Kupitia wazee unaweza kupata baraka au laana

0

Na Lion Mangole

NAPENDA kumshukuru Mungu kwa nafasi hii ya kukuandikia makala hii ambayo ni ya muhimu katika jamii yetu ili kujua jinsi ya kuwatunza na kuwahudumia Wazee na Vikongwe wetu. Mimi kama Mchungaji na Mwandishi (Mtunzi) wa vitabu, nimefanya utafiti wangu katika jamii nimegundua kuwa, Wazee na Vikongwe wetu wanaishi maisha ya shida sana na ya hatari sana.

Usalama wao kwa ujumla upo hatarini, hii imetokana na tatizo la jamii yetu kukosa uelewa wa jinsi ya kuwatunza Wazee na Vikongwe, ikiwa ni pamoja na kutokujua matatizo ya Wazee na mabadiliko ya maumbile yao kimwili na kiakili (hormone change). Jambo lililonishawishi zaidi kutoa elimu hii ni mazingira yangu ya kazi ya Uchungaji kwa kuwa nina lazimika kuwa karibu na jamii, na baadhi waumini wangu ni Wazee na Vikongwe.

Hiyo ilinisaidia kuona masumbufu mengi yanayowapata Wazee na Vikongwe, pia masumbufu yanayowapata wale wanaowalea Wazee na Vikongwe, hiyo ikawa moja ya sababu kubwa ya mimi kupata msukumo wa kuandika makala hii. Katika maagizo ya dini mbali mbali, karibu dini zote zinasisitiza umuhimu wa kuwaheshimu wazazi wetu, na ya kwamba tunapowaheshimu, itakuwa ni njia mojawapo ya kupata maisha mema na ya baraka hapa duniani.

Maisha ya heri siku ya mwisho (hata katika mila za makabila mengi sana, bado zinafundisha kuwaheshimu wazee, au wazazi, na mila nyingi zinaamini kuwa iwapo mtoto akiwadharau au kutokuwajali wazazi wake atakosa radhi, au atapatwa na mabaya). Kwa mfano katika Biblia. Efeso 6:1.3 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.

Kwa mujibu wa andiko hilo, tumeona kuwa Mungu aliweka amri mahususi ya kuwaheshimu wazazi. (wazazi ni baba, mama, na bibi, au babu, wote hawa ni wazazi wetu, kwani kuna watoto wengi walifiwa na wazazi wao au kutelekezwa, na walitunzwa na babu au bibi zao). Kwa mujibu wa mila za Kiafrika bibi na babu ndio wanatumiwa sana kama walezi wa watoto wa watoto wao, lakini baadae hao wazee mchango wao hauthaminiwi na yoyote, wanaambulia kuitwa wachawi n.k.

Maana ya ‘Heshima’ Heshima maana yake ni kumpa mtu nafasi ya pekee kwako, katika kumstahi. Au maana ya heshima ni kujinyenyekeza kwa mtu ambaye unaamini ni mtu mwenye mamlaka au uwezo zaidi ya wewe. Heshima inayoongelewa hapa sio ile heshima inayokuwa na sababu (heshima kwa sababu mtu amefanya kitu kinachostahili heshima).

Bali ni heshima isiyo na sababu yoyote, bali ni ya lazima, haijalishi mzazi yupoje au ana tabia nzuri au mbaya, kwa hali zote aheshimiwe tu. Biblia iliposema wazazi weheshimiwe, ina maana inawezekana kuna watoto watakao kuwa na sababu za msingi za kuwadharau wazazi; kutokana na matendo maovu ya wazazi wao, lakini amri hii inaonyesha kuwalinda wazazi wasidharauliwe kwa kisingizio chochote kile.

HESHIMA YA KUWATUNZA WAZAZI
Heshima isiwe ya mdomoni tu, bali iwe ya vitendo. Kila mtoto ajifunze kuwa na wajibu wa kuhakikisha wazazi wake wanahudumiwa na yeye, hata sio kwa asilimia mia moja, lakini walau kuwajali kwa asilimia fulani. 1 Timoseo 5:4 Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda
yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu.

