Hizi ni dalili njema za mafanikio ya Mageuzi ya kiuchumi ya Dkt. Samia

0

Na Derek Murusuri, Dar es Salaam

UWEKEZAJI wa umma kwenye mashirika, duniani kote umekuwa msingi imara wa kuzisaidia Serikali za nchi kupata raslimali fedha, zinazotumika kuchochea ukuaji na maendeleo ya uchumi.

Tanzania imefanya uwekezaji wa takriban Trilioni 76 katika mashirika. Huu ni uwekezaji mkubwa kiasi cha kuifanya Tanzania kuwa mojawapo ya Mataifa yenye uchumi mkubwa barani Afrika.

Ndio maana, uanzishwaji wa Mamlaka ya uwekezaji wa Umma, ni mageuzi makubwa yanayoweza kuleta tija kubwa nchini.

Huu ni ushahidi wa wazi kuwa, Mageuzi makubwa ya kiuchumi, yanayoongozwa na 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuild) za Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanakwenda kuibadilisha Tanzania ndani ya miaka michache kuongoza uchumi wa Afrika Mashariki na baadaye Afrika.

Gawio na michango ya Shilingi Bilioni 637 ambayo imetolewa hivi karibuni na matarajio ya kuongezeka zaidi kufikia Shilingi Bilioni 850 miezi kadhaa ijayo, ni habari mbaya sana kwa wanaobeza mageuzi ya kiuchumi ya Rais Dkt. Samia. Kila mwenye macho ameanza kuona.

Kuona ni kuamini. Mzee John Samwel Malecela, alizoea kusema wapo watu wanaotaka kuchuna ngozi ya kiroboto. Wale wanaojitia upofu angali wanaona. Hakika mageuzi ya kiuchumi ya Dkt. Samia yameanza kuzaa matunda.

“Mheshimiwa Rais kuna mambo mengi ambayo yamefanyika katika kuitikia wito wako na kutekeleza maono yako ya kuleta mageuzi katika utendaji kazi mahali popote penye uwekezaji wa Umma, lakini itoshe kusema kuwa, leo sio siku yetu ya kuzungumzia tuliyoyafanya kwakuwa leo ni siku maalumu ya kupokea gawio (Tanzania Dividend Day),” anabainisha Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mashirika ya umma na yale ambayo Serikali ilikuwa na hisa kidogo, kujumuika pamoja na kutoa gawio na michango kwa Serikali ya Tanzania. Huu ni ushahidi wa kufanikiwa kwa falsafa ya 4R ya Dkt. Samia na kuongezeka kwa tija kutokana na ufanisi katika usimamizi bora wa mashirika. Hongera Mchechu na timu yako.

Mashirika yachangia baada ya miaka 10

Yapo mashirika mengine kama MCC, ambayo kwa miaka 10 yalikuwa hayajatoa gawio. Leo imewezekana. Hii ni kutokana na uongozi wa mabadiliko na ufanisi, ndio uliowezesha mashirika 145 kuchangia. Idadi hii ni ongezeko la mashirika 36 kutoka mashirika 109 ambayo yalichangia mwaka 2023.

Kwa mwenendo huu, mashirika mengine 159 ambayo hayakuchangia safari hii, hayapaswi kubaki nyuma, yahakikishe yanachangia mwakani. Dhana ya mabadiliko italeta tija katika kubuni, kuongeza bidii na ufanisi ili kuendelea kuaminiwa. Ndio maana uamuzi wa kuanzisha Mamlaka wa Uwekezaji wa Umma ni muhimu kwa ajili ya kuleta tija katika uendeshaji wa mashirika ili kuleta faida.

4R na Shareholder Wealth Maximization (Kuongeza Faida kwa Mwenyehisa)

Hii ni dhana ya kawaida katika biashara. Ipo hata katika biblia. Inahusu aliyepata talanta moja hadi tano. Mashirika yana jukumu la kupata faida na kuongeza faida kwa mwenye hisa. Yanapaswa kurudisha sehemu ya faida.

“Huu ni ushahidi kuwa 4R za Dkt. Samia tayari zimeanza kuonesha mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuteua viongozi wazuri wenye sifa ya utendaji wenye matokeo kama Mchechu, toka akiwa Benki ya CBA ba baadaye NHC,” anasema Profesa Jonathan Stephen.

Mchechu ameweza kuongeza hisa za Serikali kwenye baadhi ya mashirika, kutoka 15 hadi 20, hivyo kuiongezea Serikali faida. Mashirika 304 ambayo yako chini ya uongozi mahiri wa Wizara na Msajili wa Hazina, yanatarajia kufikia asilimia 10 ya mapato ya kikodi. Gawio na mageuzi yanadhihirisha kuwa mapato yanaweza kuwa makubwa zaidi.

