LONDON, Uingereza
KINDA Ethan Nwaneri aliingia kwenye kumbukumbu za historia za ‘Guinness World Records’ baada ya kuwa mchezaji mdogo zaidi duniani kuwahi kuchezeshwa katika ligi yoyote kuu.
Nwaneri aliweka historia hiyo alipoingia uwanjani dakika ya 80 katika mechi dhidi ya Brentford, akiwa na umri wa miaka 15 na siku 181.
Kinda huyo amekuwa akifanya vizuri katika Akademia ya Arsenal kama kiungo mshambuliaji, nyota yake iking’aa zaidi alipopandishwa hadi kikosi cha wachezaji wasiozidi miaka 18 miezi michache iliyopita, licha ya kuwa na umri mdogo.
Aliingia uwanjani Brentford Community dakika ya 80 akiwa amevalia jezi nambari 83 na kuchukua nafasi ya Fabio Viera, wakati wa pambano hilo ambalo Arsenal ilipata ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Brentford.
Kinda huyo alivunja rekodi ya Cesc Fabregas, ambaye alichezea Arsenal kwa mara ya kwanza dhidi ya Rotherham United mnamo Oktoba, 2003.
Wakati huo, Arsenal bado walikuwa wakiandaa mechi zao za nyumbani katika uwanja wa Highbury.
Aidha, Cesc alikuwa miaka 16 na siku 177 wakati huo; aliichezea Arsenal ‘The Gunners,’ mechi 303 na kufunga jumla ya mabao 57.
Ethan hakuwa amezaliwa Cesc akiweka rekodi hiyo kwani alitua duniani Machi 21, 2007, baada ya Gunner’s kuhamia Emirates mnamo 2006.
Nwaneri sasa ndiye mchezaji mdogo kuwahi kucheza katika EPL. Alivunja rekodi ya Harvey Elliot alipowajibishwa na Fulham mnamo Mei, 2019 akiwa na umri wa miaka 16 na siku 30.
Kabla ya Elliot, Jack Wilshere, ambaye kwa sasa ni kocha wa Ethan katika timu ya Arsenal chini ya miaka 18, alishikilia rekodi hiyo.
Wilshere alikuwa na umri wa miaka 16 na siku 256 alipopewa nafasi katika mechi dhidi ya Black Burn mnamo Septemba 2008.
Nwaneri pia amechezea vikosi vya wachezaji wa Arsenal chini ya miaka 18 na 21. Arsenal ndicho kikosi kichanga zaidi EPL, umri wa wastani wa 23.8. Inakisiwa Gunners inamlipa Nwaneri pato la Shilingi Milioni 18 kila mwezi.