Rais Samia atimiza ndoto ya bwawa la mifugo la mwaka 1975

0
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, (wa kwanza) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Kiteto Edward Ole Lekaita (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara Mbaraka Al Haji Batenga (wa kwanza kushoto), wakati Ulega akikagua maeneo ya bwawa la Kaiwang lililopo katika Wilaya ya Kiteto ambalo serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya Shilingi Milioni 500 kulijenga upya baada ya kupasuka na kutofanya kazi tangu Mwaka 1978. (Picha na Edward Kondela - Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na Edward Kondela

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametimiza ndoto ya Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya kujenga upya bwawa ambalo Mwl. Nyerere alilijenga Mwaka 1975 na kupasuka Mwaka 1978.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amebainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, kukagua bwawa la Kaiwang katika Kijiji cha Ndedo ambalo likikamilika maji yake yatatumiwa na mifugo, wanyama wa porini pamoja na matumizi ya kibinadamu.

Naibu Waziri Ulega alisema, ni fahari kubwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutimiza ndoto ya Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufuata maono yake kwa kuhakikisha bwawa hilo linaanza upya kufanya kazi mara baada ya kujengwa ambapo tayari mkandarasi ameshalifanyia tafiti mbalimbali na kwamba muda wowote ataanza kufanya kazi ya ujenzi.

“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anakuja kutimiza ndoto ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere anafanya mengi yaliyootwa na kuwazwa na Mhe. Rais wa awamu ya kwanza Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba tayari fedha zimetengwa.” alisema Ulega.

Aidha, amewataka wakazi wa Wilaya ya Kiteto watakaolitumia bwawa hilo ambao wameomba liitwe Mama Samia Kaiwang kwa kushukuru jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu kuhakikisha wanalitunza ili liweze kuleta tija kwao kwa kuwa watapata maji mengi na kuondokana na adha hiyo kwa mifugo yao.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Kiteto Edward Ole Lekaita akizungumza kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, alisema mradi huo utawafanya wananchi wa eneo hilo kumkumbuka Rais Dkt. Samia maisha yao yote kwa kuwa asilimia 90 ya wakazi wanaozunguka bwawa hilo ni wafugaji.

Aliongeza kuwa, wanashukuru namna serikali ya awamu ya sita inavyoshughulika na changamoto zinazowakumbuka wananchi wakiwemo wafugaji hususan katika suala la mabwawa, malisho na majosho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto John Nchimbi ameelezea kuwa, hadi sasa ujenzi wa bwawa hilo umefikia hatua ambayo eneo limeshafanyiwa tafiti mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya bwawa na uimara wa udongo ambapo matarajio ya ujenzi wa bwawa hilo utagharimu zaidi ya Shilingi Milioni 500.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here