Andiko hilo linafundisha watoto wasikwepe majukumu yao ya kuwatunza wazazi, kwa sababu labda watatunzwa na Kanisa, au taasisi za serikali (au taasisi nyinginezo za kidini), kwa nini watunzwe na Kanisa au serikali wakati watoto mpo?

Kuwatunza wazee au wazazi ni njia mojawapo ya kujipatia Baraka nyingi maishani mwako. Kumbuka, iwapo hutawatunza wazazi au ukiwanyanyapaa wazazi wako, hiyo itakuwa kama umepanda (laana) katika maisha yako na tarajia kuvuna hayo hayo katika maisha yako. Wagalatia 6:7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.

Wazazi wetu wamewekwa kama mtihani kwetu watoto, ili tukiuvuka tupate Baraka au tukishindwa tupate laana. Usijaribu kuwakimbia wazee wako, au kuwatelekeza au kuwasahau, bali jibidishe kuwatunza, na Mungu atakubariki sana. Kumbuka hata wewe ukizeheka unategemea utunzwe.

MAANA YA UZEE
Maana ya uzee ni, kuchakaa, au kukoma kwa ukuaji wa maumbile, na kuingia katika ukomavu (utu uzima) baada ya utu uzima ni uzee. Aidha, maana ya uzee ni kupoteza ubora wa maumbile ya kiumbe au binadamu. Aidha baadhi ya viungo vya mwili kupoteza uwezo wake wa kawaida.

Mabadiliko ya mapema kuonekana kwa mwanadamu ili kuonyesha dalili za mtu kuwa mzee ni, nywele kubadilika rangi kuwa nyeupe, ngozi ya ujana kupotea na kuja ngozi ya uzee inayomtambulisha mtu kuwa ni mtu mwenye umri mkubwa. Mara kadhaa kung’oka kwa meno bila maradhi yoyote ya meno, macho kupoteza uwezo wa kuona kama zamani, masikio kupoteza uwezo wa kusikia vema. Dalili nyingine ni.

Kuona wadogo zako na wao kuwa wakubwa au kuwa na watoto wakubwa, aidha unapoona watoto wako na wao wanakuwa na watoto. Kuitwa na watu hata usiowajua ‘mzee’ (Kwa wanawake kukoma siku za mwezi). Kwa umri wetu wa sasa uzee unaanzia miaka 45 hadi miaka 70.

MAANA YA UKONGWE (KIKONGWE)
Maana ya Ukongwe (Kikongwe) ni kupita umri wa uzee ambao ni miaka 70. Kwa kawaida mtu anapopita umri wa miaka 70 atakuwa ameanza maisha ya ukongwe (kikongwe) Dalili za ukongwe ni. Kupoteza kabisa uzuri wake karibu wote wa maumbile yake ya ujana.

Dalili za kuchakaa kabisa zitaonekana waziwazi. Kushindwa kutembea vizuri, kupinda mgongo, kutembelea fimbo, kukosa meno kabisa (kwa baadhi yao), nywele zote kuwa nyeupe, kupungua kwa uwezo wake wa kufikiri au kupoteza kumbukumbu. Aidha ni vikongwe wachache sana wanaozeheka wakiwa na nguvu na hawana mapungufu kama yaliiyotajwa hapo nyuma.

MAANDALIZI YA UZEE MWEMA
Mwili wa binadamu unajengwa kwa mfano ufuatao. Mwili wa binadamu ni kama ujenzi wa nyumba, Ili kuwa na nyumba bora na imara na ya kudumu, haina budi maandalizi yake kwa ujumla yawe mazuri. Vifaa utakavyo vitumia kwa ujenzi kama vile mawe au matofari inafaa yawe imara.

Pia, uwanja wa kujenga nyumba uwe mahali sahihi ambapo hakuna dalili za hatari kwa mazingira ya nyumba. Vipimo na ujenzi wake wote ufuate taratibu za ujenzi bora. Matokeo yoyote ya kuharibika kwa nyumba mapema yanasababishwa na maandalizi yasiyo sahihi ya ujenzi wa nyumba.

Mwandishi wa Makala hii ni Mchungaji wa Kanisa la MGCT. Nyantira Kitunda Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu 0717 528 272. Email.kusomavitabu@gmail.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here