Tume ya madini na mikakati ya Mapinduzi ya kiuchumi

0
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo

Na Iddy Mkwama

TUME ya Madini ni Taasisi ambayo ipo chini ya Wizara ya Madini, ilianzishwa mwaka 2017 chini ya sheria ya Madini sura ya 123 ikiwa na jukumu la kusimamia shughuli zote zinazohusiana na madini kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 22 cha Sheria ya Madini.

“Tume ina dira ya kuwa kitovu cha utafutaji na uchimbaji endelevu wa madini Afrika kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” anasema Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo, kwenye Kikao na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika Oktoba 24, jijini Dar es Salaam.

Aidha, Lwamo anasema tume hiyo ina dhima ya kudhibiti sekta ya madini kupitia usimamizi, ufuatiliaji, udhibiti, utafutaji, uongezaji thamani wa biashara ya madini kwa ajili ya maendeleo endelevu.

“Lengo ni kuhakikisha tunaboresha usimamizi na udhibiti katika ukaguzi wa uzalishaji na biashara ya madini na kuhakikisha Sheria, Kanuni na taratibu zote zinazoongoza shughuli za madini zinafuatwa ipasavyo ili kuongeza Pato la Taifa,” anasema Mhandisi Lwamo.

Mhandishi Lwamo, kupitia kikao hicho alitaja vipaumbele vya tume hiyo ikiwemo kuimarisha utendaji kazi: “Hapa kwenye kuimarisha mazingira ya utendaji kazi, nyie wenyewe ni mashahidi, juzi tumepokea magari 25 ambayo yatakuwa ni chachu ya ukusanyaji wa maduhuli pamoja na shughuli za ukaguzi kwenye sekta ya madini.”

Magari hayo, yalikabidhiwa Oktona 21, jijini Dodoma na Waziri wa Madini Anthony Mavunde kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji wa maduhuri, ambapo aliwataka watumishi watakaokidhiwa magari hayo kuhakikisha wanayatumia ipasavyo na kufikia lengo lililokusudiwa.

Kipaumbele kingine alichotaja Mhandisi Lwamo ni kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini, kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo.

Aidha, kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi ili kunufaika na rasilimali madini, “tuna eneo la kipaumbele kuelimisha umma na kuboresha mahusiano baina ya tume na wadau mbalimbali kuhusu masula ya madini, vile vile tuna kipaumbele cha kuendeleza rasilimali watu katika mazingira ya kazi.”

Mbali na vipaumbele hivyo, Mhandisi Lwamo alitaja mafanikio ambayo yamepatikana ikiwemo ukusanyaji wa maduhuli na kuweka wazi kwamba, mbali na mambo mengine, utendaji kazi wa tume hiyo unapimwa kwa kiasi kikubwa na eneo hilo.

“Utendaji kazi wa tume mbali na kupimwa na vitu vingi, lakini kikubwa ni ukusanyaji wa maduhuli ambacho ni kipimo cha muhimu sana. Ukiangalia ukisanyaji wa maduhuli, yamekuwa yakikua mwaka hadi mwaka,” anasema.

Akitaja kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali anasema, kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024.

“Ukiangalia mwaka huu, 2024/2025, tumekewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni Moja sawa na wastani wa kukusanya Bilioni 83.33 kwa mwezi, hadi kufikia Oktoba 21, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya Jumla ya Shilingi bilioni 312.75 sawa na asilimia 31.28 ya lengo la mwaka,” anasema Mhandisi Lwamo na kusisitiza kuwa, wanaendelea vizuri na wanaamini lengo la kukusanya Trilioni Moja litafanikiwa.

Pia, kumekuwa na mchango wa ukuaji wa sekta, katika miaka mitatu 2021 hadi 2023, sekta imekua kwa kuongezeka, ilianza kwa asilimia 9.4 mwaka 2021, mpaka sasa imefika 11.3. “Mchango wa sekta kwenye Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka, ambapo 2020/2021 ilikuwa 7.2, lakini hivisasa tupo kwenye asilimia 9 na lengo ni kufika asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.”

