Na Emmaculate Mwalwego, OUT
NIMEKUWA nikifuatilia mahubiri ya baadhi ya wahubiri wa dini ya Kikristo kutoka katika madhabau ya madhehebu mbalimbali. Kuibuka kwa manabii na mitume kutoka katika madhehebu hayo limekuwa ni jambo la kawaida.
Hilo linatokana na kuwepo kwa uhuru mpana wa kuaabudu siyo tu nchini Tanzania, bali barani Afrika kwa ujumla.
Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba, uhuru wa kuabudu barani Afrika na katika maeneo mengi kote duniani umekuja na mambo mengi. Wote wanaojiita mnabii na mitume, ni watu wenye ukwasi wa kutisha.
Lakini, kuna mengine mengi ambayo yamekosa kuthibitishwa na yeyote kwa sababu kila mtu ana haki ya kuamini atakacho au kuabudu kwa njia anayoiamini.
Nakumbuka wakati fulani, nabii mmoja aliwahi kuzuia maiti ya mtu isizikwe kwa imani kwamba, angeifufua baada ya maombi ya siku tatu. Nabii yule alishindwa kumfufua mtu huyo na kujikuta akiishia mikononi mwa polisi.
Kuchomwa moto kwa baadhi ya wafuasi wa Kibwetere huko nchini Uganda ni uthibitisho mwingine wa kuibuka kwa manabii hawa wa uongo.
Hata hivyo, bara la Afrika katika miaka ya hivi karibuni limekuwa muathiriwa wa waumini wake kutumiwa vibaya na baadhi ya wahubiri ambao wamejijengea sifa na utajiri kupitia mbinu, vitendo na hata imani za kustaajabisha.
Matukio vya wahubiri kuwatumia vibaya waumini wao vimeendelea kukithiri na vingi hata haviangaziwi katika vyombo vya habari. Hata hivyo, baadhi ya vitendo na ‘miujiuza’ wanayodai kufanya baadhi ya wahubiri hao ambavyo vimeweza kunakiliwa na vimewashangaza watu wengi huku cha kusikitisha zaidi, waumini wanaopata matatizo wakiwa kwenye makanisa ya wahubiri hao, hawapati msaada wowote.
Taarifa kwamba, Mhubiri mmoja wa Afrika Kusini alikuwa akiwapulizia usoni dawa ya kuua wadudu waumini wake kama njia ya kuwaponya uliwashtua wengi. Lakini, siye pekee Afrika aliyefanya kitendo kama hicho kwa kuhusisha hatua yake hiyo na imani ama uhuru wa kuabudu.
Kwa sasa, sio jambo la kushangaza kukuta miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Dodoma, Mwanza ikiwa imetapakaa mabango yanayoonesha au kutangaza makanisa yenye majina mapya kabisa.
Kibaya zaidi, baadhi ya majina ya makanisa hayo, hutishia mwisho wa dunia, kuahidi uponyaji na hapo hapo wokovu kwa kila hali ama magonjwa.
Makanisa hayo kwa kawaida huongozwa na wachungaji wenye haiba, ambao huanzisha makanisa yao badala ya kujiunga na taasisi zilizowekwa, na mara nyingi hudai kuwa na nguvu za miujiza.
Humo huuzwa vitambaa, maji, na vitu vingine vya kushangaza ambavyo waamini uhubiriwa kuwa vinaweza kubadili jambo lolote katika maisha yao.
Walakini, miujiza hiyo imeambatanishwa na uwezo wa waamini ‘kupanda mbegu’ au kutoa pesa kwa wahubiri hao. Hivi ni baadhi ya vitendo vilivyowashangaza wengi, ambavyo vilifanywa na vinazidi kutekelezwa na baadhi ya wahubiri na manabii hao. Kibaya zaidi hao wanaolazimishwa kupanda mbegu baadhi yao ni watu dhalili na hohehahe kwa ufukara usiomithilika.
Mfano mzuri huko nchini Congo, ‘Nabii’ maarufu, Domique Khonde ana mamilioni ya wafuasi kote duniani na wengi wa waumini wake wanaamini kwamba sharubati (juisi) yake inayouzwa kanisani inaweza kutibu kila aina ya maradhi yakiwemo virusi vya UKIMWI, Saratani na hata kuwafufua watoto waliofariki dunia.
