Na Iddy Mkwama
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ni miongoni mwa Taasisi za umma ambazo zinachangia zaidi ya asilimia 40% ya mapato ya kikodi yanayotoka kwenye eneo la forodha.
TPA ipo kwa mujibu wa Sheria namba 17 ya mwaka 2004, ambayo inatoa wajibu wa Mamlaka hiyo kusimamia shughuli za Bandari Tanzania, kuendesha na kuendeleza bandari ikiwemo kuboresha miundombinu yake, kutangaza shughuli za bandari sambamba na kushirikisha sekta binafsi.
“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, inasimamia vituo sita, wakati wa THA tuliyoirithi, kabla ya TPA, tulikuwa tunasimamia vituo vitatu, kwa maana ya bandari tatu za kwenye bahari; Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, lakini baada ya mabadiliko ya sheria na mabadiliko madogo ya mwaka 2019,”
“Shughuli za Mamlaka ya usimamizi wa bandari zikaenda hadi kwenye maziwa; kwahiyo tunaenda Ziwa Viktoria na bandari zake zote, Ziwa Tanganyika pamoja na Nyasa,” anasema Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho.
Mrisho, ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa katika Mkutano Mkuu wa 13 wa Kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika hivi karibuni, kwenye ukumbi wa St. Gaspar, Mjini Dodoma, anasema Bandari ya Dar es Salaam ndio kubwa, ambapo asilimia 95% za shughuli za TPA zinafanyika kwenye bandari hiyo, huku Tanga na Mtwara wakishindana kwa kiwango cha shehena.
Akizungumzia utendaji wa Bandari za Tanzania kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 na 2022/2023, anasema kinapimwa kwa maeneo makuu matatu; idadi ya meli unazohudumia, kiwango cha mzigo ulichohudumia na Mapato uliyofanikiwa kuyakusanya, “ukiulizwa hivisasa bandari inafanya vizuri au haifanyi vizuri, unatazama hayo maeneo.”
Mrisho anasema, mwaka 2020/2021 wametoka kuhudumia meli zipatazo 1600, hadi meli 2500 mwaka 2022/2023, huku kiwango cha shehena kilichohudumiwa, kutoka Tani Milioni 16 miaka mitatu iliyopita hadi Tani Milioni 24 kwa mwaka wa fedha uliopita, ambapo ukiangalia tani hizo zote, bandari ya Dar es Salaam ambayo imehudumia zaidi ya Tani Milioni 21, ambapo imevuka kiwango kilichowekwa cha zaidi ya Tani Milioni 19.
Aidha, Mrisho anasema, kiwango cha mapato kwa miaka mitatu iliyopita; mwaka 2021, mapato ya bandari yalifika Bilioni 800 na mwaka wa fedha uliopita walifikia Trilioni 1.3, “haya ni mapato au tozo za bandari, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) anakusanya kiasi kikubwa cha kodi kutoka kwenye bandari zetu.”
Anasema, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa mapato hayo na kuchangia kuzalisha kiasi hicho cha fedha na kusaidia Taifa katika kuboresha shughuli mbalimbali za Serikali, ni uboreshaji wa miundombinu iliyopo kwenye bandari ambazo zinasimamiwa na TPA.
“Kwa miaka sita au saba nyuma, ukianza na Bandari ya Dar es Salaam, tulikuwa na matatizo makubwa sana ya miundombinu na kuleta kelele katika utoaji wa huduma kwa meli na shehena, Serikali ikafanya juhudi kubwa na kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha inapata fedha na kuboresha bandari,” anasema.
Mrisho anasema, moja ya mambo ambayo yamefanyika kwenye bandari hiyo ni kuongeza gati kwa ajili kuhudumia shehena ya magari, ambapo limejengwa gati la Mita za Mraba 300, sambamba na kutengwa Mita za Mraba 72,000 kwa ajili ya kuhifadhia shehena ya magari.
“Wote tunashuhudia, idadi ya magari yanayoshukia bandari ya Dar es Salaam ni 250,000 hadi 300,000 kwa mwaka na uzuri ni kwamba hayatumiki kwenye nchi yetu pekee, bali kwa nchi za jirani ambazo ni sita tunazozihudumia,” anasema Mrisho.
Anaendelea kusema, pamoja na kuongeza gati moja la magari, magati mengine yaliyokuwa na malalamiko kutokana na kukosa uwezo wa kuhudumia meli vizuri yalifanyiwa maboresho; mageti hayo ni kuanzia namba moja hadi namba saba, ambapo yameongezewa urefu na kina kutoka Mita 9 hadi kufikia Mita 14.5 ili kupata meli kubwa na hivi sasa zinaingia zikiwa na shehena kubwa.
“Ukiwa na meli kubwa, ndipo ambapo wasafirishaji wengi wanaweza wakaleta mzigo mwingi zaidi kupitia bandari yako, pia umefanyika uchimbaji wa mlango wa kuingilia meli na kazi hiyo imekamilika mwezi uliopita, hivi sasa unaweza kupokea meli yenye Mita 305, hapo awali zilikuwa zinaingia meli ndogo zikiwa na shehena ndogo ndogo,” anasema.
Anaendelea kusema: “Maboresho hayo yameleta manufaa makubwa na tunapozungumzia takwimu za Mapato ni kutokana na maboresho ya bandari ya Dar es Salaam. Ukienda Tanga, meli zinafika moja kwa moja gatini na zinapakuliwa vizuri, kabla ya hapo zilikuwa zinapaki nje zaidi ya Kilomita Moja kisha mzigo unafaulishwa, ilikuwa inaongeza gharama za uendeshaji, lakini sasa gharama hizo hazipo tena kwasababu meli zina uwezo wa kufika mpaka gatini.”
