MKUTANO wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) leo tarehe 17 Agosti, 2024 umekabidhi jukumu la Unyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ on Politics, Defence and Security) kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Asasi hiyo ina jukumu la kusimamia masuala ya ulinzi na usalama katika kanda ya SADC na ina mamlaka ya kuongoza na kutoa ushauri kwa nchi wanachama katika masuala yanayohatarisha amani, usalama na utulivu katika kanda hiyo. Majukumu hayo huratibiwa katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi hiyo.
Nafasi za uongozi kwa upande wa SADC Organ hufuata mzunguko kama ilivyo katika nafasi ya uongozi wa SADC lakini sio nchi zote zinaweza kuwa Mwenyekiti isipokuwa kwa kigezo cha uwepo wa hali ya ulinzi na usalama katika nchi mwanachama. Tanzania imeshawahi kuwa Mwenyekiti mara tatu katika vipindi tofauti: 2006/2007, 2012/2013 na 2016/2017 na sasa itaongoza kwa kipindi cha 2024/2025 ambapo itakuwa mwenyeji wa vikao vya Asasi hiyo kwa kipindi husika.
Kufuatia utaratibu huo, Troika ya SADC kwa mwaka 2024/2025 inaundwa na Zambia (Mwenyekiti aliyemaliza muda) Tanzania (Mwenyekiti wa sasa) na Malawi (Makamu Mwenyekiti).
Jukumu kubwa linalomkabili Mhe. Rais Samia katika asasi hiyo ni pamoja na kusimamia amani Mashariki mwa DRC hivyo, ataendeleza jitihada zake pale ambapo uongozi uliopita uliishia.
Mkutano huo pia, umemthibitisha Mwenyekiti wa SADC ambapo, Emerson Bambudzo Mnangagwa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe amepokea jukumu hilo na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa SADC imeenda kwa Andry Rajoelina Rais wa Jamhuri ya Madagascar ambapo nchi hizo zitaongoza katika kipindi cha 2024/2025.
Akihutubia mkutano huo Mwenyekiti wa SADC, Mnangangwa amempongeza Rais Samia kwa kupokea jukumu la uenyekiti wa SADC na amemuhakikishia ushirikiano katika kufanikisha majukumu hayo waliyokabidhiwa kwa ustawi wa kanda na wananchi wake.
Pia, ameeleza kuwa jumuiya hiyo inaendelea kufungua fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kikanda kupitia agenda yake ya kipaumbele ya maendeleo ya viwanda. Jitihada hizo zitakuza ubunifu na kuongeza thamani ya bidhaa katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kuhusu shughuli nyingine zilizofanyika sambamba na mkutano huo Mnangagwa ameeleza kuwa kulikuwa na Kongamano la Uwekezaji lililoandaliwa na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA) na Wiki ya Viwanda ambazo zilitumika kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali kutoka nchi wanachama pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabishara kubadilishana uzoefu na kukuza mtandao wa biashara.
Shughuli nyingine iliyofanyika ni pamoja na mhadhara wa umma ambao unasaidia katika kujenga uelewa wa masuala ya msingi ambayo husaidia katika ubunifu na kuendelea kuimarisha hatua za mtangamano. Hivyo ni muhimu kwa vyuo vikuu na vyuo vingine vinavyofanana navyo kutafakari namna bora ya kuwekeza katika ubunifu ili kuwezesha mikakati ya kikanda kupata matokeo ya kimaendeleo kwa mafanikio.
Pamoja na hayo amesisitiza umuhimu wa kukuza sekta ya nishati, kilimo, biashara, uwekezaji na usafirishaji na kuhimiza umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto zake na kuiwezesha jumuiya hiyo kuinuka kiuchumi.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali pia umemalizika kwa kusainiwa kwa: Itifaki ya Ajira na Kazi, Tamko la Kuwalinda Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi na Tamko la Kutokomeza Ugonjwa wa Ukimwi kama Janga la Kiafya kwa Jamii ya Ukanda wa SADC ifikapo 2030.