Maandalizi yapamba moto Tamasha la Sanaa Bagamoyo

0

Na Albert Kawogo, Bagamoyo

PAZIA la tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo linatarajiwa kufunguliwa kesho Jumatano katika viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni TASUBA.

Tamasha la mwaka huu ni la 43 tangu lilipoanzishwa rasmi mwaka 1981 na linaelezwa kuwa ni moja ya tamasha kongwe la Sanaa katika bara la Afrika.

Naibu Waziri wa Habari na Utamaduni Hamisi Mwinjuma amezungumza leo kwenye Mkutano wa Waandishi wa habari uliofanyika TASUBA Bagamoyo na kubainisha kuwa, Tamasha la mwaka huu litakuwa kubwa zaidi na zuri kutokana na maandalizi mazuri ubora wa kazi za sanaa pamoja na viwango vizuri vya vikundi na wasanii walioalikwa.

Naibu Waziri Mwinjuma alisema, moja ya dhima muhimu katika siku nne za tamasha ni kuliunganisha tamasha hilo na vivutio vya utalii vya mji mkongwe wa Bagamoyo.

“Pamoja na umuhimu mkubwa uliopo kwenye tamasha hili kubwa lakini nia yetu thabiti ni kuona namna gani tamasha hili linaweza kuwa sehemu ya kuutangaza mji huu wa Bagamoyo vivutio vyake vya utalii na ile mbuga ya Saadan, ” alisema Naibu Waziri.

Aidha, Mwinjuma alisema Serikali inalitafakari ombi la kulirudisha tamasha hilo liwe la siku saba kama ilivyokuwa awali badala ya siku nne, huku akisisitiza kuwa iwapo itakuwa hivyo itatoa fursa ya vikundi vingi kushiriki.

Naibu Waziri amewataka Watanzania na wageni mbali mbali kuja Bagamoyo kwa ajili ya kushiriki na pia kuona tamasha hilo ikiwa ni fursa muhimu ya kujua kazi mbalimbali za sanaa za kitanzania na zile za kutoka nje ya nchi.

Awali, akiwasilisha taarifa fupi kuhusu tamasha hilo Mtendaji Mkuu wa TASUBA Dk Hebert Makoye alisema jumla ya vikundi 71 vimealikwa kushiriki ambavyo vitatoka Tanzania bara na Zanzibar na vingine vikitoka nje ya nchi

Dkt. Makoye alisema, vikundi hivyo vitahusisha sanaa za ngoma muziki maigizo sarakasi mazingaombwe pamoja na Sanaa za ufundi

Alisema, kutakuwa na maonyesho ya filamu, makongamano sambamba na fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vya Bagamoyo.

Tamasha hilo linatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Michezo Sanaa na Utamaduni Dkt. Damasi Ndumbaro na kufungwa Oktoba 26, 2024 na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Dkt. Tulia Ackson.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here