Mashirika haya yanachangia katika bajeti ya taifa kwa mapato yasiyo ya kikodi kwa asilimia 3. Wastani wa changizo katika Afrika ni asilimia 6, lakini Mchechu anaona inawezekana yakachangia hadi asilimia 10, ikiwezekana hata zaidi ya hapo.

Mchango wa Mashirika kwenye Uchumi wa Nchi

India ni mojawapo ya Mataifa ambayo mashirika yake ya umma yana mchango mkubwa katika kuipatia Serikali yao raslimali fedha pamoja na ajira kwa wananchi wake. Hii ni pamoja na kuweka msingi mzuri wa viwanda nchini mwao. Ndio maana uchumi wa India sasa unaelekea kuwa uchumi mkubwa wa tatu duniani, kutoka wa tano sasa, baada ya miaka michache.

Ilichukua takribani miaka thelathini baada ya uhuru kwa nchi yetu kufanya mageuzi ya uendeshaji wa Mashirika ya umma chini ya usimamizi wa IMF na WB. Mageuzi ya “SAP,” ndiyo yaliyo ufungua uchumi wa Tanzania baada ya vita vya Kagera.

“Sasa tunashukuru kuwa miaka thelathini baadaye Mheshimiwa Rais, umeanzisha mageuzi kwa awamu ya pili, bila kusubiri kuambiwa ama kusurutishwa na mabwana wakubwa hawa…(WB na IMF),” anasema Mchechu.

Siku ya Gawio Tanzania

Dkt. Samia aliridhia ombi la Msajili wa Hazina kuwepo na Siku ya Gawio nchini, katika miezi ya Mei mwishoni au Juni mwanzoni kila mwaka.

Mageuzi yataleta Mafanikio makubwa

Mageuzi na kujenga upya chini ya 4R za Dkt. Samia, yanakwenda kuupaisha uchumi wa Tanzania. Bwawa la Julius Nyerere likiwa tayari limeanza kuzalisha umeme na treni ya umeme ikiwa imeanza safari zake kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, hakika miradi hii mikubwa ya kimkakati ni hamasa kuwa makubwa zaidi yanawezekana.

SGR ya Tanzania ambayo, ikikamilika, itakuwa reli ndefu ya kuliko zote barani Afrika. Pia, itakuwa ya tano kwa urefu duniani.

“Serikali katika kujenga uchumi na maendeleo endelevu ya nchi, basi mabadiliko ya kiusimamizi, kiutendaji na kiuendeshaji hayaepukiki,” anatanabaisha guru wa mabadiliko, Nehemiah Mchechu.

Mamlaka ya uwekezaji ya umma

Muswada wa sheria ya Mamlaka ya uwekezaji wa mashirika ya umma utakapokuwa sheria, Tanzania itafurahia uwekezaji wa matrilioni ya shilingi katika mashirika yake. Haya ni maono ya Dkt. Samia, akisaidiwa na Prof. Kitila Mkumbo pamoja na Dkt. Mchechu.

Hitimisho:-

Mageuzi haya ni ya ndani. Yanafanyika miaka zaidi ya 30 baada ya mageuzi yaliyoletwa na Benki ya Dunia (WB) pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Miaka mitatu tu ya Dkt. Samia, mageuzi makubwa ya kiuchumi yanafanyika. Matunda yanapatikana. Utegemezi unaendelea kupungua.

Mamlaka ya uwekezaji wa umma itakapoanza kazi, mapato ya nchi yatazidi kupaa. Ustawi na maendeleo ya uchumi wa Tanzania utashamiri. Tija itaonekana zaidi.

Hii ina maana gani? Wasomi na viongozi wazalendo wanaoweza kusimamia ustawi na maendeleo ya uchumi wetu wako kazini. Kwamba, bila ushawishi wa mabwana wakubwa, Tanzania inaweza ikaasisi mageuzi yake, ikayafanyia kazi na kuwatoa wananchi wake katika umasikini.

Maana yake ni kwamba, mageuzi na kujenga upya vimejaribiwa na kuzaa matunda. Kupitia hizi 4R, Tanzania inaweza kuibuka Taifa lenye uchumi mkubwa zaidi katika Afrika. KAZI IENDELEE.

*Mwandishi wa makala hii ni Mchambuzi wa masuala ya biashara na uchumi. derek.murusuri@yahoo.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here