MANCHESTER, Uingereza
KOCHA Erik ten Hag amemwekea Marcus Rashford malengo ya kupachika wavuni mabao 20 msimu huu ili kusaidia Manchester United kuhimili ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wakuu kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Kufikia sasa, Rashford, ameifungia Man United mabao matatu na kuchangia mengine mawili. Hiyo ni ishara ya kuimarika kwake ikizingatiwa alipachika wavuni magoli matano na kuchangia upatikanaji wa mabao msimu uliopita wa 2021-22.
“Rashford analenga kuwa sehemu ya kikosi kitakachochezea Uingereza kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Qatar. Amefufua makali yake na ndiye atakuwa fowadi tegemeo katika safu ya mbele ya Man United,” alisema Ten Hag.
“Ana uwezo mkubwa wa kuwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi duniani na tayari amedhihirisha hilo kwa matokeo ya kuridhisha kwenye mechi chache za muhula huu. Inawezekana atufungie mabao 20 na kusaidia kikosi kutwaa taji la EPL,” aliongeza kocha huyo.
Manchester United waliofungiwa mabao mawili na Rashford katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Arsenal mnamo Septemba 4, 2022 ugani Old Trafford, wanakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa EPL kwa alama 12, mbili pekee nyuma ya Tottenham Hotspur na mabingwa watetezi, Manchester City.