Wasoweto wanavyokumbuka wema wa Mazimbu

0
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mohamed Mchengerwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Afrika ya Kusini Nocawe Mafu, wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini, hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Na Saleh Saleh

HISTORIA ya maisha ya wakimbizi wa Afrika Kusini nchini Tanzania inabaki na kumbukumbu ya ukarimu mkubwa wa Watanzania. Mwanzoni, kulikuwa na tabu ya mawasiliano ya lugha kati ya wenyeji na wageni wao.

Kama inavyofahamika Tanzania imepata tunu ya lugha moja ya kuliunganisha Taifa; Kiswahili, lakini wakati huo huo, Watanzania wengi wamepata ugumu wa lugha ya Kiingereza.

Kwa ugumu huu, wakimbizi walikuwa wakijaribu kutafuta angalau watu waliodokoa-dokoa Kiingereza. Waliishi katika Kambi yao Mazimbu, lakini pia walikuwa na makazi katika majumba ya kupanga Mjini. Kwa kufanya hivyo, wakaweza kuchanganyika vizuri zaidi kijamii.

Yumkini, baadhi yao waliweza ‘kukimanya’ Kiswahili walichokisikia kwa wenyeji. Licha ya umasikini uliokuwepo Tanzania, bado uungwana wa wenyeji ukafunika aibu ya kukosa cha kuwapa wageni.

Ukarimu wa kuwakaribisha wageni wao majumbani na kuwakirimu kidogo walichokuwa nacho ndio ulioacha athari kubwa nyoyoni mwa wageni hao. Kama yalivyo makabila mengi ya Tanzania, Waluguru ambao waliunda jamii kubwa ya wenyeji wa Wakimbizi wa Afrika Kusini Mkoani Morogoro, wana maisha ya uungwana.

Huenda zama zinabadili mila na desturi, lakini kama mtu angerudi miaka ayarejee maisha yaliyokuwa majumbani na hasa katika maeneo ya wenyeji hususan milimani ambako wazee wa Kiluguru walifanya makazi yao, angekuta utajiri mkubwa au labda tuite hazina kubwa ya uungwana na ukarimu, kuanzia salamu, kuja makaribisho ya chakula hadi mizigo ya zawadi za mgeni na hatua za kumsindikiza au kumtoa mgeni.

Wakati ule majumba yalikaribisha mgeni yeyote yule bila kujali kama ni ndugu au jamaa, mpita njia au jirani. Ndizo enzi za ndugu zetu Waislamu kufuturu pamoja kwenye vibaraza vya nyumba zao Mwezi wa Ramadhani. Ukarimu ulikuwa mwingi mno.

Lakini, juu ya ukarimu, wakimbizi pia walifaidi utulivu. Ilifika mahala wao ndio waliokuwa wakileta fujo mjini pale walipolewa. Mpaka wenyeji wakawa wanasema, “hawa ni watu wa fujo kwa sababu ya mapambano ya nchini kwao.” Wenyeji walibaki na uungwana. Si vijana, si wazee. Wakimbizi walipata marafiki kila sehemu licha ya tofauti ya lugha.

Walipata marafiki masokoni, majumbani, mitaani. Walioneshwa kila aina ya upendo. Walipita mitaani kwa miguu, magari na mapikipiki yao. Walisalimiwa kwa majina ya “Wasoweto”, “wakunjan” na “Freedom fighters”.

Mluguru hana shari, ni mwepesi kujenga udugu, ni mwepesi kumwita mgeni aliyeishi naye muda mrefu, ‘mjomba wake’. Katika hili, hata waarabu waliopandisha na kuishi Mkuyuni waliitwa ‘wajomba’. Mjomba ana nguvu sana kwa Waluguru. Waarabu walipopata wake wa Kiluguru ndio kabisa! Mluguru, mtu wa amani, hataki shari, Wangoni walipofika maeneo yao walikubali hata kuyaita maeneo yao kwa majina ya Kingoni.

