Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini kuwanufaisha wasanii wa Tanzania

0
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Afrika ya Kusini Nocawe Mafu (kushoto), na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Said Yakubu (wa kwanza kulia) wakicheza ngoma mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari.

Na Mwandishi Wetu

MOJA ya sababu za Afrika Kusini kufanya shughuli mbalimbali kwa ajili ya kuadhimisha Msimu wa Utamaduni wa nchi hiyo hapa nchini, ni kutokana na uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Sababu nyingine ni utekelezaji wa mkataba uliosainiwa mwaka 2011 kati ya nchi hizi mbili ambazo zimedhamiria kukuza ushirikiano katika Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Miongoni mwa shughuli ambazo zitafanyika nchini kwa wiki nzima, ni pamoja na Tamasha kubwa ambalo linataraji kufanyika Zanzibar, Maonyesho ya mavazi na Filamu kutoka nchini humo, Semina pamoja na utalii wa Maeneo mbalimbali yenye historia ya kumbukumbu ya nchi ya Afrika Kusini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Afrika ya Kusini Nocawe Mafu, alisema Tamasha hilo limelenga kukuza uhusiano wa Tanzania na nchi yao, kudumisha na kukuza utamaduni na kubadilishana uzoefu.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Afrika ya Kusini Nocawe Mafu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

“Hapa ni kama nyumbani kwetu, Afrika Kusini na Tanzania ina uhusiano wa kihistoria tokea zamani, Mwalimu Julius nyerere alipigana kwa hali na mali kuhakikisha Afrika Kusini inapata uhuru wake,” alisema Mafu.

Alisema, licha ya burudani zitakazotolewa kwenye msimu wa tamasha hilo, kutakuwa na Semina ya biashara ya kazi za Sanaa ikiwemo muziki, maonyesho ya Filamu, maonesho ya picha za kuchora kutoka Afrika ya Kusini.

Aidha, Mafu alisema wanatarajia wasanii wakubwa kutoka Afrika Kusini watatumbuiza kwenye jukwaa la Tamasha ambalo litafanyika Novemba 27, Visiwani Zanzibar.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Said Yakubu, mbali na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli mbalimbali ambazo zitaendana na Tamasha hilo, alisema litasaidia kukuza diplomasia, ni fursa kwa wasanii wa Tanzania kuonyesha na kuuza kazi zao za mikono.

“Tamasha hili litafungua madirisha ya uwekezaji wa sekta ya utamaduni na michezo. November 19 watakuwa Morogoro ambapo kutakuwa na Kongamano kuhusu mchango wa Tanzania kwenye uhuru wa Afrika ya Kusini na Novemba 27 itakuwa ni kilele cha Tamasha hili na yatafanyika Zanzibar,” alisema Yakubu.

Aidha, Yakubu aliwataka watanzania kujitokeza kuangalia Filamu kutoka Afrika Kusini ambazo zitaonyeshwa Makumbusho ya Taifa “Pamoja na shughuli zote hizo, kutakuwa na maonyesho ya filamu za Afrika Kusini, tujitokeze kuangalia filamu hizo, wengi wanaijua filamu ya Sarafina tu, lakini zipo nyingi.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here