Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema, wanatarajia kuingia katika masoko ya mitaji kwa ajili ya kutoa hatifungani, hatua inayolenga kuongeza vyanzo vya fedha na kuwezesha uwekezaji wa muda mrefu.
Dkt. Kiwia amesema hayo leo Oktoba 12, 2026 wakati wa kikao kazi kati ya bodi hiyo na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), ambapo hatua hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa kifedha wa bodi hiyo.
Alisema, mkakati huo umechochewa na uzoefu wa nchi nyingine ikiwemo Kenya, ambako taasisi za mikopo ya wanafunzi zimekuwa zikichunguza njia za kutumia masoko ya mitaji kuongeza fedha za kugharamia elimu ya juu na ya kati.
Aidha, alisisitiza kuwa, ushirikiano na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha, pamoja na kuimarisha urejeshaji wa mikopo kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kuwafikia vijana wengine wanaohitaji msaada.
Alisema, HESLB itaendelea kuwekeza katika maeneo mbalimbali yatakayoongeza uwezo wake wa kifedha, huku ikiimarisha mchango wake katika kutatua changamoto za taifa na kufanikisha malengo ya maendeleo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akifafanua umuhimu wa uwekezaji katika elimu, Dkt. Kiwia alisema, maendeleo ya uchumi yanategemea kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika rasilimali watu, akibainisha kuwa elimu na ujuzi ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija na ushindani wa taifa.
Dkt. Kiwia ameeleza kuwa, mtaji watu una mchango mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi, huku matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yakiongeza kasi ya maendeleo kwa kuboresha ufanisi katika sekta mbalimbali.
Alisema, mabadiliko ya teknolojia duniani yameifanya TEHAMA kuwa sehemu muhimu ya shughuli nyingi, kuanzia utawala hadi sekta za sayansi na tiba, hivyo kuhitaji taasisi za elimu na ufadhili kuendana na mahitaji hayo.
Dkt. Kiwia alisema, HESLB imeendelea kuimarisha mifumo yake ya TEHAMA na kuiunganisha na taasisi mbalimbali ili kurahisisha uchakataji wa taarifa, kuboresha utoaji wa huduma na kutambua wanafunzi wanaokidhi vigezo vya kupata mikopo na ruzuku.
Alisema, HESLB imepata ithibati ya viwango vya Kimataifa vya ISO, hatua inayolenga kuimarisha mifumo ya utendaji, uzingatiaji wa taratibu na kanuni pamoja na ubora wa huduma zinazotolewa.
“Tumejiimarisha na sasa tumetambuliwa kwa viwango vya Kimataifa ISO 9001:2015 katika usimamizi wa mifumo (Quality Management System) na hivyo kazi yetu ni kuhakikisha tunaendelea kusimamia viwango, hivyo kwa kuweka mbele huduma bora kwa mteja huku tukizingatia Sheria, Miongozo na Taratibu zinazotuongoza,” alisema Dkt. Kiwia.
Alisema, bodi hiyo imezindua Mpango Mkakati wa Sita (2026/2027 – 2030/2031) baada ya kuhitimisha Mpango Mkakati wa Tano (2021/2022 – 2025/2026) kwa asilimia 82 (82%); tulipata Hati safi kipindi chote, 80% ya hoja za hesabu (audit findings) ziifungwa, ambapo asilimia 72 ya waombaji mikopo wenye sifa walipangiwa mikopo.
“Dhima ya Mpango Mkakati mpya inajikita katika kuibadili HESLB kutoka taasisi inayotoa huduma hadi kuwa Mfuko wa kitaifa wa kugharamia wanafunzi ukiwa na fursa na wigo mpana zaidi katika kukidhi matarajio ya walengwa huku tukikumbatia tunu za ubunifu, weledi, kujituma, kujali zaidi wateja na usawa katika utoaji huduma,” alisema.
Aidha, HESLB imeendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kusimamia programu maalum za ufadhili. Mfano mwaka huu 2026/2027 imerasimisha ushirikiano na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufadhili wanafunzi wa programu za shahada za uzamili kupitia ufadhili wa Mwl. Julius K. Nyerere Memorial Masters’ Degree Scholarship na Ufadhili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa wanafunzi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ambao wanaenda kusoma masomo ya uhifadhi.
Kwa upande wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 alisema, wameanza kuitekeleza mwaka huu, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu inaingia katika lengo pana la kujenga mfumo bora na jumuishi wa elimu na mafunzo, pamoja na kuongeza fursa za Watanzania kupata elimu ya juu.
“Dira 2050 inalenga angalau asilimia 25 ya Watanzania wapate elimu ya juu ifikapo mwaka 2050 ikisisitiza kuongeza upatikanaji wa elimu ya juu na ufadhili, jambo ambalo Wizara ya Elimu inalitekeleza moja kwa moja, na hivyo basi napenda kusisitiza kwamba,” alisema Dkt. Kiwia.