Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amesema, Wizara yake itahakikisha kero zote za migogoro ya ardhi zinakwisha katika Jijini la Dodoma ikiwa ni hatua muhimu ya utekelezaji rasmi maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na wananchi waliofika katika Kliniki ya Ardhi, Waziri Silaa alisema, lengo la kuweka kambi katika ofisi za Kamshina wa Ardhi wa Jiji la Dodoma ni kuhakikisha wanawahudumia wananchi ipasavyo.
Waziri Silaa amewaambia wananchi waliofika kupata huduma katika Kliniki hiyo kuwa, atakuwa akifanya nao mazungumzo kila baada ya kumaliza ratiba ya bunge ili kujionea mwenyewe kero zinazowakabili wananchi hao.
Mmoja wa wananchi hao, Foime Yohana ametoa dukuduku lake kwa Waziri Silaa baada ya kuwa na kero ya muda mrefu ya kuvamiwa na kuchukuliwa eneo lake nakuomba Waziri huyo kusaidia ili aweze kupata haki yake.
Akiongea na vyombo vya habari wakati wa zoezi la kuhudumia wananchi likiendelea Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Eng. Anthony Sanga alisema, Kliniki ya Ardhi inayoendelea kwa wiki mbili Jijini Dodoma, itakuwa mwarobaini wa changamoto nyingi za ardhi zinazowakabili wananchi wengi wa Jiji hilo.
Sanga alisema, baada ya kupokea maagizo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa tayari ameanza kuyafanyia kazi yeye pamoja na watendaji wa ardhi ikiwa ni kutatua changamoto za ardhi zinazowakabili wananchi Pamoja na ugawaji wa hatimiliki za ardhi.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amesema Jiji la Dodoma ndio lenye changamoto nyingi za mgogoro ya ardhi na wizara imejipanga kikamilifu kwa kupiga kambi ya wiki mbili ili kuhakikisha changamoto zote za Ardhi mkoa wa Dodoma zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili wananchi wapate haki zao.
“Kliniki ya Ardhi kwa sasa iko Dodoma na niendelevu kwa mikoa yote, pia Wizara ina kusudia kuweka mifumo rahisi ya kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kufunga kamera Katika ofisi za utoaji huduma ili kuepuka mianya ya ukiukwaji wa sheria,” alisema Eng. Anthony Sanga.
Katika hatua nyingine, Eng. Sanga amebainisha wakati mchakato wa kuanzisha kwa Program tumishi yaani ‘Ardhi App’ ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma popote pale nchini kwa njia ya mtandao ikiwemo huduma ya ulipaji wa pango ya ardhi.
Kliniki ya Ardhi inayoendelea Jijini Dodoma itawahudumia Wananchi kwa Wiki mbili ikiwa ni hatua muhimu ya kutokomeza kero za ardhi Jijini hapo pamoja na maeneo mengine yenye changamoto za ardhi hapa Nchini.