Wizara ya Sanaa yaja na Tatu Kubwa za 2023

0
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi.

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kesho Ijumaa, Februari 03, 2023, inakwenda kuweka historia ya fungua mwaka kwa kufanya mambo makubwa matatu, “siku ya tarehe tatu mwaka 2023!”

Hayo yamesemwa leo katika mkutano na vyombo vya habari kwenye ofisi za BASATA Dar es Salam na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi.

Mosi, Wizara chini ya Mgeni Rasmi Waziri Mohammed Mchengerwa itapokea ripoti ya Kamati kuhusu vazi la Taifa. “Baada ya mijadala mingi sasa tunakwenda kukamilisha mchakato huu hivyo watatuletea maoni yao ya
mwisho,” alisema Dkt. Abbasi na kuongeza:

Pili, Wizara itapokea taarifa ya Kamati ya Mdundo wa Taifa “Hapa Tanzania inakwenda kuwa na utambulisho wake katika muziki wake na Kamati imeanda mpaka Kivunge cha Watozi (producers’ kit) ambacho ni Mwongozo kwa kila
mzalishaji.”

“Kesho kuna wasanii ambao wataimba jukwaani kwa kutumia mdundo huo mje kuwasikiliza,” aliongeza Dkt. Abbasi.

Tatu, kufuatia nia na dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka kuona sanaa inapiga hatua, katika tatu za tarehe tatu kesho itatolewa mikopo kwa wasanii inayokaribia kiasi cha Shilingi Bilioni 1 za Kitanzania.

“Zile zama za kusema wasanii hawana mitaji zimekwisha. Mhe Rais Samia ameridhia mikopo hii ili wasanii wajiendeleze, wajiajiri zaidi na waajiri wenzao wengi zaidi. Na hii ni awamu ya pili ya mikopo isiyo na riba ambapo Awamu nyingine zitafuata. Tukutane kesho ukumbi wa JNICC Dar es Salaam kuanzia saa nane mchana,” alisema Dkt. Abbasi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here