Samia alivyowafunga midomo wapinzani uwekezaji Bandari

0

Na Daniel Mbega

“WALE waliopiga kelele Mama kauza bandari, Mama kauza bandari, Mama kauza nini – mauzo yale faida yake ni hii leo (TPA kuongeza mapato). Huu ni mwanzo, tunatarajia mtapata faida kubwa zaidi kwa bandari zetu kubwa zote ambazo ziko nchini.”

Hii ni kauli mujarabu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa Mashirika ya Umma na Taasisi ambazo Serikali ina hisa, tukio lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Jumanne, Juni 11, 2024.

Kauli thabiti hii aliitoa wakati akizungumzia kuhusu mafanikio ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo iliongoza kundi la taasisi zisizo za biashara, ambalo linajumuisha Mashirika ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mashirika ya Umma, zinawajibika kutoa michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi.

TPA iliongoza kundi hilo baada ya kutoa gawio la Shilingi Bilioni 153.9, ikifuatiwa kwa mbali sana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotoa Shilingi Bilioni 34.7, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ilitoa Shilingi Bilioni 21.3, Wakala wa Huduma za Meli (TASAC) ilitoa Shilingi Bilioni 19.1, na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ukatoa Shilingi Bilioni 18.9.

Kwa kundi la taasisi za kibiashara linalojumuisha Mashirika na Kampuni ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma na Sheria ya Makampuni, zinawajibika kutoa gawio kwa wanahisa, Benki ya NMB ndiyo iliyoongoza kwa kutoa Shilingi Bilioni 54.5, ikifuatiwa na Twiga Minerals (ya ubia baina ya Serikali na Barrick Gold) iliyotoa Shilingi Bilioni 53.4, Airtel Tanzania (Shilingi Bilioni 40.8), Puma Energy (Shilingi Bilioni 12.2), na Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi kilitoa Shilingi Bilioni 10.2.

Rais Samia alikuwa na haki ya kutoa kauli hiyo, kwani katika mchakato wa kukaribisha mwekezaji kampuni ya Dubai Port World, maarufu kama DP World, kwenye Bandari ya Dar es Salaam kulisemwa maneno mengi, mambo mengi yakatokea; yaani hata wale ambao jamii iliwaheshimu na kuwaona kama ni wazalendo, walibadilika na kuilaumu Serikali kwa uamuzi wake huo.

Kutoa kiwango kikubwa cha gawio kunamaanisha kwamba, kumekuwa na mafanikio yaliyotokana na uboreshaji katika kuendesha Bandari, ndiyo maana faida kubwa inapatikana.

Rais Samia alisema, wapo waliokuwa wakipiga kelele kuwa anauza Bandari lakini sasa faida imeanza kuonekana. “Pongezi maalum kwa makampuni yaliyoleta gawio kwa Serikali ikiwemo TPA ambao mwaka jana nina hakika level (kiwango) yenu haikuwa hivi, lakini kwa mageuzi yaliyotokea bandarini mmeweza kufikia kiwango hiki na mwakani nina uhakika mnaweza kuleta double (maradufu) ya mlichokileta leo.

“Huko ndiko tulikuwa tunaelekea Ndugu zangu, wale waliopiga kelele ‘Mama kauza Bahari, Mama kauza Bandari, Mama kauza nini’ mauzo yale faida yake ni hii hapa leo, na huu ni mwanzo tu tunatarajia kupata faida kubwa zaidi,” alisema.

Na hii inadhihirisha nia njema ya Serikali katika kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za jamii kwa kuweka mazingira bora ya kufanya baishara, kutunga sera rafiki/chanya zinazohamasisha uwekezaji nchini. “Tumeweka mazingira haya ili wafanye kazi wapate faida ili tuweze kupata gawio, bila faida hakuna gawio na bila sera nzuri hakuna kupata faida kwahiyo tunatengeneza sera nzuri wapate faida na tupate gawio.”

