Na Robert Heriel
MTUMWA akishazoea utumwa, kwake suala la uhuru ni tatizo. Hataki tena kuwa huru kutokana na mazoea mabaya ya utumwa. Yeye huona uhuru ni gharama sana. Yeye kwake ni bora utumwa kuliko Uhuru. kwake utumwa ni nafuu kuliko uhuru. Watanzania wengi wetu tayari tuna mawazo ya kitumwa.
Tumeishi chini ya utumwa wa Kifikra, Kiuchumi, Kijamii na wakati mwingine Kisiasa. Mtumwa hujiona duni siku zote mbele ya ‘Bwana’ wale. Mtumwa ni kama ‘Mbwa’ tu. Yeye mpaka apigiwe mlunzi ndio huchezesha mkia wake. Kuna baadhi ya Watanzania ukiwasikiliza maneno yao unaweza kushangaa, ni watu walioamua kuwa watumwa na kuamini wao bila wazungu hawawezi kufanya chochote.
Wanasema Marekani na washirika wake tunawategemea kwa mambo mengi. Tunawategemea katika kuendesha miradi yetu, huduma za kiafya, miundombinu, elimu, na teknolojia. Wanasema, hata Simu, mitandao tunayoitumia ni ya kwao.
Ni kweli ni ya kwao. Lakini, wakumbuke madini yanayotengeneza simu yanatoka Afrika. Pia, niwakikishie kuwa nchi hii tuna vijana wengi wenye akili zinazoweza kufanya mambo makubwa zaidi. Wapo wenye uwezo wa kutengeza simu, magari, ndege n.k.
Kwenye hii nchi nimezunguka kidogo. Nimeona vijana wa Kitanzania wenye uwezo wa kuvumbua na kubuni mambo yatakayolisaidia Taifa letu. Kama nawe umetembea, unaweza kuungana nami. Lakini, kama wewe sio mtu wa kuzunguka unaweza ukanibishia.
Vijana hawa wanachohitaji ni nafasi ya kuonyesha mambo yao. Kuonyesha akili zao ili zisaidie Watanzania. Na hawawezi kupata nafasi kama Wamarekani na washirika wake wakiendelea kutawala fikra zetu. Na hatuwezi kuondoa wakoloni weupe kwa kuwatumia viongozi wenye fikra za kitumwa. Kwa kuwatumia viongozi wanaowaamini Wamarekani zaidi ya vijana wetu.
Moja ya majibu ambayo ningeyatoa pale ambapo ningeulizwa ni kwa nini mpaka sasa nchi ya Tanzania ni masikini japokuwa imepata uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ningejibu kuwa ni kwa sababu hatupo nje ya mzunguko wa Wakoloni.
Bado tuna kundi kubwa la watu wenye kasumba ya kuona Wazungu ni bora kuliko Waafrika. Hao ndio waliomkwamisha Mwalimu Nyerere, na sasa watamkwamisha Mwalimu Magufuli, ingawa anajitahidi kupambana na malengo aliyojiwekea ya kuijenga nchi.
Kujikomboa kuna gharama kubwa, lakini hakuwezi kuwa na gharama inayozidi gharama ya utumwa. Utumwa ni gharama zaidi. Watu hawalijui hili. Kuna watu kwa fikra zao finyu za kitumwa, hufikiri endapo tutataka kujitegemea basi tutakumbwa na matatizo makubwa.
Ni kweli yapo matatizo ya kujitegemea, lakini hayawezi kuzidi uzito wa matatizo ya kuwa watumwa. Hatutapata tabu sana kama tuipatayo sasa hivi tukiwa na dhamira ya dhati kwa kushirikiana na kuwa kitu kimoja na kutompa nafasi adui wa nje. Adui wa nje siku zote hana nguvu kama adui wa ndani.
Hawa watu wanaopigia chapuo nchi za Magharibi kama Marekani, ndio wanaoturudisha nyuma siku zote. Hawa ndio wa kuogopa kuliko Marekani yenyewe. Kama ningepewa nafasi ya kushughulikia jambo hili, nisingehangaika na adui wa nje, bali hawa maadui wa ndani.
Hawa ndio watu wanaolifanya Taifa hili lisiende mbele kwa kushirikiana na adui wa nje. Nchi ya China, India, Korea ya Kaskazini na Iran, ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, japokuwa zinawekewa vikwazo na Wamarekani na vibaraka wake.
Nchi hizi zinaendelea kwa sababu moja tu, zimeamua kuendelea. Ili uendelee, ni lazima upambane na anayekunyonya. Iwe ni kwa njia ya wazi au ya kificho. Kwa njia ya amani au ya vita. Lakini, ni lazima upambane na anayekunyonya.
