Na Yisambi Mbuwi
UKWELI ni kwamba, kila mtu anaweza kupata matatizo ya Kisaikolojia, bila kujali umri, jinsia, masikini wala tajiri. Matatizo ya Kisaikolojia yanahusisha mabadiliko ya kihisia, mabadiliko ya kifikra na mabadiliko ya kitabia kwa kufupi tunaweza kusema, Saikolojia ni namna akili inavyofanya kazi na jinsi inavyoweza kuathiri tabia ya mtu.
Mtu anaweza kupata matatizo ya Kisaikolojia kutokana na changamoto tunazo kumbana nazo katika utafutaji na uendeshaji wa maisha ya kila siku ambayo husababisha watu kupata misongo ya mawazo, inayosababishwa na masuala ya uchumi kupanda au kushuka, kufukuzwa makazini kutokakana na utovu wa nidhamu au changamoto zingine; ukosefu wa ajira na mishahara isiyokidhi mahitaji.
Sababu nyingine ni majanga ya moto, mafuriko, kuondokewa na watu wao wa karibu kama vile mke mme au mpenzi, ajali, migogoro ya ndoa, migogoro ya familia, migogoro ya ardhi, kusalitiwa, kufanyiwa ukatili na mengine kadha wa kadha ambayo yanaweza kusababisha matatizo ya Kisaikolojia na magonjwa ya akili kama vile sonana, mkazo wa mawazo, n.k.
Hivyo watu wengi hawajui ni wakati gani wanahitaji kupata Saikolojia tiba, ni wakati gani wanahitaji kuwatafuta wataalamu wa Saikojia ili kupata msaada hasa wanapopitia changamoto katika maisha badala yake watu wengi wanaamua kuchukua maamzi magumu kama vile kujichukulia sharia mkononi, kujiingiza katika maswala ya uraibu wa madawa ya kulevya, uvutaji wa bangi na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Kuna watu wamejiingiza kwenye makundi na tabia hatarishi pasipo kujitambua kwa sababu ya kukosa msaada wa Kisaikolojia, na wakati mwingine kutokujua aina ya changamoto aliyo nayo na namna inavyoweza kutibiwa na kutokufahamu kuwa changamoto yake inahitaji matibabu ya Kisaikolojia.
Kutokana na kutokufahamu aina ya changamoto aliyo nayo na namna inavyoweza kutibika, wengi huchukua hatua ya kuomba ushauri marafiki zao, wenza wao au ndugu zao wa karibu, aidha kwenda kwa watalaam wa tiba asili, viongozi wa dini bila kupata mafanikio ya ufumbuzi wa changamoto zao kitu ambacho huongeza ukubwa au usugu wa tatizo, ambapo badala ya kutatua tatizo, huongeza msongo wa mawazo.
Ni dhahiri, mtu akijisikia maamivu ya kichwa, maumivu ya mwili, maumivu ya tumbo na viongo vingine ndani ya mwili huwa anaenda hospitali kutibiwa na wengine kwenda maduka ya dawa kwa ajili ya kununua dawa za kutuliza maumivu au kutibu kabisa, lakini ni mara chache kuona mtu akienda kwenye vituo vya afya au hospitali kutafuta matibabu ya Kisaikolojia; vinginevyo awe ameelekezwa na daktari awaone watalaamu wa Saikolojia.
Hii inaashiria kuwa, yawezekana watu wengi hawatambui uwepo wa matibabu au huduma za Kisaikolojia, namna matibabu yanavyo patikana, uchache wa watalaamu au ukosefu wa watalaamu wa Saikolojia katika huduma za afya au taasisi mbalimbali, kutokutambua umuhimu wa Saikolojia tiba, kutokupewa kipaumbele kwa watalaamu wa Saikolojia kuwepo katika vituo na taasisi mbalimbali kama ilivyo kwa watu wa Tehama, wanasheria, watu wa ustawi wa jamii na kada zingine, upatikanaji wa wasaikolojia na sababu nyingine kadha wa kadha badala yake watu wengi wanakufa na tai shingoni au kufanya maamzi yasiyo sahihi.
Hivi sasa imekuwa ni kawaida kusikia na kushuhudia matukio mengi ya kutisha, kushangaza na kusikitisha katika jamii zetu, ikiwa ni pamoja na watu kujinyonga, kunywa sumu, kuua wenzi wao, na matukio mengine yanayo husisha ukatili wa kijinsia, ulawiti, ukandamizaji, mauaji ya kutisha, mmonyonyoko wa maadili na mengine mengi ambayo hayaripotiwi katika vyombo vya habari.
Aidha, matukio mengine hayaelezeki kabisa, lakini ukifuatilia kwa undani, yote haya yametendeka kutokana na kuwa muhusika au mtuhumiwa alikosa msaada wa Kisaikolojia (saikolojia tiba) kabla hajatekeleza tukio hilo.
Tambua kwamba, siyo kila maumivu yanahitaji umeze dawa, wala si kila ugonjwa lazima upone kwa kumeza dawa hasa magonjwa yanayohusu mfumo wa akili na tabia. Kuna baadhi ya maumivu na magonjwa yanaweza kutibika kwa kupata Saikolojia tiba kutoka kwa wataalam wa Saikolojia bila hata kumeza dawa yoyote, lakini pia kuna muda unatakiwa umeze dawa na upate matibabu ya Kisaikolojia.
