiumbe sahalifu mno; ukifika Kingston, Jamaica utasikia radio na televisheni za Taifa zikirejerejea kutangaza athari za uvutaji wa bangi.

Nne, Kupuuzwa kwa ‘sekta za vijana’ haswa za michezo (sports) na sanaa (arts & showbiz). Ukitizama UK, US na kwingine utaona jinsi michezo na ‘Arts’ zinavyowaweka vijana bize. ‘Academy’ nyingi huchukua watoto wa mitaani. Mama mwenye nyumba yangu pale Dublin mwanae alichukuliwa na ‘Manchester United Academy.’

Mtoto huyo alikuwa na kipaji, lakini akaanza kubwia unga. MAN U walikuwa na program ya kuwasaidia. Alimradi mwanao awe na kipaji. Wao walikuwa Wanyarwanda. Kijana alijiunga enzi za kina Giggs na Paul Scholls. Mama yake akilipwa Paundi 3000 kwa wiki. Bahati mbaya kijana alipofika MAN U badala ya kuacha akaongeza kula unga! Uongozi wa klabu hiyo ukaamua kumrudisha Dublin.

Hatimaye baada ya muda, kijana alimchinja mama yake vipande vipande. Siku ya tukio, alirudi nyumbani usiku na kudai hela, aliponyimwa akamgeuza mama yake bucha. Alifungwa maisha.

Hapa kwetu, Baba wa Taifa Julius Nyerere wakati akiwa madarakani, aliona umuhimu wa michezo; kila Shirika na idara ya Serikali ikawa na timu.

Kuzaliwa mashindano kina UMISHUMTA, SHIMIWI, n.k. Wasioelewa walidhani ni kosa! Lakini, ilizuia upanya rodi, ubwia unga, ukahaba, n.k. Vijana wakajikita kwenye michezo.

Tano, kutoshirikisha jamii kikamilifu katika ulinzi. Kwenye maeneo mengi kuna polisi jamii. Je, ni kweli inashirikishwa? Inawezeshwa? Ni Kweli sungusungu ilikuwa na madhaifu, kwanini yasingerekebishwa?

Wahalifu waliiogopa mno sungusungu. Sungusungu ilipigwa vita na wahalifu haswa wazungu wa unga, majangili na majambazi. Wakijificha nyuma ya hoja ya Haki za binadamu.

Sita, kupuuzwa elimu. Vijana hawana sifa za kiajiriwa; kwa kuwa elimu na ujuzi hawana. Tumeacha elimu mikononi mwa sekta binafsi. Wanasiasa na wazazi ndio wanaoongoza kukebehi elimu. Watoto na vijana wanasikia na wanaamini hakuna haja ya kusoma.

Kama msukuma hakusoma na kawa mmbunge kwa nini yeye asome? Waliosoma nao kuna wakato wanafanya mambo yanayowavunja nguvu vijana. Jamii imeacha kabisa kuhimiza ‘elimu ni ufunguo wa Maisha’ kwa kuwa tumeruhusu wasio na elimu wafungue maisha; yaani hawana ufunguo makini wamefungua mlango. Utasubiri ufunguo darasani?

Tumewapa wasio na ufunguo nafasi za uongozi, wanawaongoza hata wenye ufunguo! Vijana wana funguo, lakini wamefungiwa nje na wasio na ufunguo! Hizi ni baadhi ya visababishi vya panyarodi. Tusikimbilie ukosefu wa ajira na kumwaga polisi mitaani peke yake.

Tukae chini tutengeneze mkakati mpana (a comprehensive national crime prévention strategic plan). La sivyo ‘panya road’ watatoweka na kurudi kama homa, lakini hawataisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here