📌 Atoa onyo kwa wataalamu wanaoshindwa kusimamia miradi kwa ufanisi
WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, ameelekeza kusimamishiwa usajili kwa aliyekuwa Mhandisi Mshauri (Doch Limited) wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (Kilometa 50) iliyobainika kuanza kupata nyufa kabla ya kukamilika na kuiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu utendaji wa Mhandisi Mshauri huyo, ili kubaini iwapo kulikuwa na uzembe au ukiukwaji wa maadili ya taaluma katika usimamizi wa mradi huo.
Pia, Waziri Kadogosa ameelekeza Wizara ya Ujenzi kuunda timu maalumu ya uchunguzi itakayowasilisha taarifa ndani ya siku Saba hatua inayolenga kubaini sababu za barabara hiyo kuanza kuharibika ndani ya kipindi kifupi, pamoja na uwajibikaji wa wataalamu waliosimamia utekelezaji wa mradi huo, hususan katika kuhakikisha ubora wa vifaa vilivyotumika na kazi zilizofanyika unakidhi viwango vilivyowekwa.
Kadogosa ametoa maelekezo hayo Pangani mkoani Tanga wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya miundombinu ya Barabara ya Tanga – Pangani Pamoja na Daraja la Pangani.
Katika hatua Nyingine Waziri Kadogosa ameridhishwa na kasi ya Ujenzi wa Daraja la Pangani na kuwataka kuhakikisha Mradi huo unakamilika kwa wakati, akibainisha kuwa kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji wa mkataba, muda wa kukamilika kwa mradi huo ni Februari 2027.
Amesema Wizara ya Ujenzi itaendelea kufuatilia maendeleo ya mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mwanaidi Rajab amesema kukamilika kwa Daraja la Pangani kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, hususan katika kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa kati ya Mji wa Pangani na maeneo ya upande wa Magharibi, ambako shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea kuvuka eneo hilo.