Rais Samia: Hatukutoa fursa watu wakavunje sheria

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wadau wa Demokrasia kabla ya kufungua Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Hali ya Siasa nchini. Mkutano huo umefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 2023.

Na Samson Alex

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wapinzani nchini kujenga hoja na kutumia vizuri fursa iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kufanya mikutano ya hadhara.

Rais Samia amezungumza hayo kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia kwenye Mkutano Maalum wa Baraza la vyama vya siasa na wadau wa Demokrasia na kuwataka wanasiasa hususani wa vyama vya upinzani kufuata kanuni zilizoundwa kwa ajili ya kuongoza mikutano hiyo.

Alisema, Serikali iliruhusu mikutano ya hadhara wakiwa na nia vyama vya siasa vizungumze ili wananchi wasikie sera zao na mipango yao kwa lengo la kuvikuza vyama hivyo na kurudisha nguvu zao na wafuasi waliowapoteza na ukifika wakati wa uchaguzi wawe madhubuti na wamejijenga vya kutosha.

“Ndio maana kutoa fursa hii ya mikutano ya hadhara, hatukutoa fursa ile watu wakavunje sheria, watu wakasimame kutukana, watu wakasimame kukashifu, watu wakasimame kuchambua dini za watu, lakini sishangai kwanini haya yanatokea, kwasababu ya kuzungumzwa hakuna,” alisema Rais Samia.

Aliendelea kusema: “Tulianza na Katiba, tukaenda ikakatika kati kati, bandari imeenda sasa Katiba tena, hakuna…kwahiyo sasa unapokuwa hakuna na unapolazimisha useme jambo, utazungumza yasiyokuwepo au yasiyo katika mwelekeo,”

“Kwa hiyo tumetoa fursa hiyo na niwaombe sana vyama vya siasa, tumieni hiyo fursa, kajijengeni kwa wananchi, elezeni sera zenu, elezeni mtafanya vipi, elezeni mmejipanga vipi, ili wananchi warudi, wawaunge tena mkono; tukienda kwenye uchaguzi vyama vyote viwe vimesimama vizuri, hilo ndilo la kufanya,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, mapema mwaka jana wakati Rais Samia alipotangaza kuruhusu mikutano ya hadhara, Chama cha Wakulima (AAFP) kilitoa tamko la kuvitaka vyama vya siasa nchini kutumia vizuri fursa hiyo, ingawa inaonekana ushauri wake haukuzingatiwa, ambapo baadhi ya vyama vimeonekana kwenda kinyume na kanuni zilizowekwa.

Mwenyekiti wa AAFP Said Soud Said wakati anatoa tamko hilo akiwa Wilaya ya Chakechake, Kisiwani Pemba, aliwataka wanasiasa wachuje na kupima maneno yao kabla ya kutamka.

Soud alisema, Mataifa mengi duniani yamejikuta yakiingia kwenye mivutano, mitafaruku, mapigano na hata kusababisha umwagaji damu kutokana na chuki za kisiasa, vurugu au kutumika kwa lugha chafu.

Alisema, zipo tabia za baadhi ya wanasiasa wanaposhindwa kufafanua sera, mirengo yao kisiasa na itikadi za vyama vyao hujikuta wakitoa kejeli, matusi na kebehi, jambo ambalo alidai hupandikiza chuki na ukorofi katika jamii.

“Kulingana na ripoti iliyowasilishwa na kikosi Kazi cha Rais kupendekeza ianze mikutano ya hadhara, ni lazima Serikali mapema iweke tahadhari mikutano inapohutubiwa na wanasiasa. Nashauri ndimi zetu zidhibitiwe kikanuni na kisheria,” alisema Soud.

Aidha, Mwenyekiti huyo aliongeza kusema kuwa, vyama vya siasa vitabaki milele, lakini Taifa likizanishwa kwa hitilafu za maneno yenye tashwishi za kikabila, dini au ukanda ili kusimama tena haitakuwa kazi nyepesi.

Alisema, wapo baadhi ya wanasiasa ni hodari wa kutunga uongo, uzushi na fitna na kueneza ikiwemo kuwavunjia heshima watu wengine wakiwemo viongozi wa Kitaifa bila ushahidi wa tuhuma zinazotewa.

“Ikiwa siasa zetu zitafanyika kama baadhi ya watu wanavyoandika katika mitandao ya kijamii, Taifa letu litazama. Tufanye siasa zenye ukomavu kwa kutoa hoja yakinifu. Atakayemtuhumu mwenzake au kumvunjia heshima akishitakiwa atoe ushahidi,” alieleza Soud.

Pia, alisema mfumo wa vyama vingi si kibali kwa upinzani kuukejeli utawala au utawala kuuvunja upinzani kwa maneno yanayokiuka maadili, utu au kuvunja miiko ya utamaduni wetu.

Soud alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa Serikali yake kuunda kikosi Kazi kilichokusanya maoni ya wadau wa demokrasia ikiwemo pendekezo la kuruhusiwa kufanyika mikutano ya hadhara.

“Tumpe muda Rais Samia na vyombo vyake vya dola vifanye uchambuzi utakaoendelea kuliweka pamoja Taifa letu. Bado Tunahitaji kubaki na umoja wa Kitaifa, ustawi wa amani na utulivu wa kisiasa,” alisisitiza Soud.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here