Waziri Mchengerwa ashuhudia utiaji saini mikataba ya miradi ya Bilioni 40 Arusha

0

Na John Mapepele

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ameweka jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la jiji la Arusha na kushuhudia utiaji wa saini mikataba ya mradi wa Stendi Kuu ya Mkoa wa Arusha, Soko la Mrombo na Bustani ya Mapumziko ya Themi vyote vikiwa thamani ya takriban Shilingi Bilioni 40.

Akikagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya jiji la Arusha lenye sakafu tisa ambalo litakapokamilika litagharimu Bilioni 9.8 amemtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati ili kuondokana na adha ya sasa ya watumishi kufanyia kazi kutokea kwenye ofisi zilizo katika maeneo tofauti hali inayochelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kutoa fedha za ujenzi wa jengo hili kwa kuwa baada ya kukamilika litakuwa mkombozi kwa watumishi,” alifafanua Mchengerwa.

Aidha, ameuelekeza uongozi wa Mkoa na Jiji la Arusha kuhakikisha jengo hilo linakamilika mara moja na endapo kutakuwa na mkwamo wowote wachukue hatua.

Amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kwa kukwamua mgogoro wa kushindwa kukamilika kwa jengo hilo kwa zaidi ya miaka 5 kutokana na masuala ya kisiasa.

Mradi huo umefikia asilimia 62 na unafanywa na mkandarasi mzawa M/S Tribe Construction Ltd na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Akihutubia wananchi baada ya kushuhudia utiaji wa saini mikataba ya mradi wa ujenzi wa Stendi Kuu ya Mkoa wa Arusha na Soko la Mrombo na Bustani ya Mapumziko ya Themi, Mchengerwa amewataka viongozi kufanya maaamuzi magumu katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.

Miradi hiyo ambayo inatarajia kugharimu Bilioni 30.6 itakapokamilika ametaka iwe inaweza kujiendesha yenyewe na kutoa faida.

Pia, amesisitiza kuilinda, na kufanya usafi ili iwezekudumu kwa muda mrefu pindi itakapokamilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here