Baada ya siku 60, NHC kuwaweka hadharani waliokimbia na madeni

0

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Nyumba la Taifa NHC limetangaza kampeni kabambe ya kukusanya madeni kwa wapangaji wa nyumba zake waliopo na waliohama ili kuhakikisha wanakusanya madeni hayo yanayofikia kiasi cha Shilingi Bilioni 26.

Moja ya mbinu ambazo NHC wameamua kuzitumia ili kufanikisha kukusanya deni hilo, ni kuweka hadharani majina ya wadaiwa hao, na kuwafikisha mahakamani baada ya muda wa siku 60 uliotolewa kulipa malimbikizo yao kumalizika.

Hayo yameelezwa na Meneja wa habari na Uhusiano Shirika la Nyumba NHC Muungano Saguya wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Shirika hilo Upanga jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kampeni hiyo ya miezi miwili itaongozwa na kauli mbiu ya “LIPA KODI YA NYUMBA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU’’.

“Hapo awali, tuliwafahamisha kuwa Shirika limekuwa likidai madeni ya kodi yanayofikia Shilingi Bilioni 26 na tuliwaeleza mbinu mbalimbali zinazotumika kukusanya madeni hayo. Pamoja na juhudi hizo zilizosaidia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 5, bado yapo pia madeni ambayo yanahitaji kufutwa na Bodi yanayofikia takriban Shilingi Bilioni 6,” alisema Saguya.

Alisema, kutokana na hali ya ukusanyaji wa madeni hayo ilivyo, Shirika limeamua kuendelea na kampeni ya kukusanya madeni hayo kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba (active tenants) na wapangaji waliohama (ex-tenants) wanaodaiwa malimbikizo ya kodi hadi sasa.

“Shirika linatoa muda wa siku sitini (60), kuanzia tarehe 01/11/2022 mpaka 30/12/2022 kuhakikisha kuwa wamelipa malimbikizo yote wanayodaiwa ili kuepuka kuchukuliwa hatua stahiki. Kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba (active tenants) ambao hawatalipa ndani ya kipindi hicho, Shirika linakusudia kuvunja mikataba yao ya upangaji na kuwaondoa kwenye nyumba na kuchukua mali zao kwa ajili ya kuuza ili kufidia madeni yao,” alisema Saguya.

Aidha, Saguya alisema kwa wapangaji ambao walishapewa notisi mbalimbali, utekelezaji utaendelea kama notisi hizo zinavyoelekeza.

“Shirika linawasihi watekeleze wajibu wao kuepuka kadhia zitakazoweza kujitokeza kwa kushindwa kufanya hivyo. Kwa waliokuwa wapangaji ambao wamehama na kuacha madeni (ex-tenants) wanayodaiwa, wanatakiwa kufika katika Ofisi za Shirika zilizo karibu nao na kupewa utaratibu wa malipo ikiwemo (control number) ili walipe,” alisema.

Alisema, kwa wale watakaoshindwa kutekeleza ndani ya muda uliotolewa, Shirika litawatangaza kwenye vyombo vya habari ili watanzania wawafahamu watu wanaokwamisha Shirika lao na tutawachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

“Kitendo cha wapangaji hao kukimbia na madeni ya nyumba ni sawa na uhujumu ambao hautavumiliwa na kwamba Shirika linaenda kuwasaka popote walipo kwa kutumia mbinu mbalimbali. Shirika linashirikiana na vyombo vingine vya dola kuhakikisha kuwa wapangaji hao wanapatikana na wanalipa kodi zao,” alisisitiza.

Aidha, Saguya aliwashukuru wapangaji wote wanaotimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya nyumba kwa wakati kama mikataba ya upangaji inavyoelekeza. “Tunashukuru wapangaji walioitikia wito wetu kwa kulipa madeni yao.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here