Na Mwandishi Maalumu
RAIS Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Tuzo ya Chakula Afrika, akichukua nafasi ya Rais wa zamani wa Nigeria Jenerali Olusegun Obasanjo ambaye amekuwa Mwenyekiti tangu 2016.
Hafla ya kutangazwa kwa uteuzi huo imefanyika katika Hoteli ya Radisson Blu mjini Addis Ababa, Ethiopia, Ijumaa, Februari 17, 2023, kando ya Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Umoja wa Afrika.
Tuzo ya Chakula Afrika ni tuzo inayotambua wanawake, wanaume, na taasisi ambazo michango yao katika kilimo cha Kiafrika inaanzisha enzi mpya ya usalama endelevu wa chakula na fursa ya kiuchumi ambayo inainua Waafrika wote.
Uteuzi wa Dkt. Kikwete unaenda sambamba na wito wa wagombea kwa mwaka 2023 kuwania Tuzo hiyo ya Chakula Afrika yenye kitita cha Zawadi cha Dola za Marekani 100,000. Mwaka huu, kampuni ya Nestlé ikishirikiana na Tuzo ya Chakula Afrika, imechangia pesa hizo ambazo zitatolewa kwa mshindi wa tuzo kuu.
Jenerali Obasanjo alimshukuru Dkt. Kikwete kwa kuukubali uteuzi huo, akimtaja kuwa ni mtu mwenye mapenzi na ari ya dhati katika kuleta mageuzi ya kilimo barani Afrika.
“Nampongeza Dkt. Kikwete kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tuzo ya Chakula Afrika. Nina imani kuwa bara hili litaendelea kutafiti na kutekeleza mikakati ya mifumo ya chakula ambayo itawainua watu kutoka katika umaskini kupitia ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu,” Obasanjo alisema kwenye hafla hiyo.
Jenerali Obasanjo alisema kuwa Dkt. Kikwete ana rekodi nzuri sana ya kuwa mchangiaji mkuu katika mabadiliko ya mifumo ya chakula barani Afrika, na kwamba akiwa rais wa Tanzania, alitekeleza ‘Kilimo Kwanza’ mpango ambao ulifungua tija na faida kwa wakulima wadogo nchini humo.
“Dkt. Kikwete pia anatajwa kama kiongozi ambaye aliongoza utekelezaji wa Ukanda wa Kukuza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), ubia kati ya sekta ya umma na binafsi unaolenga kufungua uwekezaji zaidi wa sekta binafsi katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.
“Baada ya kustaafu, Dkt. Kikwete kupitia Taasisi yake ya JMKF amekuwa akishirikiana na wakulima na watafiti kuandaa mipango na mikakati ya kuongeza mavuno na tija katika kilimo cha wakulima wadogo na biashara ya kilimo”, aliongezea Rais huyo mstaafu wa Nigeria.
Mashirika, taasisi, biashara na watu binafsi ambao wameunda fursa kwa wakulima wa Afrika kupata riziki kutokana na biashara yao wanaweza kuwasilisha mapendekezo yao kwenye www.africafoodprize.org/nominate kabla ya Jumatatu, 16 Mei 2023.