Rais Samia aagiza kero za wachimbaji wadogo zitatuliwe

0

SERIKALI ipo mbioni kutunga kanuni za kushughulikia migogoro kati ya wamiliki wa leseni na wenye maduara.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde mkoani Shinyanga katika Kijiji cha Mandu, machimbo ya Ntambalale Wilayani Kahama alipotembelea kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo.

Alisema, Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuhakikisha kero zote zinazowakabili wachimbaji wadogo zinatatuliwa ili wafanye shughuli zao bila migogoro yoyote.

“Ndiyo maana, leo nimefika hapa kuja kuwasikiliza ndugu zangu ili kutatua changamoto zenu, kufuatia migogoro ya kila wakati,” alisema na kuongeza, wenye Leseni kuanzia Julai 2024 zitaangaliwa upya.

“Tukikupa Leseni tunaamini wewe mmiliki wa leseni ndio mchimbaji, iwapo mmiliki wa leseni yeyote ambaye atawakaribisha wachimbaji kwenye leseni yake, ahakikishe anaingia mikataba itakayokuwa inatambua wenye maduara na uwekezaji waliouweka.

“Ikitokea mmiliki wa leseni anataka kuuza au kuingia ubia na mwekezaji, basi kila mmoja apate haki yake inavyostahili”, alisema Mavunde.

Kuhusu msaada wa kiufundi (Technical Support) ambao uliwekwa kwa ajili ya kujenga uwezo kwa wachimbaji wadogo, Mavunde amesema Wizara inakwenda kuangalia vizuri Kanuni ili ziweze kuendana na makusudio ya utungwaji wake.

Aidha, alisema kwa msaada wa kiufundi ni lazima uendane na kuongeza matumizi ya teknolojia katika uchimbaji mdogo, na si ilivyo sasa ambavyo inatafsiriwa kama ni kitendo cha kuuza leseni kwa wawekezaji na kuwaondoa wachimbaji wadogo huku matumizi ya teknolojia duni yakiendelea, hilo haliwezekani na Serikali haiwezi kulifumbia macho.

Katika hatua nyingine, Mavunde amechukizwa leseni za vikundi kuuzwa pasipo idhini au makubaliano ya wanakikundi wote na kuahidi kwamba kuanzia Mwezi Julai, 2024 leseni zote zitakazotolewa kwa vikundi kutoka Serikalini, hazitaruhusiwa kuingia mwekezaji pasipo kupata ridhaa kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, ili changamoto zisiendelee kujirudia.

Kuhusu suala la utoroshaji wa madini, Mavunde, ameahidi kuwa anakwenda kuongeza nguvu katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama ili kuendelea kupambana na vitendo vya utoroshaji kwa kuwa mkoa huo umekua kitovu cha vitendo vya utoroshaji wa madini.

Aidha, ameagiza Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi na Afisa Madini Mkazi wa Kahama wakae pamoja na kupitia tozo zote zilizoonekana kuwa kero ili kuondoa mzigo mkubwa kwa wachimbaji wadogo.

Nae, Mbunge wa Jimbo la Msalala Idd Kassim amemshukuru Mavunde kwa kusikiliza kero za wachimbaji na kuzipatia ufumbuzi na kutumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa jitihada zinazoendelea za kuboresha mifumo mbalimbali ya kuongeza ufanisi katika sekta ya Madini.

Awali, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Mhandisi Joseph Kumburu akijibu baadhi ya hoja za wachimbaji alisema wataendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusiana na tozo na ushuru mbalimbali ambazo wanatozwa kwani zilizopo ni zile walizokubaliana kwa mujibu wa Sheria na si vinginevyo.

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Mhandisi Joseph Kumburu

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha aliahidi kuendelea kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji wa sekta ya madini ambayo ni sehemu ya shughuli kuu za kiuchumi za Mkoa wa Shinyanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here