BERLIN, Ujerumani
MWANARIADHA Eliud Kipchoge ameweka rekodi mpya ya dunia ya mbio za Kilomita 42 baada ya kushinda Berlin Marathon kwa saa 2:01:09 mjini Berlin, Ujerumani, mwishoni mwa wiki.
Kipchoge, ambaye atagonga umri wa miaka 38 hapo Novemba 5, alifuta rekodi yake ya 2:01:39 ambayo aliweka akishinda taji la Berlin Marathon mwaka 2018.
Bingwa huyo wa Olimpiki 2016 na 2020 aliongeza taji hilo lake la nne la Berlin baada ya kukimbia kipindi chote ndani ya muda wa rekodi ya dunia alipopita Kilomita 21 kwa dakika 59:36, Kilomita 25 kwa saa 1:11:07, kilomita 30 kwa saa 1:25:40, Kilomita 35 kwa saa 1:40:10 na Kilomita 40 kwa saa 1:54:49.
Kipchoge, ambaye ameshinda marathon 17 kati ya 19 ameshiriki, anajivunia mataji ya Berlin Marathon mwaka 2015, 2017, 2018 na 2022.
Bingwa huyo anayelenga kushinda marathon zote sita kubwa za kifahari kabla ya kustaafu alifungua mwaka kwa kubeba taji la Tokyo Marathon kwa 2:02:40 mnamo Machi 6.
Ameshinda pia London Marathon mara tatu na Chicago Marathon mara moja. Imebaki sasa na New York Marathon na Boston Marathon atimize lengo lake la kushinda marathon zote sita kuu.
Kipchoge, ambaye marathon mbili alizokosa kushinda ni Berlin Marathon 2013 alipokamata nafasi ya pili na London Marathon 2020 alipomaliza nambari nane, pia ndiye binadamu pekee kuwahi kukamilisha Kilomita 42 chini ya saa mbili alipomaliza mbio maalum za INEOS1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 mwaka 2019.