Rais Samia aungwe mkono bila kujali Itikadi za Kisiasa – Shaka

0

*Asema kazi kuwa anayoifanya itailetea heshima nchi

*Ataja ujenzi Uwanja wa Msalato umedhihirisha uwezo wake mkubwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema ni jukumu la Mtanzania kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada alizionesha kuleta maendeleo nchini.

Alisema, katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, atakuwa kiongozi wa mfano katika kutekeleza azimio la kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mkoani Dodoma na kufungua fursa zenye kuwahisa wananchi moja kwa moja.

Shaka alisema hayo leo Oktoba 30, 2022 Msalato mkoani Dodoma alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua ni kwa kiasi gani CCM inaridhishwa na utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi baada ya Rais Samia kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa.

“Kwa kasi tunayokwenda nayo tunaimani kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwamba katika kipindi chake cha uongozi, Tanzania itapiga hatua kubwa za maendeleo. Tumesikia kwenye hotuba yake amesisitiza kwamba miradi yote ya kimkakati lazima iwaguse Watanzania, hiyo ni kuonyesha kwamba, Rais Samia anatekeleza miradi ya kimkakati wakati huo huo yuko makini kusimamia ustawishaji wa maendeleo ya Watanzania.

“Wote tuna jukumu la kujenga nchi bila ya kuangalia itikadi zetu za kisiasa, haya yanayofanyika ni kwa maslahi mapana ya Watanzania. Ni imani yetu kwamba wenzetu wa vyama vingine wataunga mkono jitihada hizi. Ni kweli Ilani inayotekelezwa ni ya Chama Cha Mapinduzi lakini maendeleo yanayoletwa ni ya Watanzania wote kwa ujumla, kwa hiyo nitoe wito tumeanza vizuri, Mheshimiwa Rais Samia tangu ameingia madarakani ametuunganisha pamoja, tunakwenda vizuri kikubwa ni kuendelea kusisitiza kuwa umoja wetu ndio ushindi wetu,” alisema.

Aidha, Shaka alisema, kuimarika kwa ujenzi wa miradi ya kimkakati ni kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania hivyo ni ana imani kwamba wananchi watatumia vyema fursa ambazo zinatolewa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

KUHUSU UJENZI WA MSALATO

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapongeza kwa dhati Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kwa kuandika historia kwa Taifa baada ya miaka tangu kuwekwa Azimio la Makao Makuu ya nchi kuhamia Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Meneja Mkaazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa upande wa Tanzania Dkt. Patricia Leverley kuashiria uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, Mkoani Dodoma tarehe 30 Oktoba, 2022. Wengine katika picha ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson pamoja na viongozi wengine wa Chama na Serikali.

“Kama tulivyosikia Oktoba mwaka 1973 ndipo lilipotangazwa Azimio la kuhamia hapa Dodoma. Tangu mwaka 1973 hadi leo zimepita Awamu mbalimbali na kila Awamu ilichukua sehemu ya utekelezaji wa uamuzi huo. Katika Awamu hii ya Sita ya ndugu Samia Suluhu Hassan Kasi ya utekelezaji wa uamuzi huo imekuwa kubwa sana.”

Alieleza kuwa, uamuzi huo ulikuwa wa Halmashauri Kuu ya TANU kwa wakati huo na ukarithiwa na CCM, hivyo kwa sasa unasimama kuwa uamuzi ya Chama Cha Mapinduzi.

“Ndio maana kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM kupitia Ibara ya 59 (h), tumeeleza namna ambavyo katika kipindi cha miaka mitano (2020-2025) tutajenga Uwanja wa ndege wa Msalato

“Kwenye hili Rais Samia amefanya vizuri sana, tukiangalia uendelezaji mji wa Serikali wote tumeona Awamu ya Tano imefanya vizuri, imetoa karibu Shilini Bilioni 39 katika uendelezaji wa mji huo, lakini Awamu ya Sita imechochea na kukoleza, Rais Samia tayari ameshaidhinisha Shilingi Bilioni 300 kwa ajili ya uendelezaji mji wa Serikali.

“Hiyo yote ni kuonyesha namna ambavyo maazimio na uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi unavyotekelezwa, kwenye hilo niseme tulikotoka ni kuzuri, tulipo ni pazuri zaidi, lakini mwelekeo wetu ni kuwa imara zaidi,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here