Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) limepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 baada ya kufanya mabadiliko ya Kiutendaji ili kujiimarisha zaidi Kibiashara.
NIC ni kampuni inayomilikiwa na Serikali kwa 100%, ikiwa na dhamira ya kufanya biashara ya bima za mali na ajali pamoja na bima ya maisha; ni miongoni mwa Makampuni zaidi ya 30 yaliyopo kwenye soko la bima nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Dkt. Elirehema Doriye alisema, Shirika hilo limekuwa likichukua hatua mbalimbali za mabadiliko ya Kiutendaji na Kibiashara tangu Julai, mwaka 2019 na kumudu ushindani ambao umewawezesha kufanya vizuri kwenye soko.
Dkt. Doriye alisema mabadiliko waliyoyafanya ni kwenye upande wa uongozi ili kuongeza ufanisi, weledi na tija, pia wamewekeza kwenye rasilimali watu kwa kuajiri wafanyakazi wenye sifa stahiki, wenye weledi na wabunifu.
Aidha, alisema NIC wamewekeza kwenye mifumo ya TEHAMA ambayo imewasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza Mapato, kuondoa matumizi ya karatasi, kupunguza muda wa kulipa madai hadi kufikia siku saba na kurahisisha utoaji wa huduma.
Alisema, kutokana na hatua za mabadiliko ambazo walizichukua kuanzia mwaka 2019, wamefanikiwa kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka Shilingi Bilioni 76.45, mwaka 2019/2020 Shilingi Bilioni 103.94 mwaka 2021/22. “Ongezeko hili ni sawa na asilimia 17.98 kwa mwaka.
“Vilevile usimamizi madhubuti wa matumizi pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi kumeongeza ufanisi na kuondoa matumizi yasiyo na tija, jambo lililoshusha gharama za uendeshaji na kuongeza faida,” alisema Dkt. Doriye.
Dkt. Doriye alisema, katika kipindi cha miaka mitatu, NIC wamefanikiwa kulipa madai ya bima za wateja, ambapo hadi kufikia Juni 2022, wamelipa Shilingi Bilioni 33.79 kwa bima za Maisha na Shilingi Bilioni 40.18 kwa bima za mali na ajali.
“Tumeweza kulipa kodi ya mapato Serikalini kutokana na faida inayopatikana, ambapo ulipaji huo umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 11.86 mwaka 2019/20 hadi Shilingi Bilioni 15.14 mwaka 2021/22 sawa na wastani wa asilimia 13.80 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye.
Akizungumzia faida iliyopatikana kwa kipindi hicho, Dkt. Doriye alisema, faida ghafi imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 33.65 hadi Shilingi Bilioni 63.21 ambayo ni sawa na asilimia 43.91.
“Kutokana na faida mfululizo, tumeweza kupata malimbikizo ya faida ya Shilingi Bilioni 45.74 kufikia Juni 2022 kutoka kiasi cha malimbikizo ya hasara ya Shilingi Bilioni 19.31,” alisema.
Mbali na hayo, alizungumzia kukua kwa mali za NIC; kutoka mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 350.36, hadi kufikia mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 423.99, ambapo ukuaji huo ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 10.51 kwa mwaka.
“Ufanisi katika uendeshaji umewezesha ukuaji wa mtaji wa wanahisa kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 72.16 hadi Shilingi Bilioni 217.07, ukuaji huu ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 100.40 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye.
Katika kipindi cha miaka mitatu, NIC pia imefanikiwa kuongeza uwekezaji katika hati fungani za Serikali, kutoka Shilingi Bilioni 51.58 hadi Shilingi Bilioni 105.64, ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 52.40 kwa mwaka.
“Uwekezaji katika amana ya benki umefikia Shilingi Bilioni 32.23 ukilinganisha na Shilingi Bilioni 19.53 kilichokuwepo mwaka 2019/20, ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 32.54 kwa mwaka,” alisema Dkt. Doriye na kuongeza kuwa, mwaka uliopita 2022 wametoa gawio la Shilingi Bilioni 2.0 kwa Serikali, ukilinganisha na gawio la Shilingi Bilioni 1.5 walilotoa mwaka 2021.
Katika hatua nyingine, Dkt. Doriye alisema, ili kukabiliana na uwezo mdogo wa kuhimili hasara inayoweza kutokea (low underwriting capacity) wamefanikiwa kuongeza mtaji wa Shilingi Bilioni 12.05 Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 408.47.
“Hii ni kutoka mtaji uliokuwepo wa kiasi cha Shilingi Bilioni 2.95 na kufikia mtaji wa Shilingi Bilioni 15, kilichopo sasa,” alisema Dkt. Doriye na kusisitiza kuwa, NIC itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya bima nchini na kutoa elimu ya bima kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili watanzania wengi wajiunge na huduma zinazotolewa na Shirika hilo.
“Bidhaa na huduma zetu zinapatikana KIDIJITALI zetu, kwa mfano 13% ya mapato yetu ya bima yameandikishwa Kidijitali,” alisema.