📌 Milioni 4.5 kwa kila mmoja zakumbwa na makato
📌 Wasiojulikana wadaiwa kusaini fedha za marehemu
Na Mwandishi Wetu
WATENDAJI takribani 109 wa mitaa walioondolewa kazini mwaka 2002 kwa kile kinachodaiwa hawakuwa na sifa, wamekumbwa na changamoto ya makato ya fedha katika malipo ya stahiki zao.
Suala hilo, limeibua maswali kuhusu usimamizi wa fedha hizo, uhalali wa makato yaliyofanyika na uwajibikaji wa Mamlaka na watu waliohusika kusimamia mchakato wa malipo ya watumishi hao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji hao, kila mmoja alipaswa kulipwa Shilingi Milioni 4.5, jambo ambalo kwa watendaji wote takribani 109, walipaswa kulipwa kiasi cha Shilingi Milioni 490.
Hata hivyo, katika mchakato wa malipo hayo, fedha mbalimbali zilikatwa kutoka katika stahiki zao ikiwemo Shilingi 178,000 ambayo inadaiwa ilikatwa moja kwa moja na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na hawakuwekwa wazi sababu ya kukatwa kwake.
Pia, Kamati iliyosimamia madai ya watendaji hao ambao walifungua kesi kwenye mahakama ya usuluhishi na kushinda, iliwakata viwango tofauti tofauti, ambapo wapo waliokatwa Shilingi 500,000, wengine 600,000 na wapo waliokatwa Shilingi 1,000,000.
Inadaiwa, viongozi wa Kamati iliyosimamia madai hayo inayoongozwa na Ahmad Mbilinga iliwaeleza watendaji hao kwamba, ni gharama za ufuatiliaji wa madai na kesi hiyo ikiwemo kumlipa mwanasheria, ingawa zipo taarifa kwamba makubaliano yalikuwa ni Shilingi 250,000 kwa kila mmoja.
Mmoja wa watendaji hao akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema, kwenye moja ya vikao vyao walikubaliana iwapo watalipwa, watatoa Shilingi 200,000 kwa kila mmoja kwa ajili ya kumlipa mwanasheria na Shilingi 50,000 kwa ajili ya ‘Asante’ kwa viongozi hao.
Alisema, baada mchakato wa malipo kukamilika, wakashinikizwa wajaze fomu inayowalazimu kukatwa kiasi cha fedha ambazo hawakukubaliana na wakaambiwa ni kwa ajili ya kuwalipa watendaji wa Halmashauri waliofanikisha kuharakisha malipo hayo na walitajwa.
“Kutokana na hali ya kiuchumi ya watu na kuchoshwa na suala hilo, wengine walikubali na waliokataa wakatishwa kwamba watafuatilia wenyewe, hivyo wengi walikubali kwa shingo upande,” alisema mmoja wa watendaji hao.
Alisema, katika hali ya kushangaza, fedha zao zilipoingia kwenye akaunti zao, walishindwa kuzitoa na walipouliza uongozi wa benki, waliambiwa wamepewa maelekezo na Halmashauri kwasababu wanadaiwa.
Mtendaji huyo alisema, yeye alikwenda kutoa fedha zake Benki ya CRDB, Tawi la Kinondoni, ambapo alishindwa kufanya hivyo hadi alipopewa maelekezo ya kujaza fomu mbili; moja ya kutoa fedha na nyingine ya kuweka kwenye akaunti Namba. 10160320813 yenye Jina la WATENDAJI MWAKA 2002.
“Nilipojaza fomu hiyo nikatoa kiasi cha fedha zilizobaki, lakini ikiwa tayari umekatwa mara mbili, jambo ambalo ni kinyume na makubaliano yetu, inauma sana kwasababu kwanza tumepewa kiasi ambacho hakikidhi ila tukakubali kupokea, lakini bado tena kinakatwa,” alisema kwa masikitiko.
Mbali na makato hayo, uchunguzi zaidi umebaini kuwa, zipo familia takribani nne ambazo wazazi wao walikuwa miongoni mwa wadai, lakini wakafariki dunia kabla ya kupokea fedha zao, wamedhulumiwa haki zao.
Moja ya familia hizo ni ya Mwamvua Zigo, ambaye kwenye moja ya fomu ambazo wamesainishwa watendaji hao na nakala yake ipo, anaonekana amesaini na yapo madai kwamba, fedha zake zilichukuliwa na mtu ambaye hajajulikana.
Mmoja wa watoto wa Mwamvua alipoulizwa kuhusu madao hayo alisema hakuna kati yao aliyesaini, lakini fedha zimechukuliwa bila kuhusishwa na hawakuwa wamekamilisha utaratibu wa kufungua mirathi.
“Hapo ndio unajiuliza, walitoaje fedha? Ni nani aliyesaini? Nadhani ndugu mwandishi ukiwauliza viongozi wa Kamati watakuwa na majibu, lakini hali ndio hiyo, na sio hawa tu, wengi ambao walifariki wakati mchakato haujakamilika, fedha zao zimechukuliwa,” alisema mmoja wa watu wa karibu na familia ya Mwamvua.
Mwandishi wa habari hizi alimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitia simu yake ya mkononi kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa fedha ambazo watendaji hao wamekatwa, lakini mara kadhaa iliita bila majibu.
Kwa upande wao viongozi wa Kamati iliyosimamia suala hilo walisema, fedha zilizokatwa ni kwa ajili ya kulipia gharama za kesi ikiwemo kumlipa mwanasheria ambapo Mwenyekiti Ahmed Mbilinga alipotakiwa kuweka wazi gharama halisi iliyohitajika kwa kuendeshea kesi kwa kipindi chote na malipo ya Mwanashria hakuwa tayari kuweka wazi.
Aidha, alipouliza kuhusu suala la akaunti iliyofunguliwa kwa jina la Watendaji kama anaitambua, awali alionekana kukiri moja kwa moja, lakini baadae alikubali na kusema inatumika kukusanyia fedha hizo na kisha kuwalipa wanaodai akiwemo Mwanasheria.
Hata hivyo, alipotafutwa Mwanasheria aliyesimamia kesi ya madai ya watendaji hao Wakili Saulo Kusakala, alisema hajawahi kulipwa kiasi chochote cha fedha na wahusika, na alipojaribu kuwauliza walimjibu bado wanafuatilia malipo, ingawa ana taarifa hivi sasa malipo ya awamu ya tatu yanaendelea.
Naye, Katibu wa Kamati ya watendaji hao Edmund Lusese alipoulizwa kuhusu madai ya familia ambazo fedha zao zimesainiwa na watu wasiojulikana alisema, wamezungumza na wahusika na watakutana nao kwa ajili ya mazungumzo.
Mwandishi wa habari hizi anaendelea kufuatilia kwa kina zaidi suala hilo na kufuatilia kwenye Mamlaka nyingine ili zijiridhishe kama suala hilo lilifuata taratibu zote ikiwemo makato waliyokatwa watendaji hao.
Mbali na hilo, uchunguzi zaidi unaendelea wa kubaini waliohusika kusaini na kuchukua fedha za watendaji waliofariki na mchakato uliofanyika kutoa fedha kama umekidhi vigezo vinavyohitajika ikiwemo uwepo wa nakala za vyeti vya kifo na nyaraka za mirathi.