Sharubati hiyo hutengenezwa kwa kutumia mafuta ya Petrol, maji ya ndimu na viungo vingine. Khonde aliripotiwa mapema mwezi huu katika makala ya Shirika la Habari la Ujerumani (DW) yaliyozua gumzo mitandaoni kuhusu ukweli wa tiba ya ‘miujiuza’ ya sharubati hiyo ambayo chupa moja ya mililita 300 inauzwa kwa Euro Milioni 14.
Mikutano yake ya kuhubiri huwavutia maelfu ya watu. Katika makala hiyo, ilionyeshwa jinsi watu walivyofurika kwenye uwanja mkubwa ili kumsikiliza.
Inadaiwa amefaulu kutengeneza mamilioni ya pesa kutokana na juisi yake hiyo na hata serikali ya DRC imemruhusu kuendelea na shughuli zake kwa kigezo kile kile kile cha kuendeleza uhuru wa kuabudu.
Miongoni mwa wafuasi wake ni viongozi wa zamani wa nchi hiyo na familia zao na injili amekuwa akidai kuwa ya mafanikio. Huko Afrika Kusini, Mchungaji Lesego Daniel anaongoza Rabboni Ministries katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria. Aliwaamuru waumini wa kanisa lake kunywa petroli, akidai kwamba alikuwa ameibadilisha kuwa juisi ya mananasi.
Video iliyowekwa mtandaoni ilimuonesha muumini mmoja akimimina petroli kwenye sufuria na kisha kuiwasha ili kudhibitisha kuwa ilikuwa ikishika moto, kisha anainywa na kusema ‘yuko sawa na hana athari zozote,’ wakati mhubiri huyo anapomuuliza kuhusu petroli hiyo.
Mwanamke anakimbizwa katika jukwaa na kupewa mafuta hayo kuyanywa kisha anasema ‘yana utamu’ hatua inayowafanya wanawake wengi kukimbilia mafuta hayo na kuyabugia.
Penuel Mnguni aliyewahi kuongoza Kanisa la ‘End Times Disciples Ministries’ tangu mwaka wa 2014. Awali alikuwa mfuasi wa Lesego Daniel, mhubiri wa Afrika Kusini aliyewapulizia waumini wake dawa ya kuua wadudu.
Mwaka aliofungua kanisa lake picha za waumini wakila nyasi na maua kufuatia agizo lake zilisambaa katika facebook na kwenye tovuti ya kanisa hilo. Picha nyingine zilimuonyesha akiwalisha wafuasi wake mawe baada ya kudai kwamba, alikuwa ameyageuza yawe mikate.
Alipewa jina la ‘mhubiri wa nyoka’ baada ya kutolewa kwa picha zake akiwalisha waumini nyoka na panya akidai kwamba alikuwa amevigeuza kuwa ‘Chokoleti’. Wenyeji baadaye walimfukuza kutoka mji wa Soshanguvea, Kaskazini mwa Pretoria ambako kanisa lake lilikuwepo.
Nchini Ghana, Askofu Daniel Obinim wa ‘International Godsway Ministries’ ana ibada za kipekee na ghali ambazo yeye hufanya kushughulikia matatizo mbalimbali ya waumini wake.
Katika mojawapo ya tukio linalojulikana kumuhusu, alionekana akiwa amesimama juu ya tumbo la mwanamke ambaye inaripotiwa alikuwa mjamzito ili kumtoa pepo kutokana na kuingiwa na pepo wachafu.
Katika tukio jingine alionekana akimshika mwanaume sehemu zake za siri kwa madai kwamba alikuwa akimtibu tatizo la ‘ukosefu wa nguvu za kiume’
Wanaume walisimama kwa foleni na kuinua mikono yao ili kungoja kushikwa sehemu zao hizo kwa zamu na mhubiri huyo. Mtindo wake wa kuwaombea waumini wakati mmoja uliifanya mahakama moja mjini Accra kuripotiwa kutoa waranti ya kukamatwa kwake pamoja na washirika wake wawili baada ya kuonekana akiwaadhibu kwa viboko vijana wawili waliokuwa wamefika kanisani mwake.
Tukisoma Marko 13: 21-25 inasema: “Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki; Kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule.
Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele. Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake. na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika.”
Haya na mengine mengi, yanadhihirisha wazi kwamba, tumeingia kipindi ambacho makristo wa uongo wamejitokeza na wanadanganya wengi. Ni wakati wa kujihadhari na kuwa nao macho.