Raha na utamu wa ngoma ya mdumange

0

Na Mohamed Kazingumbe

NGOMA kwa ujumla wake ni mlindimo wa ala za asili au hata ya kigeni mlindimo au mvumo unaosisimua mwili wa wachezaji na kufuata mapigo hayo.

Hapo mwenye asili ya ngoma hiyo hushikwa na mdadi au mzuka na kucheza kwa mbwembwe kulingana na aina ya ngoma husika.

Makabila mengi katika nchi mbalimbali hunyumbuka na kucheza kwa furaha kubwa kwa wachezaji wakionyesha uhodari wao.

Kupitia ukurasa huu, tumewahi kuona jamii ya Wayao na wangoni wanavyojivunia utamaduni wao kwa ngoma zao zikiwemo “Masewe” Kwa Wayao na “Mganda” na Lizombe kwa Wangoni. Ni ngoma zao wanazocheza kwa nyakati mbalimbali na madhumini mbalimbali.

Leo tunahamasika kuwatembelea jamii maarufu ya Wasambaa waliosambaa katika milima ya Usambaa katika wilaya za Lushoto, Handeni, Korogwe na wilaya ya Muheza, mkoa wa Tanga.

Hawa jamaa, ni hodari sana kwa ngoma ya “Mdumange”. Ngoma ya mdumange utamu wake ni pale unapoingia uwanjani na kucheza mapigo yake. Mdumange ni rahisi kuchezwa na kila mtu; ngoma ambayo haina mwenyewe tunaweza kusema ni ngoma ya wote, kwani kila mmoja iwe mgeni au mwenyeji anaweza kuinuka na kucheza. Ni rahisi kuchezwa na kila mtu.

Ni ngoma inayochezwa na wanaume na wanawake na kihistoria ni ngoma inayochezwa nyakati mbalimbali za furaha ikiwa ni pamoja wakati wa kufurahia mavuno; harusi; kumtoa mwali baada kuvunja ungo kwa watoto wa kike ; watoto wa kiume baada ya kitendo cha tohara (jando).

Asia Mariki ni msambaa wa Lushoto huko mkoani Tanga. Anasimulia jinsi ngoma ya Mdumange inavyochezwa na wenyeji wa kabila lake.

Anaelezea hayo alipohojiwa na mwandishi wetu huko kwenye mitaa ya Chanika- Magenge, Jijini Dar es Salaam hakusita kuelezea jinsi kabila lake linavyopenda kucheza ngoma hii. Anajitambulisha na kunogesha sifa za wasambaa wakijinadi kupitia ngoma yao hiyo maarufu ya mdumange.

Anaeleza umahiri wa ngoma hiyo kule kwao Lushoto kwamba, kihistoria huchezwa zaidi nyakati za usiku. Huku akisita kueleza kwa nini huchezwa usiku, na kusita kujibu kama ngoma hii ina madhara kwa uchezaji wa usiku. Jamii nyingi za makabila hutumia fursa hiyo ya usiku kujipatia wachumba ‘haramu’ au tuseme wapenzi.

Anasema kwao ni sawa kulinganisha na Wakongomani na Ndomboro. Ni ngoma ambayo inachezwa sio tu nyakati za harusi na sharehe za kitaifa bali ni ngoma inayochezwa mbele ya chifu wa Kisambaa kwa mujibu wa Asia ni Mkunga. Mbele ya kiongozi wa kitongoji huwa ni wakati wa sherehe maalumu.

Kikubwa kinachovutia watazamaji wa ngoma hii, ni jinsi mavazi yao rasmi yanavyovutia. Ni vibwaya, kofia ya ukindu, kaniki au khanga; wanajifunga na kunengua viuno kimahiri, wachezaji wakinengua kwa kunepa kiuhodari, wakinepa, mbele, nyuma na kiupande wakiongozwa na kiongozi aliyeshika filimbi kwenye mduara.

Kwa kweli panakuwa hapatoshi, hatumwi mtoto dukani kwani shughuli zinakuwa pevu! Kama uhondo ni huo, yanini kuendeleza ya wenzetu wakati zetu zinapendwa na wageni? Mpenda cha wenzake mara nyingi ni mtumwa!

Katika moja ya nyimbo za msanii wa muziki wa dansi nchini, marehemu Eddy Shegi, akiwa na bendi yake ya Washirika (Watunjatanjata), mpini wa solo ukiongozwa na Hamza Kalala (Kamandoo), alikuja na wimbo wa Kisambaa, uliojulikana kama, ‘’Shakaza’’.

Wimbo huo uliwatangaza Wasambaa sana enzi hizo. Ni wimbo wenye maudhui yanayoelezea kuchakaa kwa mavazi ambayo mwanamke aliyeachwa nyumbani wakati mume ametoka kwenda mbali kutafuta kazi. Mke anabaki amechoka kwa mengi ikiwa ni pamoja na kuendelea kuvaa nguo zilizochakaa na kupasukiwa kwa sana.

Mwanamke anakuwa amechakaa na kumlilia mume wake arudi hali yake ni zaidi ya kuchoka na kuchakaa. Maneno haya yanapoimbwa Kisambaa huku mdumange ukipigwa mambo huwa mazuri katika utamaduni wa Mtanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here