Ni sahihi kumsifia Rais Samia?

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Na Emmanuel Shilatu

WAPO wanaosema anayoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Serikali yake juu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ni sehemu ya kutimiza wajibu wake, hapaswi kupongezwa; Wengine wanasema anayoyafanya hayastahili kutangazwa na wala hastahili kusifiwa, kwani tutamfanya aanze kuharibu; ila wapo wengine wanaona anastahilikutiwa moyo na kupongezwa.

Kila Mtu ama kundi la Watu lina mitazamo yake. Nimekusanya mitazamo yote na mwisho wa siku nami nikajiuliza; Je, ni sahihi kumsifia Rais Samia kwa yale anayoyafanya? Nasema, ni sahihi kabisa kwa Watanzania kumsifia Rais Samia kutokana na sababu zifuatazo;

Mosi; Watanzania wanayo haki ya Kikatiba kwa mujibu wa Ibara 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa uhuru wa kutoa maoni na mawazo. Kumsifia Rais Samia, ni sehemu ya Wananchi kutimiza haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni na mawazo yao.

Pili; Watanzania wana haki yao kabisa kumsifia Rais Samia anayetimiza wajibu wake wa kutekeleza ahadi za Serikali walizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2020 – 2025 inayotokana na ilani ya uchaguzi. Kusema utafanya ni kitu kingine, kutekeleza ahadi yako ni jambo lingine. Kumpongeza Rais Samia kwa kutimiza ahadi zake ni sehemu ya kuonyesha, kukubali na kumuunga mkono kile anachokifanya.

Tatu; Wananchi wana haki ya kujivunia kumpongeza Rais Samia ambaye anaiongoza vyema Serikali yake inayotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukusanya kodi ipasavyo. Kodi hizo hizo zinazokusanywa ndizo hizo hizo zinazoenda kutuletea maendeleo Watanzania.

Nne; Watanzania wanayo haki ya kujivunia kumpongeza Rais Samia kwa kuhakikisha anatumia vyema kodi inayokusanywa kwa kuwaletea maendeleo Wananchi. Mathalani ununuzi wa ndege, Ujenzi wa vivuko, ujenzi wa reli ya kisasa ya standard gauge, ujenzi wa miundombinu ya madaraja, barabara, Madarasa yote ni matunda ya matumizi sahihi na makini ya kodi zinazokusanywa. Mama anaupiga mwingi si vibaya akisifiwa kwa sauti pana na kwa herufi kubwa.

Narudia tena kusema, kumsifia Rais Samia kwa mema anayoyafanya kwa Taifa ni sahihi kabisa, ni sehemu ya uzalendo wenyewe wa Mtanzania kwa Taifa lako.

Kama tunaona barabara zinajengwa, madaraja yanajengwa, vivuko vipya vya kisasa vinazinduliwa, ndege mpya zinanunuliwa, reli ya kisasa inaendelea kujengwa, Madarasa yanajengwa, elimu bure inatolewa, dawa hospitalini zipo, umeme umesambazwa mpaka vijijini, diplomasia inazidi kuimarishwa na mengineyo mengi tu kwanini Watanzania tusijivunie kumpongeza Rais Samia?

Nahitimisha andiko hili kwa kumpongeza Rais Samia kwa uzalendo wake kwa Taifa, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi inayowaletea maendeleo Watanzania na kuendesha nchi vyema kwa mujibu wa katiba ya nchi. Najivunia kumsifia Rais Samia. Tuendelee kumpongeza na kumtia moyo kwa mema yake anayoyafanya kwa Taifa na kwa Watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here