Mhandisi Lwamo anasema, kwenye upande wa usimamizi wa masoko, ufanisi kwenye masoko umekuwa na mchango mkubwa hususani katika kuwapatia sehemu maalum wachimbaji wadogo kwa ajili ya kuuza madini yao “ukiangalia mchango wake katika ukusanyaji, masoko yaliwezesha kuuza madini.”

Katika Mwaka wa 2021/2022 mauzo yalikuwa Shilingi bilioni 2,361.80 na mapato ya Serikali yaliyopatikana ni Shilingi bilioni 164.09 ambapo mapato hayo yalihusisha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini.

Mwaka 2022/2023 mauzo Shilingi bilioni 2,240.100 Bilioni 157.43, 2023/2024 mauzo ya madini katika Masoko na Vituo vya Ununuzi wa madini yalikua Shilingi bilioni 2,592.02 na mapato yaliyopatikana kutokana na mauzo hayo ni kiasi cha Shilingi bilioni 180.13 na mwaka wa fedha 2024/2025 hadi sasa mauzo ni Shilingi bilioni 956.76, mapato Shilingi bilioni 65.

Anasema, moja ya malengo ya kuanzishwa kwa tume hiyo ni wananchi kunufaika na sekta ya madini na katika hili tume imejitahidi kutenda haki, ambapo wamekuwa wakipitisha mipango ya ushirikishwaji wa wananchi katika sekta ya madini pindi wanapotaka kufanya shughuli zao; aidha kutoa huduma, au kufanya shughuli yoyote katika migodi.

“Jumla ya Mipango 1,050 ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi. Kati ya Mipango iliyowasilishwa, 1,036 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Mipango 14 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho,” anasema.

Aliendelea kusema, katika eneo hilo la kuwawezesha watanzania, Tume hiyo imesimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Makampuni mbalimbali ya uchimbaji, ambapo Kampuni zilizalisha ajira 19,356, kati ya hizo 18,853 ni Watanzania sawa na asilimia 97.40 na 503 ni wageni sawa asilimia 2.60 ya ajira zote zilizozalishwa.

Anasema jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodin, kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.

“Ukiangalia zaidi ya asilimia 90 ya mauzo migodini, yanafanywa na watanzania. Haya ni mapinduzi makubwa kwa uchumi wa nchi yetu na yanaonyesha jinsi gani watanzania wanavyoshiriki katika uendelezaji wa sekta hii muhimu na hivyo kupunguza umaskini na kuongeza ukaribu wa sekta hii ya madini na sekta nyingine,” anasema.

Aidha, tume ya madini imekuwa ikitoa mafunzo ya ugani kuhusu usalama, afya, mazingira pamoja na usimamizi wa baruti ili kuwa na uchimbaji salama na endelevu, ambapo wachimbaji 867, 124 walinufaika.

“Ili shughuli za madini ziwe na tija, kitu cha kwanza kabisa ni usalama, bila usalama hakuna uzalishaji na hakuna faida yoyote, kwa hiyo tume ya madini imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kunakuwa na usalama kwenye maeneo ya migodi kwa wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo kuhakikisha uchimbaji unakuwa endelevu kwa vizazi na vizazi,”

“Vile vile kuhakikisha watumishi wanaokwenda kufanyakazi, wanakwenda wakiwa salama na waanrudi wakiwa salama na kuongeza mapenzi ya kuendeleza sekta yao, sehemu ambayo haina usalama, ajali zikiwa nyingi,”

 “Watu wanakuwa vilema, sio rahisi hata kama wewe ni mzazi kumsisitiza mwanao kusoma uhandishi wa migodi, kwa hiyo suala la usalama limekuwa ni wimbo wetu katika shughuli zetu za kila siku.”

Pia, kwenye kuendeleza wachimbaji, anasema walitenga maeneo yenye tija kwa ajili ya shughuli za uchimbaji hadi sasa maeneo 58 yametengwa na imesaidia kupunguza uvamizi na kusaidia vijana wengi kujumuika kwenye uchimbaji ulio rasmi, vile vile wamefanikiwa kuwaunganisha wachimbaji na Taasisi za Kifedha ili waongeze mitaji yao katika shughuli za uchimbaji.

