Na Muhammed Khamis, TAMWA-ZNZ
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar TAMWA-ZNZ kimesema ili wanawake wengi zaidi waweze kushika nafasi za uongozi waandishi wa habari wana wajibu wa kuripoti habari zitakazowaibua wanawake katika shughuli mbali mbali zitakazowawezesha wanawake kushika nafasi hizo.
Kauli hiyo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama hicho Dkt. Mzuri Issa alipokua akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari vijana kutoka Unguja na Pemba ambao wanaendelea kupatiwa mafunzo maalumu ya kujengewa uwezo juu ya kuripoti habari za wanawake kushika nafasi za uongozi sambamba na kuchochea uwajibikaji kwa maslahi ya Umma.
Alisema, kwa muda mrefu wanawake wengi wamekua wakishindwa kufikia malengo ya kushika nafasi za uongozi katika ngalizi mbalimbali kutokana na dhana potofu ya kuamini wanaume pekee ndio wanapaswa kuwa viongozi jambo ambalo linapingwa na mikataba yote ya kikanda na kimataifa.
“Nyinyi waandishi wa habari vijana muna nafasi kubwa kuibadili hali hii, sauti zenu ni kubwa zaidi ambazo mkizitumia vizuri tunaweza kufika tunapopataka’’ alisema.
Kwa upande wake mmoja miongoni mwa waanzilishi wa TAMWA Bi Fatma Aloo akizungumzia harakati mbali mbali alizowahi kupitia zikiwemo za kuazisha chama hicho mwaka 1987 hii kutokana na ari waliyokua nayo wakiwa watu wachache sana.
Alisema, wao kama wanawake wakati wanaanza na harakati hizo walipewa majina mengi, lakini hawakukata tamaa wala kurudi nyuma bali waliangalia ni vipi wanaweza kufikia malengo yao.
Aliwataka wanahabari hao kujiwekea malengo pamoja na kuwa watu wenye misimamo pale wanapoamua kutafuta jambo kwa maslahi ya wanawake na umma kwa ujumla.
Akitoa ushuhuda Mwenyekiti wa Jumuia ya kupambana na changamoto zinazowakabili wajane Zanzibar (ZAWIO) Tabia Makame alisema, wanawake wanaotaka kuwa viongozi wana wajibu wa kujitambua na sio kuwa warahisi kwa kila jambo.
Alisema, kuna idadi kubwa ya wanawake wanaoshindwa kufikia malengo yao kwa sababu wanashindwa kujielewa na kwa hali hiyo wanajikuta wanaingia kwenye mgongano na wasiopenda kuona wanawake wakipiga hatua zaidi za kimaendeleo.
“Lazima tukubali ukweli udhalilishaji kwenye sehemu za kazi upo lakini ni wachache wanaoweza kukubali kuacha kazi kwa kulinda heshima yao hivyo ni lazima nyinyi vijana wadogo mjitambue’’ aliongezea.
Akitoa ushuhuda mwengine Makamu wa Rais mstaafu kutoka Chuo cha Kikuu cha Zanzibar (ZU) na Waziri wa fedha Bunge la vijana Tanzania Zainab Salum Saleh alisema wanawake wanaweza kufikia malengo yao iwapo watajitoa katika kila jambo.
Pamoja na changamoto ambazo wanawake wanapitia wanapoonesha dhamira yao ya kuwa viongozi lakini kwa pamoja hawapaswi kukata tamaa na changamoto hizo badala yake wazione kama fursa za kusonga mbele.
Sambamba na hayo aliwataka vijana wenzake wanaotaka kuwa viongozi kukimbia kabisa viashiria vya rushwa pindi wanapoviona kwa sababu kuchukua sehemu hiyo ni kujiharibu pia kuikandamiza jamii yako na kufanya jambo hilo liendelee.
Jumla ya waandishi wa habari vijana 18 kutoka Unguja na Pemba wanaendelea kujengewa uwezo kupitia mradi unaotekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na shirika la “National Endowment for Democracy – NED”