Mtoto mchanga huishi kwenye kivuli cha wazazi wake

0

Na Dkt. Gohar Mushtaq

HIVI karibuni, utafiti wa kuvutia wa Kisayansi ulifanyika kuhusiana na uhusiano wa mama mjamzito na mtoto ambaye hajazaliwa. Hivi sasa tunajua kuwa, moyo wa mtoto ambaye hajazaliwa huumbika na kuanza kudunda muda mrefu kabla ubongo haujaja.

Japokuwa sababu halisi inayosababisha kudunda kwa moyo wa mtoto aliye tumboni haifahamiki, lakini yaelekea kabisa kuwa mapigo ya moyo wa mama ndiyo yanayosababisha mapigo ya moyo wa mtoto ambaye yumo tumboni mwake.

Katika wakati ambao mtoto aliye tumboni ana majuma manne na nusu tumboni mwa mamaake, mlango wake wa kusikia huwa umeshakamilika ambapo hukaribia muda (wa miezi minne) ambapo Malaika humpulizia roho mtoto aliye tumboni.

Katika hatua hiyo, mtoto aliye tumboni huweza kusikia sauti zinazosikika mwilini mwa mama yake. Kati ya sauti zote ambazo mtoto huzisikia akiwa tumboni ni sauti ya mapigo ya moyo wa mamaake ndiyo inayotawala zaidi na huwa ya kudumu.

Muda wa kuwa mapigo ya moyo ya mama ni ya kawaida, mtoto aliye tumboni huwa salama. Katika miaka ya 1940, Lester Sontag, M.D., alikuwa mwanasayansi wa kwanza kugundua kuwa mapigo ya moyo ya mama huathiri kwa namna nyingi mapigo ya moyo ya mtoto aliye tumboni. (Taz. Bernard, J. & Sontag, I. (1947), Fetal Reactions to Sound. Journal of Genetic Psychology)

Kumbukumbu isiyotambulika ya mapigo ya mama wakati mtoto akiwa tumboni, hubakia kwa mtoto hata baada ya kuzaliwa kwake na hubakia kwa kipindi kingine cha maisha yake.

Tafiti kadhaa za kisayansi zinathibitisha jambo hili. Ilibainishwa kuwa wakati wakati mlio wa mapigo ya moyo ulipopigwa katika kanda ya radio katika wodi ya watoto hospitalini, ulipunguza vilio vya watoto katika wodi hiyo.

Thomas Verny, M.D., katika Kitabu chake maarufu, ‘The Secret Life of the Unborn Child,’ ameeleza kuwa kupungua kwa vilio hivyo vya watoto kulitokana na kumbukumbu isiyotambulika ya mapigo ya moyo ya mama ambayo, baada ya kuzaliwa, mtoto huendelea kuburudikanayo pale anapowekwa kifuani kwa mtu. (Watoto hubembelezewa vifuani-mfasiri).

Baadhi ya watu wazima hupata usingizi pale wanaposikia milio ya ta-ta-ta ya saa za ukutani. Baadhi ya watu wanaosumbuliwa na tatizo la kukosa usingizi (insomnia) hutumia milio ya mitambo ambayo hulingana na mlio wa mapigo ya moyo, na hiyo huenda ndiyo sababu kwa nini watu hawabughudhiwi na kelele za mashine za kuchapia maandishi maofisini.

Muhanga wa mama kujitoa kwa ajili ya mtoto wake si tu unajumuisha maumivu na taabu za kipindi kirefu cha ujauzito bali pia wakati wa kujifungua. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an, “Na Tumemuusia Mwanadamu afanye wema kwa wazazi wake. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu” (46:15)

Kwa mujibu wa hadithi, mwanamke anayekufa kwa uzazi huhesabiwa kuwa ni “Shahiid”. Kwa kulinganishwa na wanyama wote, wanadamu ndio wenye ubongo mkubwa na fuvu kubwa. Kwa sababu hii, Robert Bly kaandika hivi kuhusu mwanadamu:

“Kichwa kikubwa (cha mtoto wa binadamu) kama kilivyo na kama ambavyo kimekuwa huufanya uzazi uwe jambo la uchungu mno kwa mwanamke.” Na tena huku ni kujitoa muhanga anakokufanya mama ili kumleta mtoto duniani.

