📌 Yaelezwa lengo ni kutaka kumchonganisha na Mamlaka za uteuzi
📌 Ni mpango unaosukwa na wafanyabiashara na wanasiasa
INAELEZWA, tuhuma zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hivi sasa zikimuhusisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata, zina lengo la kumchonganisha kiongozi huyo na Mamlaka ya uteuzi ili aondolewe kwenye nafasi hiyo.
Mbali na lengo hilo, pia lipo genge la wanasiasa ambalo linataka kuhakikisha wanavuruga morali ya watendaji wa TRA na kushusha mapato, ili wapate nguvu ya kisiasa na kuharibu kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Taarifa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali zinaonyesha kuwa, mkakati huo kwa kiasi kikubwa unaongozwa na baadhi ya wafanyabiashara wanaotajwa kuwa ni vinara wa kukwepa kodi, ambao wanataka kuhakikisha nafasi hiyo inashikwa na mtu ambaye atalinda maslahi yao.
Wafanyabiashara hao, wanachochea migomo na kutengeneza propaganda mitandaoni kwa kuwatumia baadhi ya watu ambao wamewalipa kiasi kikubwa cha fedha, ili kuonyesha kwamba, uongozi uliopo hivi sasa chini ya Kidata, hauna mahusiano mazuri na wafanyabiashara, hivyo yanatakiwa mabadiliko ya kuweka safu nyingine ambayo itakuwa ‘rafiki’ kwao.
“Kama unavyoona hivi sasa mitandaoni kuna vita kubwa inaendelea ambayo inalenga kushawishi Mamlaka ya uteuzi imuondoe Kidata ili aingie (anamtaja jina) mtu ambaye ataruhusu wao kufanya mambo yao bila kikwazo,” alisema mtu mmoja ambaye yupo karibu na wanaoratibu mpango huo aliyezungumza na Afrika Leo kwa sharti la kutotajwa jina.
Alisema, kundi hilo halipendezwi na uongozi wa Kamishna Kidata ambaye amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuziba mianya ya wafanyabiashara ambao walizoea kujinufaisha kutokana na mianya iliyokuwepo ya ukwepaji wa kodi na matumizi ya rushwa ili kufanikisha mipango yao.
“Wanakiri wazi kwamba, Kidata ni mwiba kwao na amekuwa kikwazo, hivyo ni lazima ang’ooke kisha aje Kamishna mwingine ambaye ni mtu wao ili wapate nafasi ya kufanya mambo yao, kwahiyo wanafanya yote haya kwasababu ya maslahi yao binafsi, maana unashangaa katika kipindi hiki ambacho makusanyo yameongezeka na TRA inafanya vizuri, wanaibuka watu wanataka aondolewe unajiuliza kwa kosa gani?” alihoji.
Aliendelea kusema: “Ila ukiangalia mambo yote ambayo anatuhumiwa nayo (Kidata) hakuna hoja za msingi, kwani yeye anachofanya ni kusimamia sheria zilizotungwa na Bunge, sasa wanapomlaumu wanamuonea tu, lakini ninachokiona, kuna wafanya biashara wakwepa kodi walitarajia wanaweza kumuweka mfukoni, lakini mambo yamekwenda tofauti, Kamishna hacheki na wakwepa kodi na ameziba mianya ya rushwa na ukwepaji wa kodi ndio maana wanamuhujumu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Aidha, taarifa zaidi zinadai kwamba, wanasiasa wakiwemo wa baadhi ya vyama vya upinzani ambao nao wamejitosa kwa siri kuchochea mpango huo, wanataka kumuharibia Rais Dkt. Samia ambaye ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake, TRA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupaisha mapato.
Inaelezwa, wapo wanasiasa ambao hawana nia njema na uongozi uliopo madarakani, wanaona iwapo kasi ya ukusanyaji wa mapato itaendelea, Rais Samia atapata nguvu zaidi ya kisiasa na kiuchumi, hivyo itakuwa vigumu wao kutimiza malengo yao ya kisiasa.
Takwimu zinaonesha kuwa, TRA chini ya Kidata imefanikiwa kuongeza makusanyo, ambapo Desemba 2023 pekee TRA ilivunja rekodi ya makusanyo ya Serikali hadi kufikia Shilingi Trilioni 3.05 ambayo ni sawa na asilimia 103 ya lengo la msingi lililokuwa limewekwa.
Itakumbukwa, wakati Kidata anashika nafasi hiyo, TRA ilikuwa inakusanya Shilingi Bilioni 700 hadi 800 kwa mwezi kwa kipindi cha 2016/2017, lakini aliingoza TRA kukusanya kati ya Shilingi Trilioni 1.2 hadi 1.5 kwa mwezi.
“Makusanyo haya hayajawahi kufikiwa na Makamishna wote waliowahi kupita kwenye mamlaka hiyo, kwani hivi sasa wastani wa TRA kukusanya kodi kwa mwezi unafikia Trilioni 2,” kilisema chanzo chetu kingine.
Kiliendelea kusema: “Kuna watu wanataka Rais Samia afanye mabadiliko na kuwatoa watendaji wa TRA akiwamo Kamishna Mkuu ambaye amefanya kazi kubwa sana ya kupaisha mapato, wanaamini yakifanyika mabadiliko, mapato yatashuka na mambo kwa upande wa Serikali yataharibika, jambo ambalo Rais na wanaomshauri wanapaswa kuwa makini nalo, wasisikilize propaganda zinazoendelea mitandaoni.”