Wananchi watakiwa kufunga kifaa cha kuzuia athari za umeme majumbani

0
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

. Lengo ni kujilinda na athari za umeme

. Kapinga ataja juhudi zinazofanywa na Serikali kuimarisha hali ya umeme
Jimbo la Segerea

. Asema usambazaji umeme vijijini unaendelea, vitongoji 4000 kupatiwa
umeme 2024/2025

NAIBU waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka wananchi kuchukua hatua za kufunga vifaa vya kuzuia athari za umeme kwenye nyumba (circuit breaker) ili kujilinda na majanga yanayoweza kutokea pale umeme unapokuwa mwingi au kupungua.

Kapinga alisema hayo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kwa wananchi wanaopata hasara kutokana na kukatika kwa umeme au nyumba kuungua.

Alisema, uchunguzi unapothibitisha kuwa tatizo la kuungua kwa nyumba limesababishwa na TANESCO, Serikali inachukua hatua kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Akizungumzia hali ya umeme katika Jimbo la Segerea, Kapinga ameeleza kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme katika jimbo hilo ilitokana na kuzidiwa kwa kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Gongo la Mboto ambacho kinapeleka umeme Segerea.

Ametanabaisha kuwa, hali ya umeme Segerea sasa imeimarika kutokana na Serikali kuchukua hatua ambapo wananchi wengine kutoka Jimbo la Segerea wanapata umeme kutoka kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Kipawa.

Aliongeza, Serikali kupitia TANESCO pia inatekeleza miradi ya upanuzi wa kituo cha Gongo la Mboto na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ubungo hadi Tabata ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa umeme.

Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso aliyetaka kujua mpango wa Serikali kupeleka umeme kwenye maeneo muhimu katika eneo la Mishamo hasa kwenye Soko na Kituo cha Afya.

Kapinga alisema, ni mkakati wa Serikali kuhakikisha umeme unakwenda kila kijiji na miradi ya usambazaji umeme inaendelea ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25 vitongoji 4,000 vitapata umeme.

Akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali kuimarisha umeme kwenye vijiji vya Namtumbo vinavyopata umeme mdogo, Kapinga alisema Serikali tayari inao mpango wa kuongeza nguvu umeme kwenye maeneo ya vijijini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here