Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi yuko nchini Qatar katika mawindo ya kushiriki fursa za kiuchumi na uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar
CCM kimeitaja ziara hiyo ya kikazi pia ina madhumuni ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Zanzibar na Qatar.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyeitaja ziara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.
Mbeto alisema, pamoja na ziara hiyo kuwa sehemu ya juhudi za SMZ kujenga uchumi imara, itaimarisha diplomasia ya kiuchumi, kuvutia uwekezaji na kukuza ushirikiano wa kimkakati kwaajili ya msukumo wa maendeleo.
Alisema, zama hizi maendeleo ya Kijigitali, Sayansi na Teknolojia, si zama za Rais wa nchi kujifungia ikulu, bali ni nyakati za kutoka, kuhemea mawindo na na kunasa fursa za uwekezaji.
“Ziara ya Dkt. Mwinyi huko Doha nchini Qatar ni ya mawindo ya fursa za kiuchumi. Dunia ya leo imekuwa kijiji kidogo. Lazima utoke kwa ajili ya kushiriki mijadala inayohusu fursa na kuimarisha uhusiano,” alisema Mbeto.
Aidha, akiwa nchini humo, Rais Dkt. Mwinyi atatembelea kuona huduma za Afya katika kituo cha DOC Medical Center nchini Qatar ambacho ni kituo cha huduma za Afya kinachotoa huduma zake kupitia idara nane za kitaalamu katika sekta ya Afya.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi atashuhudia uendeshaji wa masuala kadhaa katika sekta ya Afya kupitia Wizara ya Afya ya nchi hiyo.
“Chama chetu kimempa baraka na mkono wa pongezi Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi za kuifanyia mageuzi Zanzibar. Unapohangaikia mawindo ya kujenga uchumi na uwekezaji lazima tuimarishe sekta ya Afya,” alieleza.
Katibu huyo Mwenezi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilio chini ya umoja wa Kitaifa, itafanya kila linalowezekana kuhakikisha Zanzibar inasongambele kimaendeleo.