WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wakuu wa mikoa kuandaa mipango mahususi yenye malengo yanayopimika ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi na kaya nchini.
Maelekezo hayo yanakuja wakati taarifa ya Wizara ya Nishati ikionesha kuwa taasisi 2,703 kati ya 31,395 zinazolengwa nchini zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo wakati akihitimisha kikao kazi kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024–2034, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Hazina Square, jijini Dodoma.
Amesema kila mkoa unapaswa kutambua taasisi zinazohitaji kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi na kuweka malengo ya utekelezaji, hususan katika shule za bweni, vyuo na magereza.
“Natamani kuona kila mkoa ukiandaa mpango mahususi kufuatana na eneo lake,” amesema.
Ametoa mfano wa mkoa wenye shule 20 za bweni kuweka lengo la kuhamishia shule 10 kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji.
Aidha, ameelekeza wizara na wakuu wa mikoa kupitia hatua kwa hatua maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa mkakati huo Mei 8, 2024, ili kubaini yaliyotekelezwa na ambayo hayajakamilika.
Waziri Mkuu pia amewataka wakuu wa mikoa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu manufaa ya nishati safi ya kupikia, kushirikisha sekta binafsi na kuandaa mipango ya kupanda miti na kurejesha uoto katika maeneo yaliyoharibiwa.
Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanahusisha afya, mazingira, uchumi na uwezeshaji wa wanawake na vijana, hivyo mafanikio ya mkakati huo yanapaswa kupimwa kwa matokeo ya utekelezaji wake.