PARIS, Ufaransa
UFARANSA imedai kuwa Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 wanaotekeleza mauaji Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Shutuma za Ufaransa dhidi ya Rwanda zimekuja wiki mbili tu baada ya Paris kuhamasisha Umoja wa Ulaya kutoa Euro Milioni 20 kusaidia oparesheni za kijeshi za Rwanda dhidi ya waasi katika jimbo la Kaskazini mwa Msumbiji la Cabo Delgado.
Gazeti la The East African limemnukuu Anne – Claire Legendre, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa akisema Paris inataka pande zote hasimu nchini DRC ziheshimu michakato ya amani ya Luanda na Nairobi.
Alisema, lengo la michakato hiyo ni katika juhudi za kikanda za kusuluhisha mgogoro kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda. Mapatano hayo yanahusu kukomesha kuunga mkono waasi kama hatua ya kwanza ya amani ya kudumu Mashariki mwa DRC.
“Tunalaani uungaji mkono wa Rwanda kwa kundi la M23 na tunaomba kwamba michakato ya Luanda na Nairobi itekelezwe kikamilifu,” ilisema taarifa ya Msemaji huyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ufaransa kulaani waziwazi Rwanda kuhusu waasi wa M23. Pia, ni mara ya kwanza kwa Ufaransa kuielekezea kidole cha lawama hadharani Rwanda, tangu uhusiano wao ulipoanza kuimarika tena takriban miaka mitano iliyopita.
Awali, nchi hizo zilikuwa na mvutano kwa miaka mingi kufuatia madai ya Ufaransa kukataa kushirikiana katika kukabiliana na wahusika wa mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi.
Itakumbukwa, Novemba 23, viongozi kutoka eneo la Maziwa Makuu na Jumuiya ya Afrika Mashariki walikutana huko Luanda, Angola kutafuta suluhu kati ya Rwanda na DRC.
Mkutano huo uliitishwa chini ya upatanishi wa kiongozi wa Angola Joao Lorenco, ambapo ulipendekeza kuondoka waasi wa M23 kutoka maeneo wanayoyakalia na kusitishwa kwa mapigano ‘bila masharti’.
Mjini Nairobi, mwishoni mwa Novemba, mazungumzo zaidi ya amani yalimalizika kwa mapatano kati ya serikali ya DRC na makundi 50 yenye silaha kwa ajili ya kuchukua hatua za kurejesha amani mashariki mwa DRC.
M23 haikuhusika katika mazungumzo hayo ya amani. Tangu wakati huo, viongozi wa M23 wameomba mazungumzo ya moja kwa moja na mamlaka huko Kinshasa.
Hivi sasa, mazungumzo ya amani yanaonekana kutotokelezwa, kwani mapigano mapya yameripotiwa Mashariki mwa DRC huku kundi la waasi la M23 limeonyesha hali ya kusitasita kuhusu ikiwa litashiriki kwenye juhudi za kurejesha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na ukanda wa Afrika Mashariki, au la!
Hili ni licha ya viongozi kadhaa wa nchi Shirika za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusema kuwa, waasi hao wako huru kushiriki katika mazungumzo hayo.
Hali hiyo iliibuka katika mkutano uliofanyika jijini Washington D.C, Marekani, ambako viongozi wa Afrika walikuwa wamehudhuria Kongamano la Amerika na Afrika.
Marais Evariste Ndayishimiye (Burundi), Paul Kagame (Rwanda), William Ruto (Kenya) na Samia Suluhu wa Tanzania walikuwa wamekutana katika mkutano mdogo baina ya viongozi wa eneo la Maziwa Makuu kujadili mizozo na mapigano yanayoendelea DRC.
Juhudi hizo za amani eneo la Maziwa Makuu zinaongozwa na rais wa Angola, Joao Lourenco, ijapokuwa zimeunganishwa na zile za EAC, inayoongozwa na Rais Ndayishimiye.
“Amani katika eneo hili ni jambo la dharura sana. Hatutakubali kupumzika hadi pale amani ya kudumu itarejea Mashariki mwa DRC,” alisema Rais Ndayishimiye baada ya mkutano huo.
Aliongeza: “Tuliwasilisha mapendekezo yetu ya mwisho kwa Rais Felix Tshisekedi kwa hivyo tunatarajia M23 kuanza kuwapokonya silaha wanachama wake.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kenya, Dkt. Alfred Mutua, alisema eneo hili linataka mikataba iliyofikiwa nchini Angola na Kenya kutekelezwa, kama hatua ya kwanza ya kurejesha amani.
“Viongozi walikubaliana kuwa ni muhimu wadau wote katika mzozo huo kuzungumza pamoja ili kupata suluhisho la mzozo huo,” alisema Dkt. Mutua.
Aliongeza, “Mkutano huo ulibuni mbinu nne ili kuharakisha mchakato wa kutafuta amani na kuwapa viongozi tofauti majukumu mbalimbali. Hili linajumuisha ufuatiliaji kuhusu utekelezaji wa mikataba hiyo ili juhudi hizi zipate mafanikio.”
Katika mkataba uliofikiwa jijini Luanda, nchini Angola, Rwanda na DRC ziliahidi kuanza mazungumzo ya pamoja.
Mataifa hayo yamekuwa yakilaumiana kuhusu ufadhili wa makundi tofauti ya waasi. Mkataba uliotiwa saini jijini Nairobi, Kenya, uliyarai makundi yote yenye silaha kuanza mazungumzo na serikali ya DRC ili kupata amani.
Hata hivyo, M23 haikuhudhuria hafla ya kutiwa saini kwa mkataba huo. Pia, Dkt. Mutua hakutoa ufafanuzi kuhusu mbinu hizo nne, ijapokuwa alisisitiza kuhusu umuhimu wa wadau wote kuzingatia masuala yaliyopitishwa kwenye makubaliano hayo.
Mapema Alhamisi, M23 ilisema mapigano mapya yalikuwa yameanza katika eneo la Bwiza, Kivu Kaskazini, huku ikililaumu jeshi la DRC dhidi ya ‘kushambulia ngome zake’.
Msemaji wa kisiasa wa M23, Laurence Kanyuka, alisema jeshi lenyewe ndilo ‘linahujumu juhudi za kurejesha amani’. Jumanne wiki iliyopita, pande hizo mbili zilifanya kikao katika eneo la Kibumba, Kivu Kaskazini, ambapo zilikubaliana kudumisha amani.