‘Wananchi waachwe waamue hatma yao’

0
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Abdulrahman Kinana, akizungumza baada ya kuzindua Shina la Wakereketwa wa CCM Majengo Sokoni.(Picha na Fahadi Siraji).

Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana ameshauri kuwa umefika wakati mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ya wananchi lazima yaamriwe na yatokane na wananchi wenyewe.

Alisema, japokuwa wapo wawakilishi wa wananchi wakiwemo wabunge, madiwani au halmashauri, lakini hawana uwezo wa kubadilisha hali iliyopo, hivyo ni muhimu wananchi wakapata nguvu zaidi kushiriki kuamua mambo ya muhimu kwao.

Kinana ametoa ushauri huo alipozungumza na wanachama wa CCM na wanachi wa Jimbo la Mtama Mkoani Lindi baada ya kuzindua Shina la Chama, Majengo Sokoni.

Akielezea zaidi kuhusu umuhimu wa wananchi kushirikishwa katika kuamua maendeleo alitoa mfano kuna wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM akiwa na Nape Nnauye walienda wilayani Ngorongoro wakafanya mkutano mkubwa.

“Tulipokuwa pale ukitazama pale kwa mimi ungeniuliza ningesema wale wananchi wanahitaji maji lakini tulipouliza wenyeji wakasema tatizo lao si maji bali ni mtandao wa simu.

“Unaweza ukaona wewe unakwenda mahali ukifikiri shida ya watu ni shule, ni maji kumbe shida yao ni jambo jingine kabisa ndio ni lazima tuwashirikishe wananchi.

“Katika kuamua mambo yanayohusu maisha yao, tusichukue amana ya kuwafikiria , tusichukue mamlaka ya kuwaamria.Ni vizuri tukae na wananchi tuzungumze nao ili watuambie kitu gani wanakihitaji kwa wakati gani na kwasababu gani,” alisema Kinana.

Alifafanua kuwa, ukiwaambia wananchi leo wajitolee kujenga barabara wanaweza kukwambia wao wanataka shule kwanza huku akieleza katika mkutano huo imezungumzwa kuhusu kupeleka madaraka kwa wananchi.

“Kwahiyo uundwaji wa vijiji, vitongoji, ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi. Ukiangalia nchi yetu ilivyokaa wakati wa Uhuru katika miaka ya 1960 na 1970 tulikuwa na mikoa tisa leo tunamikoa zaidi ya 30.Tulikuwa na wilaya 50 leo tunakaribia wilaya 200, tulikuwa na kata chache leo tunakata nyingi

“Kwa hiyo Mwenyekiti na Mbunge nimewasikia kuhusu madaraka kwa wananchi.Tupeleke uamuzi kwa wananchi uhwe na tija lazima kuwe na taasisi inayosaidia wananchi kufanya maamuzi hayo.

“Nawashukuru umetoa wazo hilo na nitalichukua kwenda kushauriana na wenzangu. Nitatoa maoni na ushauri. Nadhani kuna jambo linabidi vile vile tulijadili, tunapenda sana kukabidhi maamuzi ya muundo wa nchi yetu kwenye kikundi kidogo cha watalaamu.

“Ndio maana wakati mwingine unaweza ukawa na mantinki na ukawa na hoja ya kuwa na kijiji au kuwa na mtaa au kuwa na serikali fulani mahala fulani lakini kwasababu wanaoamua wako mbinguni, wako kule juu lazima maombi yapelekwe mbinguni kwa wakubwa.”

Alisisitiza, hiyo inamfanya afikiri mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ya wananchi lazima yaamriwe na wananchi na lazima yatokane na wananchi.Wabunge wanaona jambo jema , halmashauri kuu ya wilaya inaona jambo jema , madiwani wanaona jambo nzuri, lakini hawana uamuzi nalo.”

Hivyo, alisema umefika wakati kama kweli madaraka ni ya wananchi, basi wawakilishi wa wananchi wawakilishe wananchi, wawe na kauli katika kuamua juu ya mambo yanayohusu wananchi tusibaki na mfumo na utaratibu wa zamani.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Mtama ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alikiomba Chama kutazama upya uamuzi wa kutanua maeneo ya kiutawala hususan kwa ngazi ya vijiji na vitongoni.

Kwa mujibu wa Nape, baadhi ya maeneo kuna hali ngumu kuwahudumia wananchi kutokana na ukubwa wa maeneo na wingi wa wananchi hivyo ni vyema kuridhia kuyaongezea maeneo ya kiutawala.

Nape alisema, kutokana na wingi huo na umuhimu wa kuwahudumia wananchi, alikiomba Chama kiridhie kuanzishwa kwa vijiji na vitongoni vipya kusaidia kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefikisha huduma mbalimbali za muhimu katika Jimbo hilo.

Miongoni mwa huduma hizo ni maji safi na salama, ujenzi wa vituko vya afya na zahanati, kufungua mawasiliano ya simu za mkononi na kusambazia umeme.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here