Pia, hauwezi kupambana na adui yako ikiwa ndani ya nchi yako hampo pamoja. Hili ndilo linakwamisha Waafrika wengi. Wapo wasaliti ambao wanaishi Tanzania au Afrika. Wamezaliwa Afrika. Wake zao ni Waafrika. Watoto wao ni Waafrika, lakini wanawaamini zaidi Wazungu kuliko Waafrika.
Marekani hana nguvu ikiwa tutaamua kushikana. Tutawaondoa maadui walio ndani ya nchi yetu. Hawa tukifanikiwa kuwafuta kabisa. Nina uhakika Marekani hana ubavu wa kufanya lolote katika Taifa hili.
Wapo wanaosema tutakuwa kama Zimbabwe. Ndio ni heri tuwe kama Zimbabwe tukiwa tunajiamulia mambo yetu sisi wenyewe. Tukiwa tunajivunia Teknolojia ya vijana wetu. Tukiwa tunajivunia Miundombinu ya watu wetu wenyewe.
Wapo wanaosema tukiwafukuza Marekani sijui tutakufa kwa UKIMWI kwa sababu ARV tunapewa kama msaada. Ndio tutakufa, lakini hatutakufa wote. Matabibu na wataalamu wa madawa na miti shamba watahangaika kuhakikisha tunapata suluhu la magonjwa yanayotuzunguka sio tu UKIMWI. Kufa tutakufa, lakini hatutakufa wote. Watakaobaki wataendeleza taifa hili.
Watu hawaogopi kufa wakiwa watumwa, wanaogopa kufa wakiwa huru. Hiyo ndio hatari ya kuwa mtumwa. Utumwa kwao ni heri kuliko Uhuru. Jambo hili linanikumbusha kipindi kile Waisrael wakitoka Misri kwenda Kanaani.
Wapo waliokuwa wanalalamika sana. Wapo waliosema ni heri tungebaki Utumwani kuliko kufia huku jangwani kwa kiu na njaa. Hayo ndio mawazo ya kitumwa. Kwao waliona ni bora wangebaki utumwani wakifa wajengewe makaburi ya kitumwa kuliko kufia jangwani wakiwa huru bila makaburi.
Historia ya Biblia inatuambia. Mungu aliwafyeka wote kile kizazi cha kitumwa hakikukanyaga Kanaani isipokuwa Joshua na Kalebu. Hata Taifa hili la Tanzania. Ili tuendelee tunaowajibu wa kuwafyeka wale watu wenye mitazamo ya kitumwa. Wale wanaoona ni heri kuwa watumwa kuliko kuwa huru.
Hawa ndio huwa rahisi kuungana na adui na kusaliti vijana wa Taifa hili. Hawa ni watu wakuwafyeka kwa namna yoyote ile. Ili vita hii iwe nyepesi na uelekeo wa ushindi kwa kizazi chetu kijacho. Kama hatutawafyeka hawa watu. Tutapiga miaka mingine 50 tukiwa pale pale. Tukiwa hakuna tulichofanya.
Wapo watu wanaamini kabisa Taifa letu lenye watu Milioni zaidi ya 60 hakuna anayejua kutengeneza simu, gari ndege sijui silaha. Huyo ni mpuuzi na asiyevumilika. Huyo amelidharau Taifa hili. Amedharau vijana wake. Amedharau kina mama waliowazaa vijana wa Taifa hili.
Ni mtu ambaye ameona matumbo yao hayawezi kuzaa watoto wenye akili za kubuni Simu, Mitandao ya kijamii na vikorokoro vingine. Watu wenye dharau kwa Taifa hili hawavumiliki, ni lazima tuwakabili kabla hatujamkabili adui wa nje.
Huwezi dharau Taifa lako halafu uchekewe. Yaani watu wote hawa Milioni 60 asiwepo mtu ajuaye kutengeneza dawa za magonjwa sugu? Hizo ni dharau na kebehi ambazo hatutazivumilia. Ni watu hawa hawa ambao wakipewa nafasi za uongozi wanatusaliti na kuwaibia Watanzania. Hawatoi nafasi vijana wa Taifa hili kuendesha miradi, wanawapa wazngu.
Wanawanyima Wafanyabiashara wazawa wenye pesa maeneo mazuri ya kuwekeza, lakini wanawapa wawekezaji wa nje. Hizo ndizo dharau zilizolifikisha Taifa hili hapa lilipo. Ili mechi hii tushinde tunahitaji mambo kadhaa muhimu. Yote yapo kwenye utekelezaji.