Na Shamimu Nyaki
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema, Wizara anayoiongoza itaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa Kituo Cha Michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya mkoani Mwanza kama ilivyopanga.
Dkt. Ndumbaro alisema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni aliyehoji kwanini Wizara inahamisha ujenzi wa Kituo cha Michezo Malya kutoka Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza kwenda Ilemela wakati imeshasaini Mkataba wa utekelezaji.
“Tutaendelea na ujenzi wa Kituo Cha Michezo Malya kama ambavyo tumepanga, hatujahamisha ujenzi huo kwenda sehemu nyingine, lakini pia tutaendelea na ujenzi wa Kituo cha Michezo katika Wilaya ya Ilemela na maeneo mengine kwa kuwa azma ya Serikali ni kuwa na vituo pamoja na akademia za michezo katika maeneo mbalimbali nchini” alisisitiza Ndumbaro.