Na WMA – Pwani
WAKALA wa Vipimo (WMA) umeendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika vituo vya mafuta kuhakikisha wateja wanapata kipimo sahihi cha mafuta wanacholipia, kuanzia bandarini hadi kwa mtumiaji wa mwisho.
Afisa Vipimo kutoka Ofisi mpya ya WMA Mkoa wa ki-vipimo Mkuranga, Fabian Karera, amesema ukaguzi huo hufanyika mara kwa mara hata katika vituo vilivyowahi kukaguliwa, ili kudhibiti udanganyifu katika upimaji wa mafuta.
Karera amesema wateja wanaweza kutambua vituo vilivyokaguliwa kwa kuangalia stika maalumu zinazobandikwa kwenye pampu za mafuta. Stika hizo huonyesha tarehe ya ukaguzi na tarehe inayofuata ya ukaguzi. Kwa mfano, stika iliyopo katika kituo kimoja inaonyesha kuwa ukaguzi ulifanyika Julai 3, 2026, na ukaguzi unaofuata umepangwa Julai 3, 2027.
Ameongeza kuwa pampu za mafuta zina mifumo maalumu ya kuziba na kulinda vipimo ili kuzuia wamiliki wa vituo kuzichezea na kusababisha wateja kupata mafuta pungufu ya kiwango wanacholipia.
Akizungumza wakati wa ukaguzi kwenye Kituo chake, Meneja Msaidizi wa Kituo cha Mafuta cha Admire kilichopo Vikindu, Isack Mohamed, ameishukuru Wakala wa Vipimo kwa kutembelea kituo hicho, akisema ukaguzi huo unaimarisha imani ya wateja kuhusu usahihi wa vipimo vya mafuta wanayonunua.
Naye Rahimu Bumbo, mwendesha bodaboda kutoka Vikindu, ameiomba WMA kuendelea na ukaguzi wa mara kwa mara, akieleza kuwa udanganyifu wa vipimo unaweza kuwaathiri watumiaji wa mafuta.
Bumbo amesema wakati mwingine mteja anaweza kulipia lita mbili za mafuta lakini akapata lita moja na nusu pekee, hali inayowaletea changamoto waendesha bodaboda. Amewahimiza wenzake kuangalia stika za ukaguzi zilizowekwa kwenye pampu kila wanapofika kununua mafuta.
Ukaguzi huo unalenga kulinda haki za watumiaji na kuhakikisha kuwa mafuta yanayouzwa katika vituo yanalingana na kiwango kinachoonyeshwa kwenye pampu.