Rais Samia anasema, alifokewa na wajumbe wa NEC wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipoamua kuruhusu vyama vya siasa kuanza mikutano ya hadhara pamoja na maandamano akiwataka viongozi wengine Serikalini kuacha uoga ili kutimiza malengo.

“Ule uoga tulionao tuuvue. Tuliposema acheni vyama vifanye kazi zao walinifokea na sasa wakinitukana, wengine wanasema yakukute si uliwaruhusu… lakini tumewaruhusu wamesema nini, wamesema nini, wameandama, tena tukiwasindikiza, kimetokea nini, tulikuwa na hofu tu ya bure,” akasema. “Kwa mwoga kilikwenda kicheko kwa shujaa kikaenda kilio, si katika nafasi zote, si katika maeneo yote.”

Rais Samia alikuwa na haki ya kuendelea kusisitiza kuhusu uamuzi wake wa kukaribisha mwekezaji Bandari, ambapo anasema msingi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kuongeza utoaji wa gawio ni uwekezaji uliofanywa katika uendeshaji wa bandari kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Siyo siri, wale wapinzani wa uwekezaji katika Bandari wamezibwa midomo kwa sababu kelele zilizokuwa zinapigwa kupinga uwekezaji huo matokeo yake ndiyo faida inayoonekana.

Sakata la uwekezaji wa sekta binafsi katika Bandari hiyo liliibua upinzani mkali na hoja zaidi zilielekezwa kwenye kasoro za masharti ya mkataba wa nchi na nchi (IGA).

Miongoni mwa kasoro hizo, ni kukosekana ukomo wa mkataba, kadhalika mashauri kati ya pande mbili iwapo zitahitalifiana yaamuliwe na mahakama za nje ya Tanzania.

Mkuu huyo wa nchi akasema, kutokana na mageuzi yaliyofanyika katika eneo hilo, anatarajia mwakani TPA itatoa gawio mara mbili ya lile la mwaka huu, kwani, faida hiyo ni mwanzo na kuna matarajio ya kupata faida kubwa zaidi katika mwaka ujao. “Mwakani tunatarajia kiwango kikubwa zaidi ya kile kisichopatikana mwaka huu, hakuna sababu kama mtaendesha na sekta binafsi iliyopo pale,”

“Tumeona Benki ya NMB, Kampuni ya Twiga Mineral Corporation, Airtel Tanzania, Puma Energy na TPC Moshi wametoa gawio kubwa na sisi tuna hisa chache, nadhani kila shirika lifanye kazi kwa juhudi ili kufikia kampuni hizi.”
Rais Samia anasema, kilichofanywa na Mashirika ya Umma kama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Wakala wa Huduma za Meli Tanzania (TASAC) na BRELA ni ushahidi tosha wa kuweka mifumo mizuri na kushirikisha wawekezaji.

Kuhusu mifumo kusomana, Rais Samia ameagiza Mamlaka husika kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu mifumo iweze kusomana na kwamba suala hilo limechukua muda mrefu ambapo ameongeza kuwa, hataki kusikia Shirika ambalo mifumo yake haisomani na mingine.

Kiongozi huyo anasema, alipoingia madarakani aliagiza Mashirika ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa zibadilike na kuchangia katika Pato la Taifa, jambo ambalo limeanza kutekelezwa.

Mafanikio ya uboreshaji wa miundombinu ya Bandari yameiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuhudumia shehena ya mizigo ya tani Milioni 20.72 katika bandari zote za Tanzania Bara hadi kufikia mwezi Machi 2023/24.

Serikali kupitia TPA imeendelea kusimamia na kutoa huduma zote za kibandari katika Bandari zote za Tanzania Bara.

Wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2024/25, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa alisema, hadi kufikia Machi, 2024 TPA ilihudumia tani Milioni 20.72 ya shehena ya mizigo ikilinganishwa na tani Milioni 14.56 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 42.31.