Utafiti uliofanywa na Wanasaikolojia na wanasayansi wa sayansi ya jamii umeonesha kuwa ule mgusano wa mama na mtoto ni muhimu mno kwa ustawi wa kiakili wa mtoto. Mojawapo ya njia za hivi leo ambapo mgusano huu wa mama na mtoto huweza kutimizwa ni pale mama anapomnyonyesha mtoto wake.

Takribani miaka hamsini iliyopita, katika wimbi la umamboleo, akina mama wengi Barani Ulaya na Amerika walianza kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya chupa eti kwa sababu waliona ni ushamba kunyonyesha mtoto maziwa ya mama. Akina mama hawa hadi sasa wanalipa gharama ya jambo hili kwa sura ya masaibu mengi.

Utafiti umeonesha kuwa watoto wachanga wanaonyonyeshwa maziwa ya mama huwa na akili zaidi kuliko watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya chupa. Kuna faida nyingine lukuki za maziwa ya mama kulinganisha na maziwa ya chupa (Taz Blum, Deborah, “Is Mother Milk Key to Child’s growth?”).

Hata Mashirika ya UNICEF (Shirika la Huduma za Watoto Duniani) na Shirika la Afya Duniani (WHO), kama alivyoandika Jack Newman katika jarida la ‘Scientific American,’ sasa yametambua umuhimu wa amri ya kunyonyesha. “Na ingawaje si kanuni katika jamii nyingi za nchi za Viwanda, Mashirika ya Watoto na Chakula Duniani, UNICEF na WHO, yote kwa pamoja yanashauri unyonyeshaji wa maziwa ya mama uwe Miaka 2 na zaidi.”

Ni jambo la hakika kuwa mwitiko wa kinga ya mtoto hautimizi nguvu kamili hadi umri wa miaka mitano au zaidi.” (Newman, Jack, M.D, December 1995. “Breast Milk Protects Newborns”. Scientific American).

Kwa mujibu wa wanasaikolojia, asilimia 75 ya wajihi wa mtoto hujengeka katika miaka 3 ya maisha yake. Robert Bly, akizungumzia makuzi ya ubongo wa mtoto mchanga baada ya kuzaliwa, kaandika:

“Wakati wa kuzaliwa, ngedere wa Asia, kwa mfano, huwa na ubongo ambao tayari una wastani wa asilimia 65 ya umbile lake la mwisho; ubongo wa kima huwa ni asilimia 40.5 ya umbile lake la mwisho; lakini ubongo wa mtoto wa binadamu huwa na wastani wa asilimia 23 tu.

Hiyo ina maana kuwa robo tatu ya ukuaji wa fuvu la kichwa hujitokeza baada ya mtoto kuzaliwa.” (Bly, Robert (1996). “The Sibling Society”). Makuzi ya kawaida ya ubongo wa binadamu hayawezi kutimia bila ya msaada wa wazazi. Ndiyo sababu, Mwanasaikolojia mashuhuri wa Kiamerika, Carl Jang, alisema: “Mtoto mchanga wa binadamu huishi kwenye kivuli cha wazazi wake.”

Hata hivyo, utafiti uliotajwa hapo juu unatuonesha jinsi wazazi wetu walivyo na uzito kwetu kwa ushahidi wa kidini na Kisayansi ambapo siha ya kimwili na kiakili tuliyonayo hivi sasa kama watu wazima, ni matokeo ya mihanga waliyojitoa wazazi wetu kwa ajili yetu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here