Ieleweke kwamba, magonjwa mengi ya akili yanahitaji matibabu ya aina tatu; yani matibabu ya kijamii, matibabu ya kibaiolojia na matibabu ya Kisaikolojia, japo kuna baadhi ya changamoto za akili mtu akiwahi mapema kuwaona watalamu wa Saikolojia anaweza kutibiwa bila hata kumeza dawa.
Watu wengi wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo unao sababishwa na changamoto ya maisha ya kila siku, migogoro ya ndoa isiyokwisha, wengine kushindwa kufanya vizuri kwenye tendo la ndoa, upungufu wa nguvu za kiume, kuhisi maumivu ya mwili yasiyoelezeka, kukosa usingizi bila sababu na kujihisi upweke.
Sababu nyingine ni kukata tamaa ya kuishi, kupata hali ya hofu au wasiwasi na woga usio na tija, kupata maumivu ya chembe ya moyo, hata mda mwingine kuwa na mawazo ya kujiua na kila wakienda hospital kupimwa vipimo havionyeshi ugonjwa wowote hivyo wengine huamua kutafuta tiba asilia na wengine kuwafuata viongozi wa dini kwa ajili ya maombezi.
Hata hivyo, licha ya jitihada hizo bado hawapati suluhisho la changamoto husika pasipo kujua kuwa, kuna baadhi ya changamoto au maumivu yanasababishwa na mfumo wa akili inavyo fanya kazi, hivyo matibabu yake ni ya Kisaikolojia tu bila hata kumeza dawa.
Ni wakati gani sasa unahitaji kuwaona wataalamu wa Saikolojia kwa ajili ya kupata Saikolojia tiba? Ukiona mabadiliko haya katika mwili wako au kuona dalili zifuatazo fika vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu ya Kisaikolojia au watafute wataalamu wa Saikolojia tiba.
Kwanza; Kupata msongo wa mawazo ambao akili yako inashindwa kupata suluhu na namna kukabiliana na msongo wa mawazo kwa muda mrefu. Pili, kupata maumivu yasiyoelezeka mwilini muda mwingine hata ukimeza dawa hayaponi au ukifanya vipimo ugonjwa hauonekani ikiwemo kupata maumivu ya kichwa kisicho sikia dawa kwa muda mrefu.
Tatu, kukosa usingizi zaidi ya siku tatu na kuendelea bila sababu. Nne, upata hali ya hofu, wasiwasi na woga uliopitiliza, wakati mwingine ni wasiwasi usio na tija. Tano; Kupata hasira zisizo kuwa na sababu za msingi. Sita, kukata tamaa, kujichukia, kujihisi tofauti, au kuhisia watu wengine tofauti.
Saba, kuwa na mawazo ya kujiua, kuua wengine au kupotea, kuwa na fikra hasi muda wote au mawazo mabaya yanayoashiria hatari. Nane, kujihisi mwenye hatia bila sababu, kukosa raha na kuwa na hali ya huzuni isiyoelezeka iwapo umefanyiwa tendo la kikatili, kama vile kubakwa, kulawitiwa, kunyanyapaliwa, na hata kushuhudia matukio ya kikatili au ya kutisha kama vile kuuawa kwa mtu, kushuhudia mfululizo wa ajali mara kwa mara na matukio mengine yanayoogopesha.
Hayo ni machache tu kati ya mengi yanayo haribu Saikolojia ya binadamu, lakini ukiona una dalili hizo hapo juu au zinazoendana na hizo, tafuta msaada wa Kisaikolojia haraka kabla hujafikia hatua mbaya.
NB;- Kumbuka afya ya akili ni kiungo kikubwa katika mfumo mzima wa mwili wa binadamu kiasi kwamba, ukipata changamoto kwenye afya ya akili kila kitu kitabadilika ikiwa ni pamoja na mwonekano, kufikiria, kutenda na hata namna ya kuishi inaweza kubadilika ikiwa ni pamoja na ufanisi wa kufanya kazi ofsini au kazi zako binafsi, namna ya kujamiiana na watu, hamu ya kula au kufanya shughuli zingine, kushindwa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu pamoja namabadiliko ya kihisia.
Ushauri wangu kwa jamii na Serikali kwa ujumla, kutokana na ongezeko la magonjwa ya akili na matatizo ya Kisaikolojia nchini, ni muhimu kila mtu atambue nafasi yake katika kulinda na kutunza afya yake ya akili, lakini pia pale anapohisi kupata changamoto ya Kisaikolojia atafute msaada wa kisaikolojia.
Aidha, Serikali na Taasisi zingine zisizo za Kiserikali zielekeze nguvu katika kukabiliana na magonjwa ya akili ikiwa ni pamoja na kuajiri madaktari wa kutosha waliobobea katika maswala ya afya ya akili watalaamu wa Saikolojia wa kutosha katika taasisi na sekta mbali mbali kama vile mashuleni, vituo vya afya, na taasisi zingine zinazo husisha mikusanyiko ya watu zaidi ya kumi na kuendelea ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu magojwa ya akili.na matatizo ya Kisaikolojia. Kumbuka afya ya akili ndo mtaji namba moja wa kumsaidia mtu afanye kazi kwa ufasaha na ufanisi.
*Mwandishi wa Makala hii ni Mwanasaikolojia kutoka hospitali ya Kanda ya rufaa Mbeya, Idara ya afya ya akili, kitengo cha Saikolojia tiba. Barua pepe;- mbuwiyisambi@gmail.com. Simu:- +225744947026//0682807859.