Na Togolani Edriss Mavura
KIONGOZI rahimu, kiongozi jasiri, kiongozi mnyenyekevu, kiongozi muungwana, kiongozi mzazi na mlezi ndio sifa zinazomtambulisha Hayati Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyejaaliwa kuishi na kuona kizazi cha nne (Marais wanne) cha uongozi mbele yake.
Hayati Rais Mwinyi ni kiongozi mwenye karama ya kipekee. Amekuwa Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo ni nadra kutokea. Utulivu wake, urahimu wake na ujasiri wake, uliwezesha Zanzibar, na baadae Tanzania kuyaendea mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa.
Katika nyakati zote, alipokea nchi katika mazingira magumu sana. Alikuwa Rais wa Zanzibar baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya siasa Zanzibar’ na kujiuzulu kwa Hayati Rais Aboud Jumbe. Akawa Rais wa Tanzania akiipokea nchi ikiwa ‘hoi bin taaban’ kiuchumi, ikiwa haina bidhaa madukani, wala akiba ya fedha za kigeni.
Katika nyakati zote mbili, alipokea dhima kwa unyenyekevu mkubwa, hakulaumu waliomtangulia, alilinda stara yao, na alifanya mageuzi makubwa bila kubeza yaliyokwishafanyika.
Hayati Rais Mwinyi ameonyesha kuwa ujasiri na maamuzi magumu yanaweza kupatikana bila ya lugha kali, mkono wa chuma na kumwaga damu za watu. Alifungua uchumi wa Zanzibar, na akafungua uchumi na siasa za Tanzania.
Ndiye aliyeruhusu uchumi wa soko kupitia ‘Azimio la Zanzibar’ na ndiye aliyeunda Tume ya Nyalali, kuruhusu Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na kuruhusu Uhuru wa Habari na vyombo binafsi vya habari. Rais akaanza kuandikwa, kujadiliwa hadharani na hata kuzushiwa, wakati huo tukianza na gazeti la Motomoto.
Hayati Rais Mwinyi anabaki kuwa kielelezo cha uwajibikaji nchini Tanzania. Alionyesha uwajibikaji kwa mfano alipojiuzulu bila shuruti wala manung’uniko baada ya kadhia ya mauaji kule Shinyanga. Wakati wa Urais wake, aliwahi kuvunja Baraza la Mawaziri kuonyesha kuwajibika kwa umma kutokana na tuhuma mbalimbali zilizoikabili Serikali yake.
Hayati Rais Mwinyi alikuwa Mwanademokrasia. Itakumbukwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi ulifanyika jijini Dar es Salaam, ukiwa ni uchaguzi mdogo wa Udiwani na mgombea wa upinzani Dkt. Masumbuko Lamwai wa NCCRi alishinda na alitangazwa. Tukawa na diwani wa kwanza kutoka upinzani.
Kwa upande wa diplomasia yetu, Hayati Rais Mwinyi alifanya mengi na makubwa ikiwemo kurejesha imani ya wawekezaji na wahisani wa maendeleo, kumalizia kiporo cha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere cha ushiriki wetu kwenye harakati za ukombozi katika nchi za Namibia na Afrika Kusini, usuluhishi wa mgogoro wa Rwanda, kuirejesha Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kuanzisha mahusiano na Jamhuri ya Korea.
Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi atakumbukwa kwa busara na nukuu nyingi. Nitamkumbuka kwa nukuu yake aliyoitoa katika hotuba yake bora sana ya ‘Twende na Wakati’ aliyoitoa kwa Wazee wa Dar es Salaam akifafanua ‘Azimio la Zanzibar’. Alisema, “Kama hatukwenda na wakati, kazi yetu itakuwa ni kufukuzia wakati – jambo ambalo hatulimudu.
Tabia ya wakati ni kama ile ya bahari. Bahari inakupwa na kujaa mpaka ukingoni mwa maji. Baadaye maji hukupwa polepole, mpaka kufika wakati ikawa maji yote yamekwishaondoka ufukoni. Samaki werevu huondoka nayo hayo maji, yaani yakijaa huja nayo, yakitoka kutoka nayo, vinginevyo hupwelewa. Samaki watakaozembea kufuata maji watajikuta wamechelewa wanatapatapa juu ya mchango wakati maji hayo hayapo. Hiyo ndiyo maana ya kupwelewa”.
Maisha yake ni funzo kubwa kwetu sote. Ametuachia alama na sadaka zinazoishi. Ametuachia hadithi nzuri. Alikuwa mtu nadra. Amefariki siku nadra ya Februari 29, 2024 ambayo huja mara moja katika miaka minne. Hatudai. Hatumdai. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi mahala pema peponi.
*Mwandishi wa makala hii ni Balozi wa Tanzania, Korea Kusini.