Na Eleuteri Mangi, WUSM
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeunga mkono kazi za Sanaa ambazo zinasimamiwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutoa tisheti 300 kwa washiriki wote wa Tamasha la World Happy Deaf Family Festival 2023.
Hatua hiyo utekelezaji wa Sera ya Huduma kwa Jamii (CSR) ya shirika hilo ambayo lengo lake ni kuwahudumia sekta za huduma za jamii pamoja na makundi mbalimbali ikiwemo makundi maalum.
Akikabidhi tisheti hizo Novemba 26, 2023 jijini Dar es salaam, Muungano Saguya Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba (NHC) alisema wanaunga mkono juhudi za Serikali kwa washiriki wa Tamasha la World Happy Deaf Family Festival 2023 ambalo limeshirikisha viziwi wa kiume na wa kike.
“Tunaamini tisheti hizi zitasaidia kutangaza jina la Tanzania na Shirika letu la Nyumba la Taifa katika mataifa yenu mnapotoka ili zisaidie kuwavutia wawekezaji wakubwa watakaoshirikiana na Shirika letu ambao wanapenda kufanya uwekezaji mkubwa nchini Tanzania na muwe mabalozi wema wa nchi yetu huko mnapotoka” alisema Saguya.
Katika mashindano hayo, Nashua Patience kutoka Uganda ameibuka mshindi wa kwanza na kutwaa taji la mrembo kwa mwaka 2023 huku nafasi ya mtanashati katika mashindano hayo ikinyakuliwa na Ariko David kutoka Uganda wakati Mtanzania Caroline Mwakasaka akiibuka mshindi wa nafasi ya pili kwa upande wa shindano la Mwanamitindo Bora “modal”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanaitangaza Tanzania katika mataifa 40 kupitia tisheti walizowapa washiriki hao.
Aidha, washiriki hao wa Tamasha la World Happy Deaf Family Festival 2023 wamefanya pia ziara katika fukwe za Coco Beach jijini Dar es salaam na kupata vyakula vya asili ya kitanzania hatua ikiwa na fursa ya utalii wa kiutamaduni ambayo ni sehemu ya kukuza kipato na kuongeza uchumi wa wafanyabiashara ya kitanzania na kuongeza pato la Taifa.