Ukipandisha Mlima Magadu (fold mountain), pale unapoishi mlima huo, kuelekea njia ya kushoto, huko kunaitwa Ruvuma. Ruvuma ya kina Komba, Njozi, Simba, Mbuyu au Mapunda kuletwa kwa waluguru wapi na wapi? Nadhani ilikuwa kuogopa shari za Wangoni ‘wavamizi’!!

Marehemu Mzee Salum Lukwele alitokea Afrika Kusini. Yeye na wazulu wenzie waliondoka nchini mwao kufuatia vita maarufu vya mparaganyiko wa wazulu, ‘Mfekane’, wakasafiri safari ndefu hadi mahali walipokuja kupaita Ruvuma au Songea.

Mzee Lukwele anayesemekana kuzaliwa miaka ya 1860 hakuishia hapo, aliendelea na safari hadi Iringa, mpaka katikati ya mji wa Morogoro, akaweka makazi, akajikatia eneo kubwa lilipo soko kuu hii leo hadi shule ya msingi Kikundi, wakati huo pori tupu lisilo na mwenyewe, akajimilikisha. Ukarimu wa waluguru, wakampa na mke wa Kiluguru, mama Bwakila! Bibi Mlali! Nimefahamishwa Mzee Lukwele alikufa mwaka 1972.

Lakini, usemi wa mgeni njoo, mwenyeji apone nao ulidhihirisha ukweli wake. Miaka ya 1980 ningali mtoto kabisa, inaripotiwa kushuhudia uhaba mkubwa wa bidhaa ikiwa ni pamoja na nguo na viatu.

Wageni wakawafaa wenyeji wao kwa mitumba (vigozi) na viatu (raba mtoni). Vijana wa zamani, watu wazima sana kwangu, wa Soko Kuu Morogoro, akina Seti, Aude, Twaha Bitota, Bene, Hija, Shaaban ‘Mkimbizi’ na wengine naamini wanakumbuka zama hizo ambazo mimi sipo au mchanga, walivyokuwa wakipata nguo na viatu kutoka Mazimbu, Solomon Mahalangu, ambako sasa ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Hivyo ndivyo nilivyojaribu kuwakumbuka Wasoweto pale Watanzania wenzangu waliponiambia kuwa wanaishi Afrika Kusini vizuri, na wanapendwa na wenyeji. Dini inatufundisha kuwa nyoyo huwa na kawaida ya kuwapenda wanaozitendea wema.

Watu wa Morogoro, si lazima wawe Waluguru, wanapendwa na Wasoweto kwa namna walivyoishi nao kwa wema. Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki! Wema waliotendewa Wasoweto umeganda nyoyoni mwao kiasi kwamba kila Mtanzania anajivunia mtaji wa wema huo anapoingia Afrika Kusini.

Wale wanaowajua vizuri Waluguru wanaweza kuukubali ukweli mmoja kuwa Mluguru ni mkarimu kwa wageni japo ni mwoga wa kutoka Mkoani kwao kwenda kuishi ugenini au kula kwa mtu asiyemjua.

Ndiyo maana hukuti Waluguru wakiwa wamesambaa mikoa mingi ukiacha ukanda wote wa Pwani ambako wanabadilika majina kama Wakutu, wakwere kwa upande mmoja, wakami hadi Dar es Salaam ambako wamegeuka kuwa wazaramo (Waliozaramia, yaani waliolowea au kuselelea).

Ni mmoja-mmoja sana katika Mikoa mingine ya bara, kusini na kaskazini. Na kwa kuwa hawana hisia kali za ukabila, ndio kabisa, inakuwa vigumu hata kuiona nguvu yao ugenini.

Kinyume chake, Waluguru huweza hata kuogopana ugenini! Hawathamini sana udugu wa kikabila! Mwanasiasa wa zamani Zuberi Mtemvu, Mluguru, alipata kusema, “Waluguru ni wagumu sana!

