PARIS, Ufaransa
NYOTA Neymar Jr, ameshika nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote kambini mwa Paris Saint – Germain (PSG) baada ya kupachika bao dhidi ya Brest na timu yake kupata ushindi wa 1-0 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mwishoni mwa wiki.
Matokeo hayo yaliwadumisha PSG kileleni mwa msimamo wa Ligue 1 kwa alama 19, sawa na Olympique Marseille waliokung’uta Lille 2-1. Lens wanafunga mduara wa tatu – bora kwa pointi 17 baada ya kupepeta Troyes 1-0 uwanjani Bollaert-Delelis.
Goli dhidi ya Brest lilikuwa lake la nane kutokana na mechi saba za Ligue 1 msimu huu, na lilimwezesha kumpiku Pedro Pauleta wa Ureno aliyewahi kufungia PSG mabao 109 kati ya 2003 na 2008.
Neymar sasa anasogelea rekodi ya Zlatan Ibrahimovic, aliyewahi kufunga mabao 156 akichezea PSG kati ya 2012 na 2016.
Kylian Mbappe, ndiye wa pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa PSG inayoongozwa na Edison Cavani wa Uruguay aliyecheka na nyavu mara 200 kati ya 2013 na 2020 kabla ya kuhamia Manchester United kisha Valencia.