Kwa upande wa makasha, TPA ilihudumia makasha 805,167 ikilinganishwa na makasha 688,609 katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 16.92.

Ongezeko hilo la shehena ya mizigo na makasha limetokana na mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Kwa upande mwingine, Serikali kupitia, TPA imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa bandari nchini pamoja Bandari Kavu.

TPA imeendelea na juhudi mbalimbali za kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi nje ya nchi; kutafuta masoko; na kufanya ununuzi wa vifaa na mitambo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika bandari nchini.

Kuhusu uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Prof. Mbarawa akasema, TPA imeendelea kutekeleza kazi mbalimbali ambapo uchimbaji wa kina umefikia mita 15.5 na upanuzi wa lango la kuingia meli ambalo lina upana wa mita 200.

Kutokana na maboresho hayo, Bandari hiyo sasa ina uwezo wa kupokea meli kubwa zenye urefu wa mita 305 na upembuzi yakinifu wa kuboresha Gati Na. 8 – 11 na ujenzi wa Gati Na. 12 – 15 bado unaendelea.

Vilevile, anasema mkataba wa kuendeleza miundombinu ya kupokelea mafuta (Single Receiving Terminal – SRT) unaohusisha ujenzi wa matenki 15 ya mafuta (tank farms) pamoja na miundombinu yake, yenye uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mita za ujazo 420,000 umesainiwa Februari 26, 2024 na maandalizi ya kuanza ujenzi yanaendelea.

Anasema, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeendelea kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa baadhi ya maeneo ya bandari kwa kuingia ubia na Kampuni Binafsi katika kuendeleza na kuendesha shughuli za bandari kuanzia Gati Na. 4 hadi 7.

Akasema, kwa sasa hatua mbalimbali zikiwemo za makabidhiano na mobilization zinaendelea ili kuruhusu utekelezaji rasmi kuanza. Aidha, Serikali inaendelea na taratibu za kumpata Mwekezaji mwingine atakayekuwa na jukumu la kufanya shughuli za uendeshaji kuanzia Gati Namba 8 hadi 11, lengo likiwa kuongeza tija katika utendaji wa bandari.

Profesa Mbarawa alilieleza Bunge pia kwamba, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imeendelea kutoa huduma za usafiri na usafirishaji katika Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Akasema, hadi kufikia Machi, 2024 MSCL ilisafirisha abiria 198,080 ikilinganishwa na abiria 170,137 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 16.42.

Kwa upande wa mizigo, MSCL ilisafirisha tani 33,288.44 ikilinganishwa na tani 18,909 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 76.05.

Ongezeko hilo, Prof. Mbarawa anasema, limetokana na kukamilika kwa ukarabati na kuanza kazi kwa meli ya Mv. Umoja ambayo ilianza kutoa huduma mwezi Oktoba, 2023 katika Ziwa Victoria kati ya Bandari ya Mwanza Kusini na Bandari za Port bell na Jinja, Uganda.

Aidha, ujenzi wa Meli ya Mv. Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ umekamilika kwa asilimia 95 na tayari meli hiyo imefanyiwa majaribio ziwani ya mifumo na mitambo.

Pia, Serikali kupitia MSCL ilisaini Mkataba wa ujenzi wa meli mpya ya kubeba mizigo ya tani 3,000 katika Ziwa Victoria na ilisaini mikataba miwili ya ujenzi wa meli ya mizigo ya tani 3500; na ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli katika Ziwa Tanganyika.

Ujenzi wa kiwanda hicho ni hatua muhimu ya kujivunia kwa Taifa letu kwa kuwa ni mara ya kwanza kujenga kiwanda cha aina hii hapa nchini ambapo kwa miaka ya nyuma meli nyingi zilikuwa zinatengenezwa nje ya nchi. Vilevile mradi wa ukarabati wa Mv. Liemba tayari umesainiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here