Kwa upande wa bandari ya Mtwara, kulikuwa na gati moja, la Mita 385, lakini hivi sasa limetengenezwa gati jingine la Mita 300 ambalo limegharimu Shilingi Milioni 157 “kwasasa tuna uwezo mkubwa, tunahudumia meli zinazobeba makaa ya mawe ambazo kwa wiki zinakwenda mara mbili, tunahudumia meli za Kontena ambazo zinakwenda kuchukua bidhaa Mtwara.”
Mrisho anasema, hivi sasa wanatarajia kujenga bandari nyingine kwa ajili ya kuhudumia shehena chafu (Dirty Cargo) kwa mfano saruji, makaa ya mawe na shehena nyingine zinazofanana na hizo “lengo ni kuiacha bandari ya Mtwara ihudumie shehena nyingine ambazo sio za aina hiyo ya mizigo.”
Anasema, kwa upande wa maziwa nako wameboresha bandari ya Kemondo, ili kuwezesha meli zinazotengenezwa kwenye Ziwa Viktoria zihudumiwe vizuri, pia Ziwa Tanganyika tayari bandari ya Kalema ujenzi wake umekamilika “ni bandari nzuri na itakuwa bandari kubwa kuliko bandari ya Kigoma.”
Vile vile, anasema tayari wameshasaini Mkataba wa Shilingi Bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mbambabay ili kujenga bandari kubwa zaidi ya kuunganisha Mtwara hadi Mbambabay ili kulifikia soko la Malawi.
Hata hivyo, mbali na mafanikio hayo, Mkurugenzi huyo wa Bandari ya Dar es Salaam anasema, zipo changamoto kadhaa ambazo zinawakabili ikiwemo vitendea kazi na uduni wa miundombinu, ndio maana zipo jitihada zinaendelea za kuhakikisha wanafanya maboresho ili kulifikia soko (nchi zinazohudumiwa na bandari ya Dar es Salaam) kwa ukubwa wake.
Anasema, bandari ya Dar es Salaam ipo kwenye eneo zuri la kuzifikia nchi jirani za Kongo, Zambia, Uganda, Rwanda, Burundi na hivi sasa Zimbabwe, hivyo hakuna sababu ya kuwa na kiwango kidogo cha bidhaa zinazopitia nchini kwenda kwenye nchi hizo za jirani.
“Kama tunaweza kukusanya kiasi kikubwa cha kodi kupitia miundombinu tuliyonayo kwenye bandari zetu, na kama tutaipanua, kodi itakusanywa zaidi ya hapo. Niwape mfano tu, leo (Aprili 29, 2024) kuna meli 34 zinasubiri nje, ndani una meli 12 unazozihudumia, unatoa meli tano au sita, halafu kule ukiamka asubuhi kuna meli nyingine karibu saba mpya zimeingia…meli hazipaswi kusubiri nje, unasubiri nje kwasababu magati yako ni machache na vifaa vyako havitoshelezi,”
Aliongeza, “Kwahiyo lazima ufanye uwekezaji mkubwa kuhakikisha unaongeza magati yako ili meli kama zinasubiri, basi muda wa kusubiri iwe siku mbili au siku tatu, kukaa nje maana yake unaambiwa ongeza miundombinu yako ya magati na vifaa pamoja na yadi ili meli ziharakishwe kuhudumiwa.”
Changamoto nyingine ambayo aliweka wazi, ni miundombinu ya usafirishaji, ambapo anasema wakati TPA wanapambana kutatua changamoto za bandari, wanakutana na wadau wengine wa barabara na reli ambazo zinatumika kupitishia mizigo kupeleka kwenye soko.
“Hivi sasa mzigo unaotoka bandarini, foleni inaanzia hapo hadi Kimara. Kama barabara ni zile zile zilizokuwa na uwezo tangu wakati huo, lazima tuende haraka kuhakikisha barabara zetu zina uwezo wa kupambana na uwezo wa kiasi cha mzigo unaoongezeka kila leo kwenye bandari ya Dar es Salaam,” anasisitiza na kuongeza kuwa, kuna mpango wa kuunganisha reli tatu ambazo zinaingia bandarini.
Mrisho anasema, katika jitihada za kutatua changamoto hizo na kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kubwa zaidi, wamejipanga kuongeza gati; namba 12 na 15 na tayari mchakato umeshakamilika, kilichobaki ni utafutaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi huo.
“Pia, tupo kwenye mazungumzo na wenzetu wa NAVY upande wa pili wa bandari, ili tuende tukalichukue eneo lao la hekari 400, tukifanikiwa katika mradi huo tutajenga magati matano na eneo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia Kontena Milioni 1.6 kwa mwaka, pia geti namba 12 hadi 15 tukimaliza mradi huo, tutakuwa na uwezo wa kuhudumia Kontena Milioni 1.3.”
Anasema, eneo jingine ambalo wanatarajia kulindeleza lipo Shimo la Udongo, Kurasini jijini Dar es Salaam “tumepewa na Serikali tunamshukuru Rais, kila mmoja anasema kwanini Parachichi likahudumiwe Mombasa badala ya bandari ya Dar es Salaam, kwahiyo hapo tutakuwa na kituo chenye huduma zote.”
Mkurugenzi huyo wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Mrisho anasema, kama watafanikiwa kutatua changamoto hizo chache, watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuhudumia shehena kubwa zaidi na kuongeza Mapato kuliko hivi sasa na TRA watapata wigo mkubwa wa kukusanya kodi.