Dkt. Mwinyi: Taifa lina changamoto ya baadhi ya watumishi kukosa uadilifu

0

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Taifa linakabiliwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya watumishi wa umma waliopewa dhamana kukosa uadilifu na kusababisha mapato ya Serikali kuingia mifukoni mwao.

Alhaj Dkt. Mwinyi alisema hayo katika salamu zake kwa waumini waliohudhuria Ibada ya sala ya ijumaa iliyofanyika Msikiti Mabluu, Mkoa wa Mjini Magharibi, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ameeleza kuwa, taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilitolewa hivi karibuni imebainisha kuwepo ubadhirifu mkubwa wa fedha za Serikali, hivyo akasema Serikali itachukua hatua thabiti kudhibiti ubadhirifu wa mali ya umma.

Aliwahimiza wafanyakazi, ikiwemo wale wanaokabidhiwa nyadhifa kuwa waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kusisitiza azma ya Serikali ya kufanyakazi ya kuondosha madhila katika utumishi wa umma.

Aidha, aliitaka jamii kuendelea kuhimiza suala la kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Alhaj Dkt. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa wananchi kudumisha amani na kusema anafarijika mno kusikia watu wote wanahubiri jambo hilo na kubainisha umuhimu wake katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii, “ ………. bila ya amani hakuna ibada”, alisema.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake za dhati kwa niaba ya Familia yake kwa wananchi wote ambao kwa namna moja au nyengine wamemfariji kutokana na msiba wa kuondokewa na kaka yake Hassan Ali Mwinyi, aliefariki dunia Jumatano wiki hii katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, Mkoa Mjini Magharibi.

Nae, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alisema Rais Dkt. Mwinyi ni mtu mwenye manufaa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar kutokana an juhudi zake za kusimamia maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya ijumaa Sheikh Said Ali Saleh alisema, amani ndio msingi wa mambo yote na neema kubwa miongoni mwa neema zilizotoka kwa Mwenyezi Mungu.

Alisema, katika kufanya ibada imani pekee haitoshi ni lazima iambatane na vitendo. “Msingi mzima wa Ibada unabebwa na kuwepo kwa amani, jambo ambalo liko mikononi mwa binadamu wenyewe.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here