Kwenye upande wa utoaji na usimamizi wa leseni, tume ya madini imekuwa ikifanya vizuri, katika kipindi cha kuanzia 2021/2022 hadi 2024/2025, Tume ilikusudia kutoa leseni 37,318 hata hivyo hadi kufikia Septemba 30, 2024/2025 Tume ilifanikiwa kutoa jumla ya leseni 34,348 sawa na asilimia 92.04 kati ya leseni zilizopangwa kutolewa.

“Leseni hizo zilijumuisha leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini. Tunaamini hadi tutakapomaliza mwaka wa fedha 2024/2025, lengo hilo tutakuwa tumelifikia la kutoa leseni 37,318,” anasema.

Anasema, tume pia imefanya ukaguzi wa mazingira, migodi mikubwa 9, migodi ya kati kaguzi 144 na migodi 47, 535 ilikaguliwa, huku usimamizi ukifanyika kwenye stoo na maghala ya baruti, ujenzi na matumizi salama ya mabwawa ya tope sumu na uhifadhi wa miamba taka. “Tume imeendelea kutoa mafunzo ya usalama mahala pa kazi na utunzaji wa mazingira kwa wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo.”

Katika kuhakikisha inafanikiwa kwenye malengo yake na kuendeleza ufanisi uliopo sasa, Tume ya Madini imeweka mikakati endelevu ikiwemo kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwandani.

Mikakati mingine ni kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini hususani utoroshaji wa madini kwa kuhamasisha umuhimu wa kutumia Masoko na vituo vya madini nchini; kuimarisha vituo vya ukaguzi (exit-points) katika maeneo ya mipakani, bandarini pamoja na viwanja vya ndege lengo likiwa ni kupunguza matukio ya utoroshaji wa madini na hivyo kuwezesha Serikali kupata takwimu sahihi na mapato stahiki.

“Uboreshaji na usimamizi thabiti wa Mfumo wa Utoaji wa Leseni za madini, matokeo ni kupunguza migogoro itokanayo na mwingiliano wa maombi ya leseni, kupunguza muda wa utoaji huduma pamoja na kuongeza idadi ya leseni zitakazotolewa kwa mwaka hivyo kuhamasisha uwekezaji,” anasema Mhandisi Lwamo.

Mkakati mwingine ni kuimarisha ukaguzi katika shughuli za uchimbaji katika migodi kwa lengo la kuwa na uchimbaji endelevu unaozingatia usalama, afya na mazingira; lengo ni kuongeza mapato, kuimarisha uchimbaji endelevu unaojali mazingira kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Tutaimarisha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMO’s) na Maabara katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji hapa nchini, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wadau hivyo kuchochea uwekezaji utakaowezesha Serikali kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini,” anasisitiza Mhandisi Lwamo.

Anasema, wataimarisha shughuli za tafiti zinazohusiana na utambuzi wa vyanzo vipya vya mapato yatokanayo na rasilimali za madini ili kuiwezesha Taasisi hiyo kuongeza wigo wa makusanyo yatokanayo na rasilimali madini ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa wachimbaji wa madini na kuongeza mapato, ajira na kuwa Sekta endelevu.

Kutokana na mikakati hiyo, Mhandisi Lwamo anasema wanatarajia matokeo mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato na kuimarisha uchimbaji endelevu, kupungua kwa matukio ya utoroshaji wa madini, kupunguza migogoro itokanayo na muingiliano wa maombi ya leseni na kuongeza mapato, ajira na kuwa na sekta endelevu.

“Sekta ya madini ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa. Mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita ni kielelezo cha uongozi imara na Madhubuti wa Rais Samia Suluhu Hassan. Aidha, ukuaji wa sekta utasaidia kuongeza mapato ya serikali na kukua kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa kufikia 10% ifikapo 2025,” anasema Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here