Ndio waliomzika akiwa hai kwa kubeba jeneza tupu na kulipeleka makaburini, enzi hizo Msamvu. Yalikuwa ni mazishi ya kisiasa ya kumzika Mluguru mwenzao Mtemvu na chama chake ndani ya Mkoa wake! Mluguru ni “msusa” sana, yaani mtu mwenye kuzira au “kafea” kwa lugha yake ya Kiluguru! Akisusa, kasusa! Ukisikia ‘kafea’, maana yake mluguru hapo kakususia (kazira), pengine kuna jambo limemuudhi.

Ukimkorofisha Mluguru, anaondoka, hutamuona tena nyumbani kwako, hata kama alikuwa jamaa yako wa karibu sana! Marehemu mzee wangu, alipata kunihadithia kuwa aliyekuwa mlezi wa Bendi ya Moro Jazz ambaye pia alikuwa mfanyakazi mwenzake, Railway, idara ya PWI, marehemu mzee Seif Ally alikuwa akimtania ‘Kefeaga Ugali’.

Yaani mzee alikuwa msusa (mtu mwenye kuzira) sana, ukimkorofisha anakuwakia, ikiwezekana mnazipiga au anakupiga kisha mnaagana, hutamuona tena kukufurahia!

Nikiwa kwenye moja ya ziara zangu nchini Afrika Kusini niliwakuta vijana wa Kiluguru, na wa Morogoro hata kama si Waluguru. Lakini sikuona dalili ya Waluguru wale kususa na kuwa na mawazo ya kurudi kwao kwani wenyeji wao hawajawaudhi.

Malipo ya hisani ni hisani. Yaelekea wenyeji wamelipa hisani. Nimekuta maisha ya kuchanganyika na wenyeji. Wameoa wake wa Kizulu na kuzaa nao japo wanawake wa Kizulu wanapenda sana watoto na hawako tayari watoto wao waondoke Afrika Kusini.

Kule Soweto, kuna ishara fulani za kihistoria kwamba mchanganyiko wa makabila ya Afrika Kusini una asili ya makabila ya Tanzania. Kaka yangu mmoja aliwahi kunipa misamiati ya Kiluguru ambayo inafanana na ile ya Kizulu, moja ya makabila ya Afrika Kusini.

Wazulu wanamwita “Mkubwa” kwa jina la “Nkulu”, Waluguru nao wanamwita hivyo hivyo “Mkulu”. Mlurugu husema, “Mwanamkulu” yaani mtoto mkubwa (kuzaliwa).

Wazulu wanamwita Mungu kwa jina la “Mulungu”, Waluguru nao humwita Mungu “Mlungu”. Utawasikia wakisema, ‘Mlungu chibidu’, tafsiri yake Mungu hupindua chini-juu, juu-chini! Tafsiri yake, wa juu anaweza kushuka chini, na wa chini kupanda juu. Na kwa tafsiri ya kiistilahi, ‘Mungu hupindua hila.

Wengine wamesema hata Rais wa Pili Mweusi wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, jina lake limebadilika tu baada ya kupitia mabadiliko ya vizazi lakini usahihi ni Tabu Mbiki. “Mbiki” au “Wambiki” ni moja ya koo za Waluguru.

Sijui labda Wasoweto walijihisi kama wako nyumbani Morogoro kwa damu ya asili, huenda labda mababu zao walitokea kwanye Milima ya uluguru na kusambaa katika Mataifa mengine ikiwemo Afrika Kusini. Au huenda mababu zao wa mto Zambezi ndio waliokuja kwenye milima ya uluguru. Nilichokiona Afrika Kusini kwa siku saba nilizokaa pale ni kwamba nchi sasa imetulia. Amani imetawala.

Mtu yuko huru kuvinjari hata maeneo ya Ikulu bila tatizo. Nimeridhika kuwa wenzetu walioamua kwenda kuishi huko wako salama. Na watakuwa salama zaidi kama wataishi kwa kuepuka shari, mambo ya fujo, shughuli zisizofaa na kadhalika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here