NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni nyenzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza ufanisi wa taasisi na kupanua fursa za kiuchumi kupitia mifumo ya kidijitali.
Akizungumza Novemba 26, 2026, katika hafla ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Shirika la Posta Tanzania iliyofanyika katika ukumbi wa Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, Mkama amesema vifaa hivyo vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) vitaliwezesha Shirika la Posta Tanzania kuimarisha mifumo yake ya utoaji huduma kwa kufanya mageuzi ya kidijitali.
Amesema uwekezaji huo utaongeza uwezo wa Shirika hilo kuunganisha huduma mbalimbali hadi ngazi ya vijiji, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na Serikali Mtandao, pamoja na kuchochea biashara mtandao na kukuza uchumi wa maarifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Shirika la Posta Tanzania kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yanayotarajiwa, ikiwemo kuboresha uzoefu wa wateja, kuongeza thamani ya huduma na kuimarisha imani ya wananchi kwa shirika hilo.
Kupitia uwezeshaji huo, UCSAF inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kukuza matumizi ya TEHAMA na kupanua fursa za kidijitali nchini kwa kuwezesha taasisi kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
Hatua hiyo pia inaunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa kidijitali na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma zinazotolewa kupitia teknolojia.