Waziri Silaa: Ni kazi ngumu, ila lazima tuifanye

0
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa.

Na Mwandishi Wetu

“Nimeridhishwa na utekelezaji wa maagizo na vipaumbele 12 vilivyotolewa na Rais Samia kwenye sekta hii ya ardhi, nawapongeza wakuu wa mikoa kwa kazi nzuri waliyoifanya, nawaomba waendelee na kazi hiyo ili tutimize matarajio ya Rais wetu,”

Ni kauli ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa kwenye mkutano wake na Wahariri na Waandishi wa habari kwa lengo la kuelezea mambo aliyoyafanya ndani ya siku 100 tangu alipoingia Wizarani hapo Septemba 4, 2023 na mipango wanayotarajia kuitekeleza kwa siku za usoni.

“Nimetembelea mikoa 25 ya Tanzania Bara kwa ajili ya kutatua changamoto za ardhi na kuangalia changamoto nyingine kupitia mpango wa Kliniki ya ardhi ambao umeleta matunda makubwa, kwani tumehudumia wananchi wengi kwa wakati mmoja na tumetatua migogoro mingi na wengine wameondoka na hati zao,” anasema Silaa.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, Kliniki hiyo ilianza Dodoma na baadaye Dar es Salaam, hivi sasa wamepanga ifanyike nchi nzima “ni kazi ngumu, ila lazima tuifanye. Ni lazima tutatue mambo ambayo yamezidi vimo waliopo mikoani, viongozi wa Wizara wakiwepo inasaidia kutatua matatizo kwa haraka.”

Waziri Silaa anasema, baada ya kuona matunda ya Kliniki hiyo kwa siku alizokaa Wizarani, wamepanga kuendeleza utaratibu huo kwa kuweka vituo (mahema) nchi nzima kwa ajili ya kuhudumia wananchi na kutatua changamoto zao za ardhi kwa haraka.

“Tunatarajia kuweka vituo vya wazi nchi nzima kwa ajili ya kutoa huduma, kwenye vituo hivyo kutakuwa na ‘One stop Centre’ ambapo wananchi watapata huduma zote za ardhi kwa pamoja na kutakuwa na watendaji walio chini ya Wizara ambao watakuwa wanatatua changamoto hapo hapo.”

Anasema, kwenye vituo hivyo wataweka kamera ambazo zitafuatilia utendaji ikiwemo muda ambao watendaji wa Wizara hiyo wanafika kwa ajili ya kuhudumia wananchi na jinsi wanavyoshughulikia changamoto zao bila vikwazo vyovyote.

Mbali na kuelezea kwa kirefu jinsi walivyotekeleza mpango wa Kliniki ya ardhi, Silaa anasema wanakuja na mpango mwingine unaoitwa KKK- Kupanga, Kupima na Kumilikisha; ambao lengo lake ni kuhakikisha hakuna ujenzi holela unaofanyika nchi nzima na amepiga marufuku kwenye maeneo ya Majiji na Manispaa kuuzwa bila kupimwa.

“Kwa kuanzia tutatumia utaratibu wa upimaji wa awali ambao hauna gharama na hili litafanyika kwenye maeneo ambayo yatakuwa bado hayajapelekewa fedha; tutawapa majukumu hayo Watendaji kwenye Mitaa, Vijiji na Vitongoji kupima maeneo yao, na baada ya wananchi kupimiwa na kujua gharama zinazohitajika, watalipa baadae,” anasema.

Aidha, kwenye mkutano huo Waziri Silaa katika kuhakikisha hakuna upotevu wa mapato ya Serikali kwenye sekta hiyo, alitangaza kwamba, kuanzia sasa fedha za mauzo ya viwanja yatasimamiwa na Wizara na yatafanyika kwa mfumo wa Kieletroniki ili kuhakikisha fedha hazipotei kwenye mikono ya halmashauri.

Pia, Waziri Silaa alipiga marufuku Wenyeviti wa Serikali za mitaa kuhusika na mauzo ya viwanja na kuchukua asilimia 10 ya fedha za mauzo hayo na badala yake zoezi hilo litasimamiwa na Maafisa wa ardhi.

