Na Oscar Mbuza, Morogoro
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetaja mafanikio mbalimbali iliyoyapata kutokana na kuenzi kwa vitendo maono ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kulinda maliasili za nchi na kusimamia uhifadhi.
Mafanikio hayo yameelezwa mbele ya hadhara ya wakazi wa Mkoa wa Morogoro na mikoa ya jirani wakati wa Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 27 ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika katika Kampasi ya Solomon Mahlangu ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro leo Oktoba 10, 2026.
Akitoa mada katika kongamano hilo, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Malikale katika Wizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita amesema moja ya mafanikio hayo ni suala la uhifadhi ambapo mpaka sasa maeneo yenye ukubwa wa jumla ya kilometa za mraba takribani 307,800 sawa na asilimia 32.5 ya eneo lote la Tanzania yametengwa kwa shughuli za uhifadhi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi huyo, miongoni mwa maeneo hayo yaliyohifadhiwa zipo Hifadhi za Taifa 21, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mapori ya Akiba 29, Mapori Tengefu 23, Maeneo matatu ya Ardhioevu, Mashamba ya Miti ya Serikali 26 na Hifadhi za Nyuki 14.
Ametaja pia uwepo wa Maeneo ya Malikale 158, Makumbusho za Taifa 7 na 35 za Binafsi, Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) 40, Mashamba sita ya Ufugaji wa Wanyamapori, Maeneo 36 ya Uzalishaji wa Wanyamapori na Ranchi sita zinazomilikiwa na Sekta Binafsi.
Akizungumzia fursa za kuleta maendeleo endelevu ya Watanzania kupitia Sekta ya Maliasili na Utalii kupitia Dira 2050, Mkurugenzi Msaidizi Mwita amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa na Wizara ikiwa ni pamoja na kufungamanisha mnyororo wa thaman uliopo katika Sekta ndogo za Wanyamapori, Misitu na Nyuki, Malikale na Utalii.
Aidha, ametaja fursa nyingine za kimaendeleo kuwa ni kuanzisha mashamba ya miti, mashamba ya wanyamapori, ranchi na bustani za wanyamapori, kuongeza thamani katika ufugaji nyuki na kuanzisha kambi za watalii, maduka ya zawadi, kuuza malighafi ya vyakula na bidhaa nyingine kwenye hoteli za kitalii na kuanzisha hoteli na migahawa ya vyakula vya asili na vya kisasa na maeneo ya burudani na kuvinjari.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Msaidizi huyo wa Idara ya Malikale, Wizara ya Maliasili na Utalii ametaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Mwalimu Nyerere katika kuhamasisha utunzaji wa maliasili na mazingira ikiwemo upandaji wa miti katika maeneo yote nchini na kutaka jamii ya sasa kuendelea kuenzi kwa vitendo maono hayo.
Mgeni rasmi katika Kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Khalid Matengo.
Mwalimu Nyerere aliyeng’atuka katika madaraka ya Urais mwaka 1985, alifariki Dunia Oktoba 14, 1999.