“Ninatoa maelekezo kuanzia leo (Desemba 22, 2023) na ninaagiza watendaji wa Serikali za Mitaa waache mara moja kujihusisha na masuala ya ardhi. Waache kuchukua asilimia 10 za wananchi kwenye ardhi. Maelekezo yangu ni kwamba, kuanzia leo masuala yote yanayohusu ardhi yafanywe na maafisa wa ardhi waliopo kwenye eneo husika,” anasema.

Waziri Silaa anasema, kumekuwa na malalamiko mengi ya wananchi katika ununuzi wa ardhi na kwamba viongozi hao wamekuwa wakihusishwa kwenye malalamiko kwa kuchukua asilimia 10 za wananchi wakati wa mauziano. “Watendaji wa Serikali za mitaa na vijiji hawana Mamlaka ya kisheria kuchukua asilimia 10.”

Mbali na hilo, Waziri Silaa alifafanua kuhusu suala la uuzaji na ununuzi wa maeneo makubwa vijijini kwa ajili ya uwekezaji, wasinunue kwa Wenyeviti, badala yake badala yake wafuate utaratibu wa kuomba, ambapo halmashauri ya kijiji itapokea maombi na kuitisha mkutano mkuu wa kijiji na maeneo hayo ni bure.

Anasema, anachotakiwa kufanya mwekezaji au mwananchi anayetaka kununua maeneo hayo ni kusaidia mahitaji ya jamii husika kwa chochote wanachohitaji kwa mfano darasa au huduma za kijamii watakazopendekeza.

Jambo jingine ambalo alitangaza kwenye mkutano huo, ni kuanza kwa zoezi la kukagua maeneo ya wazi ambayo yalitengwa kwa ajili ya shughuli za kijamii ambayo mengine yamekodishwa bila kufuata utaratibu na yanatumika kibiashara. “kuanzia sasa maeneo hayo yatakuwa chini ya Wizara,”

Waziri Silaa anasema, tangu alipoingia Wizarani amefuatilia utekelezaji wa zoezi la urasimishaji ambalo liltarajiwa kuisha mwaka 2023, lakini limekumbwa na changamoto nyingi na limekwama, hivyo linasogezwa mbele na Serikali itaweka nguvu kubwa ili kulikwamua.

Anasema, zoezi hilo litaendelea kwa kutumia kampuni zenye uadilifu, kwani kukwama kwake pamoja na sababu nyingine, limekwamishwa na baadhi ya kampuni ambazo zilikosa uadilifu ambapo anasema watachukua hatua kwa kampuni zinazokiuka taratibu ikiwemo kufutwa.

“Serikali imepanga kutoa fedha kwa ajili ya kuliendeleza kwa kuanzia Dar es Salaam, na kama kwenye Kilimo kuna BBT ( Building a Better Tomorrow) nasisi tunataka tuwe na BBT yetu, vijana wenye taaluma ya ardhi kwenye mitaa yao wapate kazi ya kukwamua zoezi hili ambalo litafanyika kwa miezi mitatu na baadae watakuwa Mawakala na watalipwa kwa kazi hiyo,” anasema Waziri Silaa.

Anasema, sambamba na kukwamua zoezi hilo la urasimishaji, kwa mwaka huu wa 2024 wataweka nguvu kubwa kwenye maeneo yanayotajwa kuwa yamekithiri kwa migogoro ya ardhi ambayo imesababishwa na uuzaji holela unaofanywa na wavamizi. “Nawasihi wananchi waache kununua ardhi kienyeji hususani kutoka kwa wavamizi, wajue kwamba wavamizi ni wahalifu kama wahalifu wengine.”

Waziri Silaa anasema, katika kuhakikisha wanashughulikia kwa haraka changamoto za ardhi, mbali na kuanzisha ‘App’ inayoitwa ‘ardhi kiganjani,’ wameanzisha Mikoa mipya ya ardhi ili kila mwananchi apate huduma alipo, ambapo hilo litasaidia kupunguza gharama za muhusika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma, sambamba na kuokoa muda na kupunguza msongamano kwenye ofisi za ardhi.

“Tukifanya haya, tutakuwa tumefanya maboresho makubwa na kutumiza malengo ya Rais Samia, nawasihi watendaji wote kutumiza wajibu wao na kufanya kazi zao weledi na kutoa lugha nzuri kwa wananchi,” anasema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here